Monday, December 5, 2011

PROFESA BAVU ASEMA HATUNA CHA KUJIVUNIA KWEYE ELIMU




Profesa Bavu
Gedius Rwiza
WAKATI tunapoadhimisha miaka50 ya uhuru wa Tanganyika, Profesa Immanuel Bavu anaeleza kuwa elimu imeporomoka na inayotolewa sasa haina matumaini ya kuwaandaa viongozi wenye uadilifu kuiongoza nchi.
Anaeleza kuwa pamoja na kuadhimisha miaka 50 ya uhuru hatuna cha kujivunia katika suala la elimu pamoja na ujenzi wa madarasa mengi hali ambayo anaiita kuwa ni ‘danganya toto’ na kwamba elimu inayotolewa kwa sasa kila mtu anaona athari zake na kwamba baada ya miaka kumi ijayo hali itakuwa mbaya zaidi na wale walioona elimu kabla ya ukoloni wanaweza kutamani kurudi wakati wa enzi hizo.
“Nasikitika kuona viongozi wanasimama na kutangaza kwamba elimu imeboreshwa kwa kuwa wamejenga madarasa, wakati madarasa sio elimu bora, elimu bora ni pamoja na walimu bora, vitabu na vitendea kazi vyote lakini katika madarasa hayo tunaona wanafunzi wanakaa chini bila madawati hata walimu hakuna na wanafunzi wanaosoma katika mazingira hayo watafidiwa na nani?” Anahoji Profesa Bavu.
Profesa Bavu ni mhadhiri mstaafu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikuwa mhadhiri katika idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala.
Profesa Bavu amekuwa ofisa elimu wa kwanza baada ya Uhuru akiwa ofisa elimu wa Dar es Salaam na ameshiriki katika kubadilisha sera ya elimu ya mkoloni kutoka mfumo wa matabaka hadi elimu ya wote mwaka 1964.
Profesa Bavu anaeleza kuwa yeye amesoma katika shule za wakoloni kabla ya Uhuru na amefanya kazi wakati wa ukoloni. Alianza kazi Januari 1953, akiwa mwalimu.
Anaeleza kuwa elimu ya mkoloni ilifundisha maadili ingawa ilitolewa kwa matabaka lakini viongozi na watu walifuata sheria na kuzingatia maadili na kuwa wazalendo lakini kwa sasa hakuna kiongozi mzalendo.
Anasema zamani suala la rushwa halikuwa wazi kama lilivyoa wakati huu ambapo nchi inaadhimisha miaka 50 tokea ipate Uhuru.
Anaeleza kuwa viongozi waliosoma enzi za ukoloni ndio kidogo wanaonekana kuwa na unafuu katika utendaji na bado wana aibu, wanafuata maadili.
“Elimu ya mkoloni ilimuandaa mtu kimaadili na maarifa lakini elimu yetu imechakachuliwa kama unavyoona hata mhitimu wa chuo kikuu hana uwezo wa kujikwamua kimaisha badala yake anawaza wapi afanye ufisadi, ukitaka kuamini angalia waliosoma enzi za mkoloni na baada ya uhuru utapata jibu,” anaeleza Profesa Bavu.
Anasema zamani elimu ilikuwa nzuri zaidi kwa sababu kulikuwa na vifaa vya kufundishia na kujifunzia, kadhalika walimu wa enzi hizo walikuwa bora ingawa elimu yenyewe ilitolewa kwa matabaka kati ya Waafrika, Wahindi na Wazungu.
Profesa Bavu anasema kuwa shule maalumu zilikuwa ni shule ya msingi Bunge, Upanga na Mchikichini na kwamba shule za Wazungu ziliongoza kwa ubora zikifuatia za Wahindi huku Waafrika wakiwa wa mwisho, lakini shule zilikuwa na miundombinu ya kutosha.
Anaeleza chanzo cha elimu duni ni baada ya mwalimu Julius Nyerere kutangaza elimu kwa wote mapema mwaka 1970. Kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule alilazimishwa kwenda ambapo maandalizi ya miuondombinu yalikuwa duni.
“Kusema ukweli watu wote waliosoma kuanzia mwaka 1970 hadi 1985 angalia tabia zao na maadili yao unaweza kugundua tofauti ya waliosoma enzi za ukoloni na baada ya ukoloni tabia zao zinasikitisha maana wengi wao walipata elimu duni,” anaeleza Profesa Bavu.
Anasema kuwa baada ya walimu wa (UPE), elimu ilianza kushuka kwa kiwango kikubwa kutokana na waliokuwa wanatoa elimu kuwa na uwezo mdogo, wengi hawakuwa na taaluma ya ualimu, matokeo yake hata wale wanaowapa elimu hawawezi kufanikiwa katika harakati za kupambana na changamoto za maisha.
Anaeleza kuwa walimu wa enzi za ukoloni waliandaliwa kwa ubora unaotakiwa, walichaguliwa wanafunzi bora ndio waliokwenda kusoma vyuo vya ualimu na kazi ya ualimu wanafunzi walikuwa wanaichagua kabla ya kumaliza masoma, walisikika wakisema kuwa wakimaliza wanataka kuwa walimu.
“Enzi za ukoloni wanafunzi walichagua kazi ya ualimu bila kuambiwa na mtu au kushauriwa, yaani mwanafunzi hajamaliza masoma ulisikia nikimaliza nakwenda kuwa mwalimu, lakini sasa hivi hadi mwanafunzi afeli ndipo anataka kwenda ualimu kwa mtindo huu hatufiki popote,” anaeleza Profesa Bavu.
Aidha Profesa Bavu anasema kuwa zamani walimu waliheshimiwa kuanzia mtaani, Kanisani, Msikitini hata vijijini, na wao pia walijiheshimu na wale waliokiuka maadili waliwajibishwa kwa mujibu wa sheria za kikoloni ilipobidi hata kuchapwa viboko ili kusimamia maadili.
Anasema kuwa enzi za ukoloni hakuna mtu ambaye aliruhusiwa kujenga au kuanzisha shule bila maandalizi na aliyekiuka sheria alishitakiwa kwa mujibu wa sheria ya elimu ya ukoloni hali ambayo iliweza kuleta mafanikio makubwa katika sekta ya elimu tofauti na sasa ambapo kila mwanasiasa akijisikia anatangaza kujenga shule lakini siku zote kujenga shule lazima kuwepo maandalizi ya kutosha kuanzia walimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kadhalika.
Profesa Bavu anasema kadiri siku zinavyosonga mbele ndivyo elimu inavyozidi kuporomoka kutokana na mipango mibovu.
“Unajua kinacholeta tatizo viongozi wanaopewa madaraka ya kusimamia elimu wote wanasimamia sekta hii kwa msukumo wa kisiasa na wala sio kwa maslahi ya nchi na wananchi, maana elimu ilianza kuporomoka miaka saba tu baada ya kupate uhuru na mpaka sasa hakuna jitihada za kuboresha elimu badala yake kila kukicha hali inazidi iuwa mbaya,” anaeleza Profesa Bavu.
Kuhusu ukaguzi wa shule enzi za ukoloni, Profesa Bavu anasema kuwa Mkaguzi alikagua shule kuanzia usafi wa mazingira ya shule, usafi wa mwalimu anayefundisha darasani pamoja na usafi wa wanafunzi  na semina za walimu mara kwa mara zilikuwa zinafanyika.
Anaeleza kuwa wakati huu nchi inapoadhimisha miaka 50 ya uhuru kuna kila sababu viongozi wote kuangalia namna ya kuboresha elimu na kutoa elimu yenye kufundisha maadili kwa viongozi wa baadaye.
 “Elimu bora inawezekana iwapo viongozi watakuwa waadilifu na wa kweli kwa kusimamia rasilimali za nchi maana, suala la kushindwa kuimarisha elimu kwa kisingizio cha ukosefu wa bajeti, siyo kweli maana nchi inajitosheleza ila usimamiaji ndio una tatizo kwa hiyo wakati huu wa kuadhimisha miaka 50 lazima tuangalia mwenendo wa elimu nchini,” anasema Profesa Bavu.
Aidha anaishauri serikali kubadilika kimtizamo na  viongozi kumuogopa Mungu kwa kufuata maadili na kuwa wakweli katika kusimamia rasilimali za nchi na kuacha kupanga mipango ambayo haitekelezeki.

HABARI KWA HISANI YA MWANANCHI

No comments: