Friday, November 11, 2011

UTOVU WA NIDHAMU KWA WALIMU

Na Kokuteta Mutembei
SEKTA ya elimu katika Tanzania imekua kwa kasi sana, hasa ongezeko la shule za umma na binafsi. 
Ongezeko hili la shule za awali, msingi na sekondari limesaidia kuziba pengo ambalo lilionekana la ukosefu wa shule za kustosha nchini  na kwa baadhi ya shule hizi, kiwango cha elimu kinachotolewa kinakidhi viwango vya taifa.
Kama taifa tunapaswa kujivunia suala hili  na hili tumeshalidhihirisha katika ripoti mbalimbali za nchi kuhusu maendeleo na ustawi wa Watanzania. 
Lakini, vile vile kuna kasoro kubwa ambazo zinajitokeza na tunapaswa tuangalie ni kwa kiasi gani kuna ufuatiliaji wa karibu kwa upande wa Serikali katika kukabili changamoto zinazoendana na ongezeko hili.
Kuna suala moja ambalo linajitokeza katika shule mbalimbali za Serikali na binafsi za awali, msingi na sekondari, na hili linahusiana na ubovu wa maadili ya walimu na utovu wa nidhamu na  jinsi ubovu huo unavoathiri maendeleo na makuzi ya watoto kisaikolojia, kimwili, kiroho na kiakili.  
Inawezekana kwamba kutokana na ufuatiliaji hafifu wa Serikali katika kuhakikisha kwamba shule hizi zina walimu wanaokidhi viwango vilivyoweka kitaifa na kimataifa kuna  upungufu mkubwa ambao matokeo yake ni hasara kwa mtoto, mzazi na taifa kwa ujumla.
Wakati wazazi na walezi tuna imani kwamba shuleni mtoto atapata elimu na malezi ya msingi akiwapo mazingira ya shule, ukweli ni kwamba zipo shule ambazo zimegeuka uwanja wa fujo, hakuna kinachoendelea zaidi ya uharibifu wa watoto, kisaikolojia, kimwili, kiroho na kiakili.
Wakati tunajisifu kwamba kuna idadi kubwa ya watoto ambao wamesajiliwa katika shule za msingi na ongezeko kubwa ya watoto hao  wanaoenda shule za sekondari, ukweli ni kwamba tumeshindwa kuhakikisha kwamba watoto hao wanaingia katika mazingira ambayo ni salama na yatawajenga kielimu na kimalezi. 
Katika upungufu huu wa ufuatiliaji kwa upande wa Serikali, ipo haja ya wazazi na walezi kutupia jicho shule zote zilizopo karibu nasi kubaini ni nini kinachoendele na pale inapoabinika kwamba watoto wanatendewa visivyo, kuchukua hatua za haraka kunusuru maisha ya watoto wetu kwa kutoa ripoti sehemu husika.
Ripoti ya mwaka 2011 ya ukatili dhidi ya watoto ya Tanzania imeonyesha wazi kwamba suala la watoto kutendewa ukatili mashuleni lipo na linaongezeka. 
Kati ya watoto wote walioulizwa wametendewa na nani ukatili, asilimia 51.2 walijibu ni watu wanaowafahamu, wakiwamo walimu wao. 
Ripoti pia inabainisha kwamba asilimia 15 ya watoto wa kike wanafanyiwa ukatili wa kimapenzi wakiwa shuleni, ikimaanisha kwamba wanafanyiwa na walimu wao hasa wa kiume. 
Tuliangalie suala hili kwa makini sana.  Walimu wa kiume wanakuwa ni tishio kwa maendeleo ya elimu ya mtoto wa kike na pengine hata wa kiume kwa idadi kubwa tu maana hili la watoto wa kiume linafanywa katika hali ya maficho zaidi. 
Ipo haja kwa Serikali na wazazi  kufuatilia kwa karibu sana kinachoendelea katika shule zetu. Ripoti inabainisha kwamba kati ya kila watoto kumi, mmoja amefanyiwa ukatili wa kingono na mwalimu wake.
Mpaka hali inafikia hivi, Serikali, Chama cha Walimu (CWT), jamii na wadau wengine wako wapi? CWT imekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya walimu, na hii ndio desturi ya vyama vya walimu kote duniani. 
Nchini Tanzania, CWT imeweza kufanikiwa kuleta mabadiliko kwa kiasi kwa upande wa maslahi ya walimu, bado changamoto ni nyingi,  zikiwamo changamoto ndani ya chama chenyewe. 
Ila, changamoto kubwa inayokikabili chama hiki ni sura ya walimu wa leo na uwezo wao hafifu wa kufundisha pamoja na tatizo la mmomonyoko wa maadili. 
Chama hiki hakina budi kuchunguza mwenendo wa wanachama wake na kubaini kama kweli wana sifa stahili za kuwa walimu.
Pia,   ifuatilie kwa ukaribu suala la ukatili wa kingono unaofanywa na walimu wa kiume kwa wanafunzi. 
Chama cha walimu ni muhimu kitudhihirishie kwamba ni chama kinachozingatia sio tu stahiki za walimu, lakini wajibu wao katika kuelimisha na kulea watoto wakiwa shuleni. 
Suala hili sio la Serikali peke yake kwa maana ni dhahiri kwamba hili linajitokeza kutokana na upungufu katika ufuatiliaji, wazazi, walezi, wanajamii ni lazima tuchukue jukumu la kusimamia haki za watoto wetu na kuchukua hatua zinazostahili, tusiache tatizo hili liendelee.

 

No comments: