Friday, November 4, 2011

MIAKA 50 YA UHURU NA CHANGAMOTO ZA MITAALA

Na Mdau, Fredy Azzah
ZUNGUMZA na mdau yoyote wa elimu, hatosita kutaja mabadiliko ya mara kwa mara ya mitalaa kama mojawapo ya chanzo cha kushuka kwa kiwango cha elimu.
Hiki ndicho pia kimekuwa kilio cha walimu wengi nchini ambao pamoja na kupinga mabadiliko hayo ya mara kwa mara wanaishukia Serikali kwa kushindwa kuwandaa namna ya kukabiliana na mabadiliko hayo.
“Haiwezekani kufanya mabadiliko katika jambo lolote  bila kuwashirikisha walengwa. Kitendo cha kubadilisha mitalaa bila ya kuwashirikisha walimu ni hatari kwa taifa,  maana walimu watakuwa wanafundisha mambo wasiyoyaelewa na wanaoathirika zaidi ni wanafunzi,”anasema mwalimu Jamali Maringo.
Sauti ya Maringo  anayefundisha katika Shule ya Sekondari ya Kiislamu ya Ubungo ya jijini Dar es Salaam, inawakilisha maoni na mtazamo wa maelfu ya walimu nchini ambao ukizungumza nao hawasiti kutaja mabadiliko ya mitalaa kama jambo linalowakwaza katika utendaji wao.
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ndicho chombo kinachosimamia utungaji na utekelezaji wa mitalaa ya elimu ya msingi, sekondari na mafunzo ya ualimu.
Katika makala haya,  Mkurugenzi Mtendaji wa TET, Dk Paul Mushi anaeleza historia ya mabadiliko ya mitalaa na changamoto wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa mitalaa hiyo.
Kwa mujibu wa Dk Mushi, tangu Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961, mabadiliko ya mitaala yamefanyika mara mbili ambayo ni mabadiliko ya miaka ya 1960 yaliyofanyika kubadili mfumo na filosofia ya elimu kutoka ile ya kikoloni kwenda filosofia mpya ya Elimu ya Kujitegemea.
Sambamba na hili, mwaka 1966 masomo ya Biolojia, Kemia na Fizikia yaliiingizwa katika mtalaa wa elimu ya sekondari kuchukua nafasi ya somo lililoitwa ‘General sciences’ lililokuwa likifundishwa wakati wa  ukoloni kwa lengo la  kujenga uelewa baina ya nadharia na vitendo.
Mabadiliko ya pili kwa mujibu wa Dk Mushi  yalifanyika mwaka 1992 na 1993 kufuatia mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa yaliyoikumba nchi tangu miaka ya 1980.   .
Katika kipindi hicho, ilishuhudia Tanzania ikibadili mfumo wa siasa kutoka mfumo wa chama kimoja kwenda ule wa vyama vingi, huku sekta ya uchumi nayo ikibadilika kutoka katika mfumo wa udhibiti wa Serikali kwenda ule wa soko huria. Ni kipindi hiki ambacho masomo ya shule za msingi yalipunguzwa kutoka masomo 13 hadi tisa.
Kuhusu uboreshaji wa mitalaa, anasema zoezi hilo hufanywa ndani ya mzunguko mmoja au baada ya mzunguko mmoja wa mtaala (curriculum cycle) kwa lengo la kufanya masahihisho na kuingiza masuala muhimu yanayotokea katika jamii kwa wakati huo.
Kwa mfano anasema, uboreshaji wa mitalaa wa mwaka 1963, ulilenga  kuwatayarisha Watanzania kupata elimu bora tofauti na ile ya zamani iliyokuwa na mtazamo wa kukidhi mahitaji ya wakoloni.
Hata mwaka 1972 uboreshaji mwingine ulipofanyika wa kuingiza masomo ya Biashara, Sayansi Kimu, Ufundi na Kilimo, lengo lilikuwa kutekeleza mpango wa Siasa ni Kilimo katika shule.
Mwaka 1976 mtalaa ukaboreshwa tena  kwa kuingiza masuala ya Azimio la Arusha lililopigia cahpuo Elimu ya Kujitegemea  na  matakwa ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Mtalaa huo ulilenga kuhakikisha kila mtoto anayemaliza elimu ya msingi,  anakuwa na uwezo wa kujiajiri kwa kutumia ujuzi aliopata shuleni na rasilimali zilizopo katika jamii inayomzunguka.
Mwaka 2005 anasema kulifanyika uboreshaji mwingine uliosisitiza kile kinachojulikana kitaalamu kwa jina la ‘Muhamo wa Ruwaza’ ambao ni mfumo unaomjengea mwanafunzi uwezo wa kujitafutia maarifa.
Mwaka 2006 Serikali ililazimika kufanya uboreshaji  wa mtalaa wa sekondari kwa  kurudisha utaratibu wa masomo ya Physics na Chemistry baada ya kupokea malalamiko  kutoka kwa wadau waliopinga utaratibu wa kuyaunganisha masomo hayo na kuwa somo moja.Pia katika uboreshaji huo, masomo ya michepuo yalirudishwa.
Aidha, mwaka 2007 mtalaa wa Ualimu ngazi ya Stashahada,  uliboreshwa kwa Serikali kuamua wanafunzi kutumia mwaka mmoja chuoni na mwaka mwingine katika mazoezi shuleni.Lengo la uboreshaji huu, lilikuwa kupunguza uhaba wa walimu shuleni.
Uboreshaji wa mtalaa wa Ualimu ukafanyika tena mwaka 2008 kwa kuhusisha ualimu wa ngazi ya cheti ambapo suala la ujuzi   (competence) ndilo lililosisitizwa.
Mabadiliko hayo yalienda sambamba na kuondoa maudhui yaliyopitwa na wakati na kuweka maudhui mapya yanayoendana na wakati katika jamii yakiwemo masuala mtambuka kama ugonjwa wa Ukimwi, usawa wa kijinsia, mazingira, masuala ya umaskini na rushwa.
Mwaka 2009 mtalaa wa elimu ya sekondari kwa kidato cha tano na sita uliboreshwa, lengo likiwa
kuingiza ujuzi ambao wanafunzi husika wanategemewa kujengewa kupitia  mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji.

No comments: