CHAMA cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (Umati) kinafanya utafiti nchini ili kubaini tatizo la utoaji mimba kwa wanafunzi wa vyuo na sekondari. Mkurugenzi Mkuu WA Umati, Josephine Mwankusye alisema mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa kasi ya utoaji mimba katika shule za sekondari na vyuo ni kubwa na imesababisha wasichana wengi kupoteza maisha kutokana na suala hilo.
Chama hicho kimesema ingawa utoaji mimba unajulikana, lakini suala hilo bado ni changamoto kwani Serikali bado haijaridhia. Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusiana na suala la afya ya uzazi, Mwankusye alisema bado wanaendelea na utafiti nchi nzima ili kubaini ukubwa wa tatizo hilo. Alisema walitembelea shule za sekondari na vyuo na kubaini kuwa hata elimu ya afya ya uzazi bado vijana wengi hawana. “Tunatakiwa tuelimishe ili mimba zisipatikane ili vijana wetu wasome halafu mimba zitakuja baadaye,”alisema Mwankusye.
Mkurugenzi huyo alisema pia asilimia 98 ya wanawake walioko kwenye ndoa wana taarifa za uzazi wa mpango, lakini huduma za njia za uzazi wa mpango hazitoshelezi. Alisema asilimia 24 tu ya wanawake ndiyo wanaopata huduma hizo na kuzitumia na kutahadharisha kuwa kama jitihada za makusudi hazitachukuliwa kuna hatari ya kuwa na ongezeko kubwa la watu.
No comments:
Post a Comment