Kwa hisani ya gazeti la mwananchi
Na Julius Samwel Magodi 0754 304336 \n juliusmagodi@yahoo.com KAMA kuna jambo ambalo linashangaza, ni tamko la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu matokeo ya mitihani ya darasa la saba kwamba, wanafunzi 9,000 wamefutiwa matokeo kutokana na udanganyifu na hata wale ambao watapangiwa shule za sekondari, watalazimika kupimwa uwezo wao kabla ya kuanza masomo. Nasema ni jambo la kushangaza kwa sababu inaonyesha sasa elimu ya darasa la saba ni sawa ya chekechea ambako ufaulu wa juu ni kusoma na kuandika tu. Nilimsikiliza kwa makini na kumwangalia kwenye televisheni wakati akitangaza matokeo hayo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo pamoja na mambo mengine, akisema kutokana na tatizo hilo, wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwakani, watapaswa kuchujwa upya. Mulugo bila ya kupata kigugumizi alisema wanafunzi waliofutiwa mtihani huo ni 9,736 na utaratibu wa kuchuja wale waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza utaanza rasmi Januari mwakani. Alisema wizara imegundua kuwapo kwa aina nne za udanganyifu ikiwamo wanafunzi kukutwa na majibu katika karatasi, rula na viatu na kuwapo kwa wanafunzi 9,629 waliokuwa na mfanano usio wa kawaida katika kukosea majibu ya maswali. Katika taarifa hiyo ya Waziri aliutaja Mkoa wa Manyara kuwa ni kinara wa kuchakachua ukiwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliofutiwa matokeo, ukifuatiwa na mikoa ya Arusha na Lindi. Kwa hakika, tukio hili la wanafunzi wengi wa darasa la saba kuchakachua mitihani na serikali kuamua kuwapima upya kwa kuwapa mitihani ya kusoma na kuandika ni ishara kwamba sasa taifa lipo katika janga kubwa la elimu. Ni janga kwa sababu inavyoonyesha elimu ya msingi sasa haina mwenyewe wa kuiendesha, inakwenda kama gari lisilokuwa na dereva. Nasema hivyo kwa sababu kama elimu ya msingi ingekuwa na usimamizi makini, mwanafunzi hawezi kuanza darasa la kwanza akafanya mtihani wa darasa la nne akapita mpaka akafika darasa la saba akiwa hajui kusoma wala kuandika. Lakini kinachosikitisha zaidi ni kusikia kwamba watoto wa shule ya msingi ambao wanapomaliza darasa la saba mara nyingi huwa na umri wa miaka 12 hadi 14 nao wameingizwa katika vitendo vya uchakachuaji. Nasema wameingizwa katika vitendo hivyo kwa sababu katika mazingira ya kawaida, hakuna mtoto wa umri huo anayeweza kujua au kuwa na upeo wa kutafuta mbinu za uchakachuaji bila ya kusaidiwa na ama walimu au wasimamizi wa mitihani. Vitendo vya mitihani kuchakachuliwa tulizoe kuvisikia au kuviona vikitokea katika elimu ya sekondari, lakini kuanza kutokea katika shule za msingi ni ishara kwamba, kama ni saratani basi inazidi kuitafuta nchi.Kama mtoto ataanza kufaulu mtihani kwa kupewa majibu akiwa darasa la saba ni wazi atakuwa anajua njia rahisi ya kufaulu mitihani yake akiwa sekondari hadi chuo ni kupata kupata majibu mapema. Je, Mwanafunzi kama huyu akiimaliza chuo na kupata kazi, ataacha tabia yake hiyo ya kuchakachua? Akiamua kuingia katika siasa akabahatika kuukwaa uwaziri ataacha tabia yake hiyo? Ni wazi kwamba hawezi kuacha na ndio mwanzo wa kupata mawaziri wasiokuwa na uwezo wanaoshiriki katika michezo michafu ya kugushi nyaraka au kuingiza nchi katika mikataba mibovu. Kwa upande wa uamuzi wa serikali kuwafutia wanafunzi matokeo, kwanza tunapaswa kujiuliza mazingira ambayo mitihani hii inavyosafirishwa hadi kwenye vituo vya mitihani, inapatiwa ulinzi wa aina gani inaposafirishwa, inasafirishwa kwa usafiri gani? Je, ni kwa kutumia magari, pikipiki au ni basikeli? Swali lingine la kujiuliza mitihani hii ilihifadhiwa wapi? Tunajua kuwa shule zetu nyingi za msingi wanafunzi wanasomea chini ya miti kutokana na kukosa vyumba vya madarasa na ofisi za walimu. Je, walipata wapi eneo la kuhifadhia mitihani ili isiingie katika mikono ya walimu au wasimamizi wasiokuwa waaminifu? Wanafunzi 9,000 ni wengi kuwatia hatiani na kusha kuwaharibia maisha kwa makosa pengine si yao kirahisi namna hiyo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu. Suluhisho lingekuwa kurudia mtihani na kuziba mianya yote iliyosababisha uvujaji wa mtihani na wala si vinginevyo. Mfano mzuri ni ule mtihani wa kidato cha nne mwaka 1998 ambao tulishuhudia watoto wa viongozi wengi serikalini walikuwa na mitihani yote siku kadhaa kabla hata ya kuanza mitihani. Serikali ilichofanya wakati ule ni kufuta mtihani wote na kurudiwa upya Januari ya mwaka 1999. |
Sunday, December 18, 2011
SERIKALI IMETOA MAJIBU RAHISI MTIHANI WA DARASA LA VII
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment