Tuesday, November 1, 2011

IJUE WILAYA YA SENGEREMA KIELIMU (kutoka kwa watu wa sengerema)

Sengerema ni kati ya wilaya nane za Mkoa wa Mwanza, ilizinduliwa rasmi mwaka 1975. Wilaya hii imejikita sana katika masuala ya elimu. Kulingana na takwimu za hivi karibuni Wilaya ya Sengerema ina jumla ya shule za msingi 164 kati ya hizo 2 ni za watu binafsi. Shule za awali zinafikia 172, za serikali zikiwa 159 na za watu binafsi ni 13. Shule za sekondari ziko 29 za serikali ni 21 na binafsi ni 8. Wilaya hii inavyo vituo 7 vya Walimu.

Wilaya hii inayo malengo kadha wa kadha ya kuboresha elimu. Malengo hayo ni pamoja na kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi kutoka asilimia 42 hadi asilimia 50, kuongeza ufaulu wa darasa la nne kutoka asilimia 67 hadi 80, kuandikisha watoto wote wenye umri wa kuanza shule yaani miaka 5-6 kwa shule za awali, na miaka 7 ya Elimu ya msingi kwa asilimia 100.

Malengo mengine kwa mujibu wa taarifa ya elimu ya Wilaya ni pamoja na kuhamasisha jamii kutumia nguvu zao ili kujenga vyumba vya kutosha vya madarasa, nyumba za walimu, maktaba, vyoo, pamoja na kutengeneza madawati kwa ajili ya elimu bora na kujengea jamii uwezo wa kupanga, kutekeleza, kusimamia, kufuatilia na kutathimini programu ya MEMKWA.

Sengerema pia katika suala zima la kuboresha elimu, imejikita katika utunzajia na ununuzi wa vitabu na zana za kufundishia shuleni, kutoa semina za mara kwa mara ili kupata walimu bora kwa taaluma bora kila shule na kutoa mafunzo kwa walimu wa daraja la IIB/C ili kuwa IIIA. Haya yote ni malengo ya muda mfupi.

Malengo ya muda mrefu ni pamoja na ujenzi wa sekondari kila kata, kujenga maktaba kila shule, uimarishaji wa vikundi vya MUKEJA, kujenga vituo vya walimu na kuwaendeleza walimu wa IIIA kuwa Stashahada au Shahada.

Ili kuboresha elimu wilayani Sengerema, imebuniwa pia mikakati ya kuinua taaluma na kupunguza utoro shuleni.

No comments: