Saturday, January 25, 2014

matokeo ya kidato cha pili ni hatari



SHARE THIS STORY
0
Shar
Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakisubiri matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013, imebaini kuwa Serikali imetoa agizo kwamba wanafunzi wote waliofeli mtihani huo kuendelea na masomo ya kidato cha tatu, huku wakisoma mafunzo ya kurudia mtihani wa kidato cha pili., imebainika kuwa waliofaulu mtihani huo uliofanywa Oktoba 7 hadi 21 mwaka jana ni asilimia 62 tu, asilimia 31 wakitakiwa kukariri (kurudia) kidato cha pili mwaka huu, huku asilimia saba wakishindwa mtihani huo kwa mara ya pili.
Jumla ya wanafunzi 531,457 walitajwa na Wizara ya Elimu mwaka jana kuwa watafanya mtihani huo.
Uamuzi huo wa Serikali ni tofauti na ule uliotolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa Novemba 4, mwaka 2012, kwamba kuanzia wakati huo mtihani wa kidato cha pili utakuwa ni wa mchujo na kwamba atakayefeli atatimuliwa.
Dk Kawambwa alisema matokeo ya mtihani wa kidato cha pili yatatumika kama kigezo cha kuchuja na kukariri kidato cha pili kwa watahiniwa watakaoshindwa kufikia wastani wa ufaulu wa alama 30.
Alisema mtahiniwa ataruhusiwa kukariri kidato cha pili mara moja tu na endapo mtahiniwa atashindwa mtihani kwa mara ya pili kwa mwaka utakaofuatia, itabidi aendelee na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi.
Gazeti hili limeiona barua iliyoandikwa Januari 16 mwaka huu na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kusainiwa na Katibu Mkuu wake, Profesa Sifuni Mchome, kwenda kwa wadau wa elimu nchini, wakiwamo maofisa elimu wa mikoa na Chama cha Wamiliki wa Vyuo na Shule Binafsi (Tamongsco).
Katika barua hiyo, wizara hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa wanafunzi watakaofeli mtihani huo, wanaendelea na masomo ya kidato cha tatu.
“Matokeo ya kidato cha pili yamepokewa na kufanyiwa uchambuzi ili kupata taswira ya taifa. Taarifa ya matokeo hayo imebaini kuwa watahiniwa waliofanya mtihani na kufaulu ni sawa na asilimia 62 tu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo na kuongeza;
“Hali hii inaonyesha kuwa asilimia 31 ya wanafunzi watatakiwa kukariri kidato cha pili, 2014. Wale walioshindwa kwa mara ya pili ambao ni asilimia saba wanatakiwa kuendelea na masomo nje ya mfumo rasmi.”
Barua hiyo inaeleza kuwa wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 na kuendelea waendelee na masomo ya kidato cha tatu mwaka 2014, wakati awali Serikali ilitoa tamko kuwa watakaoshindwa kufikisha alama 30 watatimuliwa.
“Wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 hadi 39 wapewe mafunzo rekebishi ‘Remedial class’ wakiwa kidato cha tatu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo

Wednesday, November 6, 2013

ELIMU YA TANZANIA SASA NI MZIGO USIOBEBEKA



Suala la kuporomoka kwa ubora wa elimu ya Tanzania na mfumo wake wa uendeshaji ni moja ya mambo yanayoendelea kutawala mazungumzo ya watanzania kwa sasa.

Kwa walio wengi, suala hili halina kificho tena kutokana na ushahidi mbalimbali, kama vile utata wa matokeo ya mitihani ya kitaifa ya kuhitimu masomo ya msingi na yale ya sekondari.

Tukichukulia kwa mfano, matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana, kati ya watahaniwa 431,650 waliofanya mtihani, watahaniwa waliofaulu kwa ubora , yaani daraja la kwanza hadi la tatu walikuwa 35,599 tu, sawa na asilimia nane.

Hii inamaanisha kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya watahaniwa hawakuwa na ufaulu wenye kiwango bora.

Ushahidi mwingine ni ule wa wanafunzi kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza wakiwa hawajui kusoma wala kuandika, kama ilivyoripotiwa katika baadhi ya mikoa ya Lindi, Dodoma na Shinyanga.

Kwamba mwanafunzi amesoma mwaka moja elimu ya ngazi ya chekechea na miaka saba elimu ya shule ya msingi, lakini hajui kusoma wala kuandika ni suala linalostajaabisha.

Lakini lingine lililoonyesha kuwepo kwa tatizo la kuporomoka kwa ubora wa elimu inayotolewa katika shule zetu, ni tafiti mbalimbali.

Shirika lisilo la kiserikali la Uwezo kwa mfano, ambalo limekuwa likitoa tafiti za ubora wa elimu katika nchi za Afrika Mashariki, yaani za Tanzania, Uganda na Kenya, limeonyesha namna Tanzania inavyozidi kuachwa nyuma kielimu.

Katika utafiti wake wa mwaka 2011 uliojumuisha nchi zote tatu, Uwezo liligundua kuwa wengi wa wanafunzi wa darasa la tatu ambao walipaswa kuwa na stadi za hesabu na kusoma kwa ngazi ya darasa la pili, hawakuwa nayo kwa nchi zote.

Utafiti ulibainisha kwa ulinganifu kwa nchi zote tatu, karibu wanafunzi wote wa darasa la saba kwa Uganda na Kenya, waliweza kufaulu majaribio yote ya ngazi ya darasa la pili waliyopewa.

Hali ilikuwa tofauti kwa Tanzania, kwani ni asilimia 50 hadi 80 ya wanafunzi wa darasa la saba, ndiyo waliweza kufaulu majaribio ya ngazi hiyo

Mifano hiyo mitatu inahalalisha sababu za kushuka kwa ubora wa elimu, kutawala sana katika mazungumzo ya watanzania na wadau wa elimu ya Tanzania, ikiwamo Benki ya Dunia (WB)

Serikali na wadau wa elimu hadi sasa hawajaweka bayana sababu za kuporomoka kwa ubora wa elimu kiutafiti.

Serikali nayo imekiri kushuka kwa ubora wa elimu inayotolewa na shule zake kupitia kwenye hotuba ya Waziri wa Elimu na Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa aliyoitoa Agosti Mwaka huu.

Dk. Kawambwa alikiri uwepo wa tatizo hilo wakati wa uzinduzi wa Utekelezaji wa mikakati ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya elimu, uliofanyika kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa Dk Kawambwa katika kutekeleza mpango huo wa serikali kwa sekta ya elimu, wizara yake iliwakusanya washiriki 34 kutoka taasisi 31 zikiwamo za serikali na zisizo za serikali, kwa lengo la kutafakari kwa kina changamoto zinazoathiri sekta hiyo.

“Changamoto kubwa iliyoanishwa na washiriki ni utambuzi kwamba, ingawa shule zimeongezeka na kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi vimeongezeka, ubora wa elimu unashuka, hususan kuporomoka kwa kiwango cha ufaulu katika elimu ya msingi na sekondari,” kwa mujibu wa Dk Kawambwa.

Kwamba waziri hakueleza dhahiri sababu ya kushuka kwa ubora wa elimu, na badala yake anaeleza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu na kuathiri utoaji wa elimu bora, inathibitisha ukubwa wa tatizo.

Alitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na uhaba wa walimu, uwezo mdogo wa walimu kufundisha, motisha kwa walimu, uwajibikaji wa walimu na watumishi wa sekta ya elimu.

Changamoto nyingine ni zile za upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, miundo mbinu isiyokidhi mahitaji, mapungufu katika usimamizi wa elimu ngazi ya shule, ufutiliaji na tathmini na uthibiti wa ubora wa shule.

Kilichonisukuma kuandika makala hii,ni  kutokana na utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia (WB) katika shule mbalimbali, kuangalia sababu za kushuka kwa ubora wa elimu nchini, mwaka 2010.

Matokeo ya utafiti huo ambao uliweka bayana moja ya sababu za kushuka kwa ubora wa elimu nchini, ulifafanuliwa na Mtaalamu  Kiongozi wa benki hiyo, upande wa Elimu wa Maendeleo ya Rasilimali Watu,Kanda ya Afrika, Arun Joshi.

Ilikuwa ni kwenye mazungumzo maalumu aliyoyafanya Joshi na gazeti la Nipashe, wakati wa hafla iliongozwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Rasiliamali Watu wa WB, kanda ya Afrika, Ritva Reinikka.

Hafla hiyo ilitumiwa na WB kutangaza kutenga kiasi cha shilingi bilioni 162 kwa miaka minne kuanzia 2014 hadi 2018 kwa ajili ya kuchagiza mpango wa serikali wa BRN, kwa upande wa sekta ya elimu.

Akizungumzia utafiti huo,Joshi alisema uligundua kuwa walimu wanatumia muda kidogo sana wa kufanya kazi ya kufundisha.

“Utafiti wetu uligundua walimu wanatumia muda wa wastani wa saa mbili na dakika nne tu za kufundisha, tofauti na saa tano zinazotakiwa kwa kutwa nzima,” kwa mujibu wa Joshi.

Anasema kwa shule zilizo mjini, hali ni mbaya zaidi, kwani huko walimu wanatumia saa moja na ushee, ukilinganisha na wale wa shule zilizo vijijini.

Josh anasema utafiti umegundua kuwa saa nyingi zinatumiwa na walimu kufanya shughuli zingine zisizokuwa na uhusiano na taaluma wakati wa kazi, wakati mwingine wakiishia kupiga soga, kiashirio kimojawapo cha kutokuwa na morali wa kufundisha.

“Hapa ndipo penye tatizo la msingi kwa sababu ikiwa walimu hawafundishi kwa mujibu wa muda unaotakiwa, huwezi ukatarajia ubora ukaongezeka ila ni yumkini kwamba utashuka tu,” anasema.

Anasema hali hiyo ndiyo iliyosababisha waone umuhimu wa kuchagiza jitihada  za serikali, kwa kutoa fedha zitakazotumika kugharamia pamoja na mambo mengine, mafunzo zaidi ya walimu wa shule za msingi pamoja na kuwamotisha ili wafundishe kwa muda wote unaotakiwa.

Ni muda mrefu sasa wadau wamekuwa wakitaja sababu ya walimu kukosa morali wa kufundisha kuwa ndiyo sababu ya msingi, ya kuporomoka kwa ubora wa elimu nchini.
 
Kukosekana huku kwa morali kama utafiti wa WB ulivyobainisha, mbali na mambo mengine, unatokana na kukosekana kwa motisha kwa walimu.

Pamoja na udogo wa mishahara, walimu wamekuwa wanadai malimbikizo ya mishahara, posho na malipo mengine bila mafanikio.

Wakati serikali, kupitia wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi ikiwa katika utekelezaji wa mikakati ya BRN, ni muhimu ikatibu kwanza suala la morali kwa walimu.

Nia ni kuwawezesha wafundishe kwa muda unaotakiwa wa kufanyakazi kwa mujibu wa miongozo, ili kuboresha kiwango cha ubora wa elimu inayotolewa kwa watoto wa kitanzania, na hatimaye taifa liwe na wahitimu wenye stadi stahiki kwa ustawi wa nchi.

CHANZO: NIPASHE

IDADI YA MIKOA NA HALI YA ELIMU KWA MWAKA 2013

Orodha ya Mikoa

Ufaulu kwa ujumla unahesabiwa kwa wastani kwa miaka yote ambayo takwimu ziliwezakukusanyika. Daraja zinakadiriwa kwa wastani wa pointi za mkoa.Pointi za chini huonyesha ishara ya kufaulu.
Nafasi[Sortable]Jina[Sortable]Alama kwa Wastani[Sortable]Idadi ya Watahiniwa[Sortable]Idadi ya Shule[Sortable]
1KILIMANJARO29.30156,908304
2DAR ES SALAAM29.85185,293298
3MBEYA29.86143,035272
4UNGUJA30.0551,641118
5MWANZA30.13133,698272
6IRINGA30.18114,011228
7ARUSHA30.2397,053182
8PWANI30.3355,155132
9SHINYANGA30.6276,863276
10KAGERA30.6383,948221
11MARA30.8581,909169
12MANYARA30.9548,076122
13RUKWA30.9935,105108
14TABORA31.0247,967161
15MOROGORO31.0782,882200
16RUVUMA31.2154,825167
17KIGOMA31.2360,163130
18DODOMA31.4765,488201
19PEMBA31.5027,39271
20SINGIDA31.5642,983130
21TANGA31.6198,364235
22MTWARA32.0639,467128
23LINDI32.3523,20099

Saturday, May 4, 2013

KIPANYA NAE



KWA

KWA HISANI YA MWANANCHI

Serikali yachukua uamuzi mgumu, yafuta matokeo

 


Dodoma/Dar. Serikali imechukua uamuzi mgumu na kuamua kuwafariji wanafunzi waliofeli mitihani ya kuhitimu kidato cha nne mwaka 2012 baada ya kufuta matokeo hayo na kuamua yaandaliwe upya kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011.

Uamuzi huo wa Serikali umetokana na matokeo mabaya ya mitihani huo yaliyosababisha zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi kupata sifuri.

Kutokana na matokeo hayo, Serikali iliunda Tume inayoongozwa na Profesa Sifuni Mchome kuchunguza matokeo hayo ili kupata ufumbuzi wa kudumu.

Muda mfupi baada ya tamko la Serikali, baadhi ya wadau wa elimu wameeleza kufurahishwa na uamuzi huo, huku Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kikiikosoa hatua hiyo, kuwa imekiuka sheria na kupora madaraka ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).

Akitoa kauli ya Serikali bungeni kuhusu taarifa ya awali ya Tume ya Taifa ya Kuchunguza Matokeo ya Mtihani wa Taifa Kidato cha nne mwaka 2012 jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema wameagiza Necta kuweka viwango ili matokeo ya wanafunzi yalingane na juhudi zao.

Standardization ifanyike ili matokeo ya wanafunzi yalingane na juhudi wazizoziweka katika kusoma kwa mazingira, hali halisi ya Tanzania na uamuzi wa taifa kuongeza idadi ya shule na wanafunzi wakati uwekezaji katika ubora unaendelea,” alisema Lukuvi.

Lukuvi alisema Necta imeelekezwa kuwa licha ya sheria ya kuanzishwa kwake kuruhusu kufanya marekebisho ya mchakato wa mtihani, marekebisho yoyote ya kubadilisha utaratibu wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya mitihani yanatakiwa yahusishe wadau wote wanaohusika na mitalaa, ufundishaji na mtihani.

“Wakati Tume inaendelea kukamilisha kazi yake, uamuzi wa Necta kutumia utaratibu mpya wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya mitihani uliotumika 2012 usitishwe,” alisema Lukuvi na kuongeza:

“Badala yake Necta itumie utaratibu uliotumika mwaka 2011 kwa kidato cha nne na sita kwa mitihani yote, ikiwamo utaratibu wa Standardization na kutoa matokeo mapya kwa kuzingatia maelekezo haya.”

Pia, Serikalli imeagiza mchakato wa tuzo wa taifa (National Qualifications Framework) na Mfumo wa Kutahiniwa/ kuthamini maendeleo ya mwanafunzi masomo yake (National Assessment Framework) ukamilishwe haraka iwezekanavyo.

Katika mtihani wa mwaka 2012, wanafunzi 367,756 walifanya mtihani huo na waliofaulu ni 126,847.

Waliofaulu kwa kwa madaraja ya kwanza hadi la tatu ni 23,520 sawa na asilimia 6.4 na daraja la nne ni 103,327 sawa na asilimia 28.1, huku 240,909 ambao ni asilimia 65.5 wakipata daraja sifuri.


Kauli ya CWT

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch alisema Baraza la Mawaziri limepora kazi za Bodi ya Baraza la Mitihani kwani ndio yenye jukumu la kufuta matokeo kisheria.

Mbali na hilo Oluoch alisema bado wanafanya utafiti ili kuona kama Baraza la Mawaziri lina uwezo wa kufuta matokeo na kuamuru mitihani isahihishwe upya, badala ya Bodi ya Baraza la Mitihani.

Oluoch aliyesema tamko rasmi la CWT kuhusu uamuzi huo wa Serikali litatolewa wiki ijayo, alieleza kuwa kwa sasa wanachunguza kuona kama jambo hilo lina usahihi kwa kiasi gani.

“Mitihani iliyofutwa ilitolewa na Bodi ya Necta ambayo ndio itakuwa na jukumu la kusimamia usahihishaji mpya na kutangaza tena matokeo.

Kama hali yenyewe ndio hiyo ni wazi kuwa haina tena uwezo wa kusimamia jambo hilo, inatakiwa kung’oka na kuundwa bodi mpya,” alisema Oluoch na kuongeza;

“Nasema hivyo kwa sababu hawawezi kula matapishi yao kwa kuwa wao ndio wenye mamlaka ya kutoa tena matokeo hayo na walishasema kuwa yalikuwa mabaya, sasa uzuri wake utatoka wapi tena.”

Alisema kuwa kufutwa kwa matokeo hayo kunaonesha wazi kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeshindwa kazi ya kusimamia elimu nchini.

“Pia katika utangazaji wa matokeo anatakiwa waziri mpya wa kufanya hivyo kwa kuwa huyu wa sasa alieleza sababu za wanafunzi kufeli, sasa akiwa anatangaza matokeo mapya atatueleza nini,” alihoji.

Sababu za matokeo mabaya

Waziri Lukuvi alisema takwimu zinaonyesha kushuka kwa ufaulu huo unahusu shule zote na asilimia kwenye mabano, shule za wananchi (1.82); Shule za umma yaani kongwe (6.43); Binafsi (6.39) na Seminari (7.29).
Kuhusu matokeo ya kidato cha nne 2012, Lukuvi alisema tume imebaini licha ya wanafunzi kuwa kwenye mazingira yanayofanana na wenzao waliopita, ufanisi umekuwa ukishuka kwa sababu mbalimbali.

“Ufaulu wao umeshuka zaidi kwa sababu ya mabadiliko ya mchakato wa kuandaa na kutoa matokeo ya mtihani mwaka 2012, mfumo uliotumika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti na ule uliotumika miaka iliyotangulia,” alisema Lukuvi na kuongeza:

“Uchunguzi unaonyesha kuwa mwaka 2011, Necta lilikuwa linachakata alama za mwisho kwa kutumia mfumo ambao ulikuwa unabadilika kutegemea hali ya ufaulu kwa mwanafunzi ambao ni National Mean Difference (NMD).

Alisema uataribu huo ulitokana na tofauti ya wastani wa kitaifa wa alama za maendeleo, kutoka alama ya maendeleo endelevu (Continued Assessment-CA) za watahiniwa wote na wastani wa kitaifa wa ufaulu wa mtihani wa mwisho kwa somo husika.

Aliendelea kuwa kila mtahiniwa aliongezewa NMD iliyokokotolewa kwenye alama za mtihani wa mwisho, ili kupata alama itakayotumika kupada daraja la ufaulu.

“Lakini mwaka 2012 lilitumia mfumo mpya wa kuwa na viwango maalumu vya kutunuku (Fixed Grade Range). Tume imebaini kwamba licha ya mfumo huo ulioandaliwa kwa nia nzuri, utaratibu huo mpya hakufanyiwa utafiti wa maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika,” alisema.
Lukuvi alisema taarifa ya awali ya tume, inaonyesha kutokana na uchunguzi uliofanyika kwa muhtasari imebaini mambo mbalimbali.

Alisema matokeo ya  kidato cha nne kuanzia mwaka 2008 yamekuwa na mserereko wa kushuka tofauti na miaka iliyotangulia, kwa sababu ya changamoto zinazotokana na mafanikio yaliyopo sasa ya kuongezeka kwa idadi ya shule za msingi na sekondari, hususan mwaka 2011 na 2013 hivyo kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi.

“Mwaka 1961 hadi 2011 idadi ya wanafunzi kwa shule za msingi imeongezeka kutoka 486,470 hadi 4,875,764, sawa na ongezeko la wanafunzi 4,389,294 kwa takriban miaka 40,” alisema.
Alisema wanafunzi wameongezeka kutoka 4,875,764 mwaka 2001 hadi 8,247,472 mwaka 2012, sawa na ongezeko la wanafunzi 3,371,708 kwa kipindi cha miaka 11.

Sekondari wanafunzi wameongezeka kutoka 11,832 mwaka 1961 hadi 289,699 mwaka 2001 sawa na ongezeko la wanafunzi 274,867 kwa miaka 40.
Lukuvi alisema kati ya mwaka 2001 hadi 2012 wanafunzi wameongezeka kutoka 289,699 hadi 1,884,270 sawa na ongezeko la watu 1,594,571.

Tume hiyo imebaini changamoto nyingine ni mazingira yasiyo ya kuridhisha ya kufundishia na kujifunzia, ikiwamo upungufu wa miundombinu muhimu ya shule; madarasa, madawati, maktaba, nyumba za walimu, bweni na majengo mengine muhimu.

“Kuna tatizo la uhaba wa walimu, vitabu, zana za kufundishia na matatizo ya ukaguzi wa shule. Vilevile tumebaini Mfumo wa Elimu ya Msingi na Sekondari unakabiliwa na changamoto nyingine mbalimbali ambazo taifa linapitia kwa sasa,” alisema Lukuvi na kuongeza:

 “Yapo masuala ya sera, sheria, mfumo, muundo na changamoto za uhaba wa rasilimali fedha na watu. Tume inaendelea kufanyia kazi maeneo haya kwa kushirikiana na wataalamu na wadau wengine.”

HABARI KWA HISANI YA MWANANCHI

Thursday, April 18, 2013

Tatizo la elimu nchini siyo viboko





Taifa liko katika wakati mgumu juu mustakabali wa sekta ya elimu kutokana na changamoto mbalimbali zinazoikabili.  Kuna mengi yanazungumzwa, yamependekezwa na mengine bado yanaendelea kutolewa juu ya njia sahihi ya kukoa elimu ya watu wa taifa hili.

Kuna hoja zinatolewa kwamba sekta ya elimu imeachwa kuporomoka hadi kufikia hali mbaya ya sasa kutokana na kuminywa kwa bajeti ya sekta hiyo, matokeo yake ni janga la kufeli kwa wananfunzi wengi katika mitihani yao kama ilivyodhihirika kwa wanafunzi wa kidato cha nne waliomaliza elimu ya sekondari mwaka jana kwa zaidi ya asilimia 60 kupata daraja sifuri.

Ukiacha suala la kufeli, kuna hoja za kweli na zenye mashiko zinazojengwa kwamba wanafunzi wengi wanaomaliza viwango mbalimbali vya elimu, kuanzia msingi, sekondari hadi vyuo vya elimu ya juu, hawafanani na matarajio ya watu kwa kuwa na uwezo wa kielimu kwa waliopita kwenye ngazi hizo za elimu.

Wapo wanafunzi wanamaliza darasa la saba bila kujua kusoma wala kuandika, lakini wanafaulu mtihani wa kuendelea na elimu ya sekondari; wapo wanaomaliza sekondari, lakini hawawezi hata kuandika sentensi moja iliyonyooka.

Kuna mgogoro mkubwa sana wa mitalaa ya elimu, mgorogo huu umejadiliwa kwa mapana yake na wadau wa elimu, ulifikishwa bungeni, lakini serikali kwa kutumia mlango wa nyuma iliikimbiza hoja hiyo kutoka bungeni kabla ya kupata mjadala wa kina ili ufumbuzi upatikane kwa nia ya kuokoa elimu ya nchi hii.

Katika harakati hizi na kizunguzungu katika sekta ya elimu, Waziri Mkuu ameunda Tume kuchunguza chanzo cha anguko kubwa la elimu kutokana na taifa kushtushwa na matokeo mabaya ya kidato cha nne kuliko mengine yote ambayo yamepata kuikumba nchi hii tangu uhuru.

Wakati hali ya elimu ikiwa katika mkanganyiko mkubwa, juzi Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, aliibuka na kusema kuna mpango wa kurudisha viboko pamoja na kupiga marufuku wanafunzi kumiliki simu shuleni kama njia ya kuokoa sekta ya elimu nchini.

Alisema hayo jijini Dar es Salaam katika hafla ya utambulisho wa tovuti ya www.shuledirect.co.tz ambayo
imeanzishwa na aliyewahi kuwa Miss Tanzania 2004, Faraja Kotta, huku akisisitiza kuwa wanafunzi wasipopigwa viboko, mambo hayaendi, ndiyo maana mwanafunzi anaingia darasani saa tatu yaani muda anaoutaka yeye, lakini anaachwa tu bila kuadhibiwa, matokeo yake wakifeli wizara inalaumiwa.

Inawezekana Mulugo ana hoja, kwamba maisha ya binadamu bila utaratibu na makubaliano yanayojenga wajibu mambo hayaendi, kwa maana hiyo kuibua hoja ya kucharaza wanafunzi fimbo, kunaweza kutajwa kuwa ni sehemu mojawapo muhimu ya kujenga uwajibikaji kwa wanafunzi katika kutimiza wajibu wao. Hili linawezekana na linajadilika.

Naibu Waziri huyu hapana shaka anasukumwa na uzoefu wa alikotoka, kwamba zamani wanafunzi walikuwa wanacharazwa viboko ndiyo maana walikuwa na nidhamu, walikuwa wanasoma kwa bidii, walifaulu vizuri na kwa maana hiyo taifa halikuwa na aibu kama hii ya kufeli kwa wanafunzi kwa kiwango hicho.

Pamoja na hoja ya Naibu Waziri kuwa na msimamo huo, lakini anashindwa kutambua kuwa fimbo pekee hazikwezi kupandisha ubora wa elimu, fimbo haziwezi kuokoa elimu kama tabia ya nchi hii kuhusu uwekezaji finyu katika sekta ya elimu itaendelea kuwa kama ilivyo sasa.

Kabla ya serikali kufikiria habari ya fimbo tungefarijika kama ingetambua kuwa ina kazi nzito na ngumu kufanya katika kurejesha sekta ya elimu katika mstari wake.

Hali ya shule nyingi ni duni mno, hakuna walimu, hakuna vifaa vya mafunzo, walimu hawana motisha yoyote ya maana, ujira wao ni wa kijungu jiko mazingira ya kazi kama nyumba za kuishi hazipo, heshima kwa walimu kutoka kwa serikali yao na hata kwa jamii hakuna kabisa.

Kwa miaka mingi serikali imekuwa inaahirisha matatizo ya sekta ya elimu, malalamiko ya walimu yamepuuza kwa kitambo kirefu sasa, shule nyingi za umma zimegeuka kuwa mahame, siyo mahali panapompa mwanafunzi motisha ya kusoma na kujifunza kwa bidii.

Viongozi wengi ambao wamepewa jukumu la kusimamia sekta ya elimu wamegeuka kuwa waigizaji badala ya kuyakabili matatizo ya elimu kisayansi. Kwa kifupi hali ni mbaya katika sekta ya elimu.

Ni kwa kuangazi haya tunaamini kabla ya Murugo kuanza kuzungumzia habari ya kurejesha viboko shuleni, angeangazia kwanza matatizo ya kumsingi ya sekta hii.

Wenzetu waliopiga hatua ni marufuku hata kumfokea mwanfanzi achilia mbali kucharazwa bakora, lakini viwango vyao vya elimu viko juu. Shule nyingi za binafsi haziruhusu viboko hapa nchini, viwango vya ufaulu katika shule hizo uko juu mno kulinganisha na za umma ambako pamoja na bakora kuwa ruksa kwa utashi wa mwalimu, ziko chini kwa ubora.

Ni hali hii tunawaomba viongozi wa sekta ya elimu wajaribu kusumbua vichwa vyao zaidi kupata majibu ya maana kuhusu changamoto za elimu nchini.


CHANZO: NIPASHE

Saturday, April 13, 2013

VYETI VYA WAZIRI VINA MUSHKERI

 
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo anadaiwa kutumia ujanja katika wasifu na elimu yake ambapo katika maisha yake ya kielimu ametumia majina manne tofauti.
Philipo Augustine Mulugo ndiyo jina lake halisi ambalo alilisomea mpaka alipohitimu darasa la saba kwa mara ya kwanza 1988, lakini kutokana na kwamba hakufaulu kwenda sekondari alirudia darasa hilo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa takriban miezi mitatu sasa umebaini kuwa 1989, Mulugo alirudia darasa la saba katika Shule ya Msingi Rukwa ya mkoani Mbeya akitumia jina la Hamimu Hassan.
Imebainika kuwa kabla ya kuhitimu darasa la saba kwa mara ya pili, alibadili jina hilo (kutoka Hamimu Hassan) na kuwa Hamimu Augustino ambalo aliendelea nalo wakati akisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari kutwa ya Mbeya (Mbeya Day) mwaka 1990.
Hata hivyo, Mulugo mwenyewe akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam alipuuza tuhuma hizo kwa kusema kuwa ni njama za kisiasa zinazofanywa na maadui zake. Mulugo anasema madai hayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na amekuwa akiyajibu kwa kuwaonyesha vyeti vyake halali vya shule.
“Hayo madai ni ya muda mrefu, wewe sijui utakuwa mtu wa 20 kuuliza swali kama hilo. Mimi vyeti ninavyo na hata ukitaka ushahidi nitakuonyesha,” alisema Waziri Mulugo na kuongeza:
“Haya mambo kabla hata sijachaguliwa kuwa Mbunge, tulivyokuwa bado kwenye mchujo wa ndani, usiku wa manane watu walisambaza huu uvumi na nilivyoenda kwenye kikao nikatoa vyeti vyangu, wakaviona.”
Waliomfundisha
Baadhi ya walimu waliomfundisha Mulugo, watu waliofanya kazi naye pamoja na wakazi wa Kijiji cha Udinde alikozaliwa, maelezo yao yanathibitisha mabadiliko ya majina ya Mulugo kwa nyakati tofauti pia ngazi mbalimbali za kielimu.
Uchunguzi unabainisha kuwa baada ya kuhitimu kidato cha nne, alifaulu kwenda Shule ya Sekondari ya Wavulana, Songea ambako alisoma kati ya 1994 na 1996 akiendelea kutumia jina la Hamimu Mulugo.
Baada ya kuhitimu kidato cha sita, uchunguzi ulibaini kuwa Mulugo alirejea Mbeya na 1998 alilazimika kubadili tena jina pale alipotumia cheti cha mtu aitwaye Dickson Mulungu, kuombea kazi ya kufundisha katika Shule ya Sekondari ya Southern Highlands.
Habari zinasema Mulugo alichukua hatua hiyo ili kumshawishi mmiliki wa shule hiyo mfanyabiashara, Gulnoor Dossa (sasa ni marehemu), kumpa nafasi ya kufundisha shuleni hapo.
“Mulugo alilazimika kutumia cheti cha rafiki yake aliyekuwa akiitwa Dick Mulungu ambaye alipata daraja la pili katika Shule ya Sekondari ya Songea Boys, hivyo ikawa rahisi kwake kupata kazi ya ualimu katika shule hiyo,” alisema mmoja wa waliofanya kazi naye shuleni hapo (jina tunalihifadhi kwa sasa).
Aliongeza kuwa Mulugo alianza kama mwalimu wa kawaida, lakini baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Shule (headmaster) wakati hakuwa hata na cheti cha ualimu. Alichukua nafasi hiyo ya ukuu wa shule baada ya aliyekuwapo kufariki dunia.
“Unajua wale wahindi (wamiliki) walikuwa ni wafanyabiashara kwa hiyo hawakufuatilia kiwango cha elimu ndiyo maana walimpandisha tu madaraja bila kujali kuwango cha elimu,” alisema rafiki yake huyo na kuongeza:
“Nilimshauri aachane na cheo hicho kwani kama ungefanyika ukaguzi wa Serikali na kumkuta bila vyeti vya ualimu angechukuliwa hatua, hivyo alinisikiliza na akaachia nafasi hiyo na kujipa cheo cha umeneja wa shule.”
Suala la uwezo na elimu ya Mulugo liliibua mjadala siku chache zilizopita baada ya kutoa kauli nchini Afrika Kusini aliponukuliwa akisema Tanzania ni muungano wa nchi mbili ambazo ni Tanganyika na Zimbabwe badala ya Zanzibar.
Alikotokea
Uchunguzi wa gazeti hili ulianzia katika kijiji alichozaliwa cha Udinde, Kata ya Kapalala wilayani Chunya mkoani Mbeya na alisoma Shule ya Msingi ya Rukwa.
Mmoja wa walimu waliomfundisha aliyejitambulisha kwa jina la Nyoni anasema anakumbuka kwamba Naibu Waziri huyo 1989 na wakati huo alikuwa akijulikana kwa jina la Hamimu Hassan.
“Mimi nilihamia hapa 1989 nikitokea Shule ya Msingi Kapalala. Kulikuwa na mwalimu mmoja tu kwa hiyo nikawa wa pili. Namfahamu Mulugo wakati huo akiitwa Hamimu Hassan. Sijui kabla hapo alikuwa akitumia jina gani,” alisema Nyoni anayetarajia kustaafu kazi ya ualimu mwakani.
Mmoja wa ndugu wa karibu wa Waziri Mulugo anayeishi kijijini hapo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini alikiri kuwa awali waziri huyo alikuwa akiitwa Philipo Augustino Mulugo.
“Philipo amesomea hapo Rukwa, ambayo ni Shule ya Msingi na alikwenda Kijiji cha Mkulwe kabla ya kwenda Mbeya kuwa Mwalimu. Sijui kama alirudia shule,” alisema ndugu huyo.
Mkazi mwingine wa kijijini hapo, Peter Kayuti alikiri kumfahamu Waziri Mulugo tangu enzi za utoto na kwamba alirudia darasa la saba, lakini alisema hakumbuki jina la pili alilolitumia. “Ni kweli Philipo alirudia shule, lakini sijui kama alitumia jina jingine zaidi ya hilo la sasa,” alisema Kayuti.
Mwalimu aliyemfundisha katika Shule ya Sekondari Mbeya ambaye pia aliomba jina lake lihifadhiwe, alikiri kumfahamu kwa jina la Hamimu Augustino, lakini akasema hafahamu lilibadilika lini.
“Ni kweli, nilimfundisha Waziri Mulugo na alikuwa akiitwa Hamimu Agustino. Sidhani kama ni jambo geni kwa wanafunzi hasa wa zamani kurudia shule… Zamani ilikuwa kawaida kwa kuwa shule zilikuwa chache. Sijui alibadilisha jina hilo lini, lakini hilo ni suala la kisheria tu,” alisema mwalimu huyo.
Utata wa majina
Mwalimu mwingine aliyewahi kufanya kazi na Waziri Mulugo katika Shule ya Southern Highlands alisema waziri huyo alikuwa na tabia ya kuchanganya majina yake ya awali ili kuficha cheti alichoombea kazi.
“Yule alikuwa mjanja sana, ndiyo maana ukiangalia kadi zake zilikuwa na majina mengi tu na yana badilika. Leo atasaini barua kwa jina hili kesho lile. Mara utaona ameandika kifupisho cha PHDA, yaani Philip Hamimu Dick Agustino, mara Mulungu EDM, mara Mulugu D. Philip,” alisema mwalimu huyo na kuongeza:
“Amekuwa akijaribu kulibadilisha jina la Mulungu kuwa Mulugu mwisho amelipeleka kuwa lake la awali la Mulugo. Yote hayo ni kuficha tu ukweli kwamba alitumia cheti cha Dick Mulungu,” alisema mwalimu huyo.
Mmoja wa wakuregenzi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (jina tunalihifadhi) alisema: “Ili mwalimu wa sekondari awe headmaster (mkuu wa shule) ni lazima awe na shahada ya kwanza kutoka kwenye chuo kikuu kinachotambulika. Anatakiwa pia kuwa na uzoefu wa kazi wa miaka isiyopungua minane.”
Kuhusu kughushi vyeti mkurugenzi huyo alisema, ikigundulika kuwa mwalimu ameghushi cheti anafukuzwa kazi mara moja, lakini alikiri kwamba katika shule binafsi inawezekana walimu wasio na sifa wakapenya, lakini wakaguzi wakibaini hutoa maelekezo wafukuzwe.
“Kwanza siku hizi ili mwalimu aajiriwe ni lazima akabidhi vyeti vyake wizarani na hupelekwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) ili kuhakikiwa. Zamani ukaguzi haukuwa makini kwa hiyo inawezekana kuna watu wasio na sifa walipenya,” alisema.
Kuhusu kurudia darasa la saba, alisema sheria haijawahi kuruhusu watu kurudia darasa la saba na kwamba wale waliorudia hutumia mbinu zao kufanya hivyo.
“Sheria haijawahi kuruhusu watu kurudia darasa la saba. Ni kweli wengi wamerudia sijui wanatumia mbinu gani, lakini hairuhusiwi. Ukishafanya mtihani wa darasa la saba mara moja ndiyo basi,” alisema mkurugenzi huyo.
Msemaji wa wizara hiyo, Mtandi Bunyanzu kwa kila swali aliloulizwa alisema hana uhakika hivyo asingeweza kutoa jibu lakini kwa suala la kughushi vyeti, alisema ni kosa la jinai siyo kwa walimu tu bali kwa kila mtu atakayebainika.
“Kughushi vyeti ni kosa la jina siyo kwa walimu tu, hata waandishi wa habari,” aliongeza Bunyanzu.
Kwa upande wake, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) halikuwa tayari kutoa matokeo ya mitihani ya Mulugo na badala yake msemaji wa baraza hilo John Nchimbi alisema matokeo hayo ni siri ya mtahiniwa na hawezi kupewa mtu mwingine.  
Chanzo: Gazeti Mwananchi

Saturday, January 12, 2013

MATOKEO YA KIDATO CHA PILI HAYOOOOOOOOO

1.0UTANGULIZI


Mtihani wa Taifa wa Elimu ya Sekondari Kidato cha Pili ulifanyika nchini kote kuanzia tarehe 05/11/2012 na kumalizika tarehe 16/11/2012. Mwaka 2012 kulikuwa na jumla ya vituo 4,304 vilivyosajili watahiniwa, ikiwa ni ongezeko la vituo 117(2.79 %) ikilinganishwa na ile ya mwaka 2011.

2.0 WATAHINIWA WALIOSAJILIWA, WALIOFANYA NA WASIOFANYA MTIHANI
2.1Idadi ya watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani walikuwa 430,327, kati yao wasichana walikuwa 205,476 na wavulana 224,851. Idadi hii ni upungufu wa watahiniwa 36,240 (7.76%) ikilinganishwa na mwaka 2011 ambapo walikuwa 466,567.

2.2 Watahiniwa 386,271 sawa na asilimia 89.76 ya waliosajiliwa, walifanya mtihani wakiwemo wasichana 187,244 na wavulana 199,027.

2.3 Watahiniwa 44,056 sawa na asilimia 10.24 hawakufanya mtihani, kati yao wasichana ni 18,231 na wavulana 25,825. Mwaka 2011 watahiniwa 47,527(10.19%) hawakufanya mtihani. Sababu za watahiniwa kutofanya mtihani ni pamoja na utoro, kuugua, kudaiwa ada, kufukuzwa shule, mimba na vifo.

3.0 UFAULU WA WATAHINIWA

3.1Watahiniwa waliofaulu ni 249,325 (64.55 %) kati yao, wasichana ni 113,213 na wavulana 136,112. Kiwango cha ufaulu kimepanda kwa asilimia 19.15 kutoka asilimia 45.40 mwaka 2011. Watahiniwa waliofaulu kwa kiwango cha A, B, na C walikuwa 127,981 (33.13%) na waliofaulu kwa kiwango cha D ni 121,344 (31.42%). Alama ya juu ya ufaulu ni 92%

3.2 Wastani wa ufaulu kwa masomo ni 38%, wastani huu umepanda kwa asilimia 7 ukilinganishwa na mwaka 2011 ambapo ulikuwa 31%.

3.3Watahiniwa 136,923 (35.45 %) hawakufaulu mtihani, wakiwemo wasichana 74,020 na wavulana 62,903. Watahiniwa hawa watalazimika kukariri kidato cha pili mwaka 2013. Aidha, mwaka 2011 watahiniwa 228,759 (54.59%) hawakufaulu mtihani.

3.4 Watahiniwa 23 matokeo yao yamefutwa kutokana na tuhuma za udanganyifu. Watahiniwa hawa wanatoka katika shule zifuatazo;


Na Jina la Shule Kanda Idadi ya watahiniwa
1. Kiyongwire Mashariki 2
2. Nyashishi Ziwa 4
3. Thaqaafar Ziwa 3
4. Paroma Ziwa 2
5. Murangi Ziwa 1
6. Bukene Magharibi 7
7. Kili Magharibi 1
8. Binza Magharibi 1
9. Kizumbi Magharibi 1
10. Kolandoto Magharibi 1


Watahiniwa hawa nao watalazimika kukariri kidato cha pili mwaka 2013.

4.0 UFAULU KWA SHULE

4.1 Shule Zilizoshika Nafasi Kumi za Mwanzo

4.1.1 Shule za Serikali
NA. SHULE KANDA
1. MZUMBE MASHARIKI
2. TABORA WAVULANA MAGHARIBI
3. ILBORU KASKAZINI MAGHARIBI
4. KIBAHA MASHARIKI
5. IYUNGA NYANDA ZA JUU
6. MSALATO KATI
7. MALANGALI NYANDA ZA JUU KUSINI
8. IFUNDA UFUNDI NYANDA ZA JUU KUSINI
9. SAMORA MACHEL NYANDA ZA JUU
10. KILAKALA MASHARIKI


4.1.2 Shule Zisizo za Serikali
NA. SHULE KANDA
1. KAIZIREGE ZIWA MAGHARIBI
2. MARIAN WAVULANA MASHARIKI
3. ST. FRANCIS NYANDA ZA JUU
4. DONBOSCO NYANDA ZA JUU KUSINI
5. BETHEL SABS NYANDA ZA JUU KUSINI
6. MARIAN WASICHANA MASHARIKI
7. DON BOSCO (MOSHI) KASKAZINI MASHARIKI
8. CANOSSA DSM
9. ST. JOSEPH ITERAMBOGO SEM. ZIWA MAGHARIBI
10. CARMEL MASHARIKI
4.2 Shule zilizoshika nafasi kumi za Mwisho
4.2.1 Shule za Serikali

NA SHULE KANDA
1. MIHAMBWE KUSINI
2. DINDUMA KUSINI
3. KIROMBA KUSINI
4. MARAMBO KUSINI
5. MBEMBALEO KUSINI
6. KINJUMBI KUSINI
7. LITIPU KUSINI
8. LUAGALA KUSINI
9. MIGURUWE KUSINI
10. NAPACHO KUSINI
4.2.2 Shule Zisizo za Serikali

NA. SHULE KANDA
1. MFURU MASHARIKI
2. PWANI MASHARIKI
3. DORETA KATI
4. KIGURUNYEMBE MASHARIKI
5. RURUMA KATI
6. AT-TAAUN MASHARIKI
7. JABAL HIRA SEM MASHARIKI
8. MKONO WA MARA MASHARIKI
9. KILEPILE NYANDA KUSINI
10. KIUMA NYANDA KUSINI

5.0 UFAULU WA WANAFUNZI
Wanafunzi Walioshika Nafasi Kumi za Mwanzo
Na JINA JINSI SHULE
1. MAGRETH KAKOKO KE ST FRANCIS
2. QUEEN MASIKO KE ST FRANCIS
3. LUKUNDO MANASE ME KAIZIREGE
4. FRANK J NYANTARILA ME KAIZIREGE
5. GRACE MSOVELLA KE ST FRANCIS
6. HARIETH MAKIRIYE KE ST FRANCIS
7. ROBINNANCY MTITU KE ST FRANCIS
8. HUMRATH LUSHEKE KE ST FRANCIS
9. MUKHSIN HAMZA ME KAIZIREGE
10. ANASTAZIA KABELINDE KE KAIZIREGE

6.0 HITIMISHO
Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Elimu ya Sekondari Kidato cha Pili mwaka 2012, yanaonesha kuwa kiwango cha ufaulu kimepanda kutoka asilimia 45.40 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 64.55 mwaka 2012. Aidha, watahiniwa 249,325 wataendelea na masomo ya kidato cha tatu mwaka 2013. Napenda kuwapongeza wanafunzi wote waliofaulu kuendelea na masomo na kuwataka kuendelea na bidii katika kujifunza.

Kwa upande mwingine, watahiniwa 136,946 ambao wameshindwa kupata wastani wa ufaulu wa alama 30 na wale waliofutiwa matokeo yao kutokana na udanganyifu watalazimika kukariri kidato cha pili mwaka 2013. Ni vema ikaeleweka kuwa kukariri kidato si adhabu bali ni kutoa fursa nyingine kwa mwanafunzi kuweza kupata maarifa, stadi na ujuzi wa elimu ya sekondari kidato cha kwanza na cha pili kwa kiwango kizuri. Hivyo ni matumaini yangu kuwa wanafunzi hawa watafanya bidii katika kujifunza na kuzingatia masomo ili waweze kufaulu, pia walimu kuwasaidia Wanafunzi hao waweze kufanya vizuri.

Serikali kwa upande wake itaimarisha usimamizi wa elimu katika ngazi ya shule na kuziwezesha shule kukabiliana na changamoto mbalimbali kwa kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji ikiwa ni pamoja na walimu kubadili mikakati ya ufundishaji na ujifunzaji na wazazi kufuatilia maendeleo ya wanafunzi.

Vilevile, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi chini ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) itaendelea na jitihada zake za kuimarisha na kuboresha mazingira ya utoaji elimu bora kwa kujenga maabara za sayansi, kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu, kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuimarisha usimamizi wa shule. Aidha, wizara itaendelea kutoa walimu kwa awamu kila mwaka ili kukabiliana na upungufu uliopo.
Mhe. Philipo Mulugo (Mb)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
11/01/2013


Shule za Kiislam zimefeli Islamic Knowledge na Shule za kanisa zimefaulu mpaka masomo ya Kiarabu -- Ukistaajabu ya Musa utashangaa ya Firauni

CHANZO: JAMII FORUM