unaikumbuka hii?
haya tuburudike kidogo basi.
SIZITAKI MBICHI HIZI
1. Hadithi inayokuja, ni ya Sungura sikia,
Hadithi uliyongoja, leo ninakuletea,
Alitoka siku moja, njaa aliposikia,
Njaa aliposikia, Sungura nakuambia.
2. Siku ile akaenda, Porini kutembelea,
Akayaona matunda, mtini yameenea,
Sungura akayapenda, mtini akasogea,
Mtini akasogea, Sungura nakuambia.
3. Sungura karukaruka, lakini hakufikia,
Matunda hakuyashika, mikononi hakutia,
Hakika alisumbuka, nguvuze zikapungua,
Nguvuze zikapungua Sungura nakuambia.
4. Mtazame hapo juu Sungura amelegea,
Mtazame na miguu, matunda anarukia,
Atafanya sikukuu, matunda akifikia,
Matunda akifikia, Sungura nakuambia.
5. Karuka tena karuka, matunda akarukia,
Mwisho wake akachoka, kachoka hata mkia,
Penye mti akatoka, pembeni akasogea,
Pembeni akasogea, Sungura nakuambia.
6. “Sizitaki mbichi hizi” Sungura akagumia,
“Naona nafanya kazi, bila faida kujua”,
Yakamtoka machozi matunda akalilia,
Matunda akalilia, Sungura nakuambia...
No comments:
Post a Comment