Friday, November 4, 2011

HISTORIA FUPI YA ELIMU TANZANIA HII HAPA

Na mdau Stephen Maina

kuanzia mwaka 1962 katika ngazi mbalimbali za elimu kuanzia elimu ya msingi, sekondari, vyuo vya ualimu, elimu ya watu wazima na vile vile katika Makao Makuu ya Wizara, hadi nilipostaafu mwaka 1996, nitajitahidi kuwapa mwanga wasomaji wangu kuhusu hali ilivyokuwa  tangu mipango ya elimu ilipoanza kubadilishwa kuanzia tarehe 1 Januari 1962  hadi sasa na kuona tumeteleza wapi na tujikwamue vipi.
Hapo mwanzoni mara baada ya kupata uhuru mwaka 1961, tulirithi mfumo wa elimu uliokuwa wa kibaguzi. Shule  zilikuwa katika makundi matatu.
Makundi hayo ni shule za Wazungu, shule za Waasia hasa Wahindi na shule za Waafrika. Kila kundi lilikuwa na utaratibu wake tofauti kama vile masharti ya ajira kwa walimu, mitalaa, mitihani, vitabu, lugha ya kufundushia, usimamizi na utawala.
Kwa shule za Waafrika, lugha ya kufundishia katika shule za msingi  ilikuwa Kiswahili kuanzia darasa la kwanza hadi la sita na lugha ya  Kiingereza ilikuwa ikitumiwa kama lugha ya kufundishia katika madarasa ya saba na nane na kuendelea hadi shule za sekondari. Waasia walikuwa wanatumia lugha zao za asili kama vile Gujarat, Urdu na Kipunjab na pia Kiingereza.
Katika kipindi cha mwaka 1962 na 1966 yalifanyika mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu nchini Tanganyika. Mwaka 1961 ulikuwa mwaka wa shughuli nyingi za kisiasa na hasa marekebisho ya Katiba.
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitatu (1961 – 1964) ulianzishwa na ulikuwa ni mpango wa kipindi cha mpito kutoka utawala wa kikoloni na kuelekea kipindi cha uhuru. Katika kipindi hiki mkazo ulitiliwa katika upanuzi wa elimu ya msingi na pia elimu ya sekondari.
Elimu ya msingi ilipanuliwa hasa katika madarasa ya nne hadi ya sita (District Schools) lengo likiwa ni kujenga shule nyingi za Middle School madarasa ya tano hadi ya nane. Lakini mwaka 1964 uamuzi ukapitishwa wa kupunguza mafunzo ya elimu ya msingi kutoka darasa la nane na kuishia darasa la saba. Mfumo huu unatumika  hadi leo.
Elimu ya ufundi ilisimama na kukawa na shule tatu za ufundi ambazo zilikuwa ni Dar es Salaam, Ifunda na Moshi. Kwa hivyo, elimu ya ufundi haikutiliwa mkazo sana katika mpango huu.
Uamuzi wa kutotilia mkazo elimu ya msingi unatuathiri hadi leo kwa kusababisha upungufu wa wafundi wa kutosha wa ngazi za kati  katika fani za umeme, uashi, useremala, ufundi magari na kadhalika.
Vile vile hali hii imeendelea kuwa vivyo hivyo hadi leo katika taaluma za kilimo, ufugaji, afya na biashara. Hawakuandaliwa wataalamu wa kutosha wa ngazi za kati ambao wangeweza kusukuma gurudumu la maendeleo vijjini ili kuinua uchumi na maisha ya wananchi kwa jumla.
Mwaka 1963 serikali iliamua kufuta ada katika shule zilizofadhiliwa na serikali kutokana na Waafrika kutomudu kugharimia ada kwa kuwaelimisha watoto wao. Wanafunzi ambao wazazi wao hawakuwa raia wa Tanganyika na Zanzibar walilipa ada na wengine walisoma katika shule binafsi.
Kwa mfano The International School of Tanganyika  ilijengwa kwa ajili ya watoto ambao wazazi wa kigeni waliokuwa watumishi wa serikali au wataalamu wengine. Shule hii ilifuata mitalaa ya Uingereza na Marekani.

Suala jingine lililoanzishwa lilikuwa ni kuanzishwa kwa Mamlaka za Elimu katika ngazi ya wilaya. Kwa mfano Chagga Council ilikuwa ni ya kwanza kuanzishwa na kuanza kusimamia elimu katika ngazi ya msingi badala ya Serikali Kuu. Baadaye nchi nzima ilikuwa na mamlaka za elimu kwa ajili ya shule za msingi.
Maofisa Elimu wa Mikoa na Wilaya walikuwa ni wasimamizi au washauri tu. Elimu ya sekondari. Mafunzo ya ualimu yalikuwa chini ya usimamizi wa Serikali Kuu.
Pamoja na kwamba halmashauri za wilaya zilipewa mamlaka ya kusimamia shule za msingi, walikuwapo pia mawakala wa elimu waliokuwa wanasimamia elimu.
Mawakala hawa walikuwa Wamisionari wa makanisa ya Katoliki na Waprotestanti hasa Waanglikana na Walutheri. Kutokana na hali hii, walimu waligawanyika katika makundi mbalimbali kulingana na wanaowasimamia.Walimu wa misheni hawakutendewa haki sawa na walimu wa serikali.
Walimu wa misheni hawakupewa misaada ya kodi ya pango, matibabu, pensheni na pia malipo ya likizo.Kwa upande wa walimu wa serikali hawakuruhusiwa kujiunga na vyama vya siasa. Pia walimu hawa walikuwa wanapata uhamisho wa mara kwa mara nchi nzima wakati walimu wa misheni walikuwa wakihamishwa kulingana na madhehebu husika.

Tofauti hizi zilisababisha walimu kuunda vyama vyao vya kutetea maslahi yao. Kwa mfano, walimu Waafrika walikuwa na chama chao kilichojulikana kama Umoja wa Walimu Waafrika Tanganyika (Tanganyika Union of African Teachers -TUAT) Walimu waliokuwa wanafundisha shule za Kikatoliki walikuwa na chama chao kilichojulikana kama Umoja wa walimu Wakatoliki (Tanzania Catholic Teachers Union – TACTU).
Vyama hivi viliungana na kuwa na chama kimoja kilichojulikana kama Umoja wa Walimu Tanganyika (Tanganyika National Union of Teachers – TNUT).
Hatimaye serikali ikaona umuhimu wa kuwa na chombo cha kushughulikia maslahi ya walimu wote bila kubagua walimu wa misheni na serikali.. Chombo hiki kiliitwa Umoja wa Huduma kwa walimu – Unified Teaching Service- UTS). Hivi sasa huduma za walimu zinashughukiwa na Chama cha Walimu Tanzania – CWT.

No comments: