Friday, November 4, 2011

JOHO LA UHITIMU - VAZI LILILOPOTEZA HADHI YAKE


Na Mdau wa Elimu 

KATIKA hatua yeyote ya kupata elimu, siku ya uhitimu huwa ni maalumu na yenye hadhi yake kwa wahusika.
Kwa kawaida, kumekuwepo na vitambulisho vinavyotoa heshima kwa wahimu. Kwa mfano, ukitoa cheti, heshima nyingine anayopata mhitimu, ni lile joho analovaa, vazi linalomtambulisha kuhusu aina ya uhitimu alioufikia.
Pamoja na mabadiliko ambayo sidhani kama itakuwa sahihi kuyaita ya kimaendeleo, umezuka mtindo wa kila taasisi hata zinazotoa elimu ya chekechea kuwavisha majoho wanafunzi wao wakati wa mahafali.
Hata hivyo ukweli unabaki  pale pale kuwa joho la uhitimu, si vazi la kawaida.Ni vazi la heshima na lenye kubeba hadhi ya uhitimu wa elimu ya juu na si vinginevyo.
Kwa mantiki hiyo,  mwenendo mpya wa kila mtu kuvaa vazi hili, umepunguza  hadhi na haki kwa joho kuvaliwa na wahitimu wa kiwango cha elimu ya juu kama shahada na stashahada.  Ieleweke kuwa, joho hili la kielimu lina maana na umuhimu wake katika utamaduni wa kielimu, si kwa Tanzania tu, bali duniani kote.

Katika sekta ya  elimu, elimu ya juu ni nyanja muhimu na nyeti kwa jamii.  Kuhitimu stashahada au shahada katika taasisi za elimu ya juu hufungua milango katika nyanja nyingi na muhimu kwa maendeleo ya jamii. Nyanja hizo ni pamoja na udaktari, ualimu, siasa, uchumi, uanasheria na nyinginezo.

Lakini ikumbukwe kuwa sio rahisi kwa kila mtu kufikia hatua hiyo, ni lazima anayesomea elimu hiyo ajitume kwa kadri awezavyo na wakati mwingine kujinyima baadhi ya haki zake ili mradi tu aweze kuhitimu nyanja hiyo.
Ndio maana akishahitimu, moja ya faraja kwake ni kuvaa joho ambalo wengine hawakuweza kupata nafasi hiyo. Kulifanya   livaliwe ovyo ovyo, kunapunguza faraja hiyo na hata msukumo wa kusoma.

Kwa mfano, katika kiwango cha chuo kikuu ambayo ndiyo ngazi ya juu zaidi kielimu kote duniani, digrii   ni cheo au ngazi ambayo mwanafunzi msomi hukubaliwa kuwa nayo kwa dhana ya kutambua maarifa yake iwe  ni shahada ya kwanza, shahada ya Uzamili, au shahada ya Uzamivu.

Digrii ni jina lililowekwa na vyuo kama utambuzi wao maalum kwa wanafunzi kumaliza kozi ya masomo au kwa upatikanaji wa maarifa fulani kupitia elimu ya chuoni.

Ili msomi mhitimu wa mafunzo ya digrii atambulike hivyo, huwepo siku maalumu ambayo mhusika hupewa cheti na kuvaa vazi hili linalomtambulisha aina ya kozi ama taaluma aliyosomea.

Aidha, kila taasisi ya elimu ya juu duniani ina utamaduni na utaratibu wake wa aina ya joho la kielimu wanalolitaka litambulishe taasisi husika, aina ya shahada au vitivo vya masomo kama vile sheria, uhandisi, sanaa na vinginevyo.

Kihistoria, joho hili la kielimu limepitia mabadiliko na mageuzi kadhaa kutoka katika nguo za kawaida zinazovaliwa na mwanadamu. Kwa mfano, awali joho hili lilikuwa ni gauni refu lililotumika kama koti la juu na wasomi wa zamani.Sambamba na koto hili, kulikuwa na kofia iliyotumika kama mfuniko wa kichwa.


Kwa miaka mingi sasa, joho hili limekuwa likivaliwa na wahitimu wa digrii na wale wa elimu ya juu kwa jumla.

Kimsingi, kila taasisi mpya ya elimu ya juu duniani huchagua aina ya joho lake la heshima kipindi cha kupokea hati au mkataba wa kutoa elimu.Vazi hili hupaswa kuwa ni la kipekee likiipambanua taasisi hiyo na nyinginezo.

Kwa mfano, aina ya majoho  yanayovaliwa na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro ni  tofauti na yale yanayovaliwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine ambacho nacho kipo Morogoro.

Hali kadhalika, majoho ya Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM) ni tofauti na yale   yanayovaliwa katika Taasisi ya Ufundi Dar es Salaam (DIT). Na ndani ya  taasisi moja, majoho haya  yanaweza kuwa  tofauti kulingana na ngazi na fani aliyoihitimu mtu.


Kuna taratibu zinazowekwa na taasisi  kupambanua aina ya vitambaa ambavyo vitatumika kutengenezea majoho yao. Kwa mfano, mara nyingi tawala za taasisi hizi, huchagua  vitambaa vya hariri kwa majoho na kofia.

Lakini uchaguzi wa aina ya vitambaa na rangi yake haufanywi kiholela, kuna maana maalum kama vile rangi fulani kwenda sambamba na aina ya digrii.
Pamoja na kuwa vazi hili maalumu huvaliwa kwa siku moja tu, thamani yake ni kubwa kwa vile ni wachache wenye kupata nafasi ya heshima kuvaa vazi linaloonyesha kiwango chao cha maarifa walichopata.

Ni muhimu basi kulinda hadhi ya kielimu na heshima ya wanaopaswa kuvaa joho hili kwa kuendelea kulifanya kuwa ni vazi maalumu, kwa wakati maalumu na kwa watu maalumu.

Itakuwa ni kuzishusha hadhi taasisi zetu za elimu ya juu pamoja na wahitimu wanaostahili kulitumia vazi hili katika kupewa heshima yao ya kutunukiwa kwao digrii zao kama vazi hili litaachwa litumike au kuvaliwa na wanafunzi ambao hawajafikia kiwango cha heshima hiyo.

Joho hili la kielimu liendelee kupambanuliwa na mavazi mengine yanayovaliwa na taasisi zingine zenye kutoa elimu ya kawaida, taasisi ambazo tangu awali hazikuwa na utamaduni wa uvaaji wa mavazi haya maalumu

No comments: