Sunday, December 18, 2011

NILIKIMBIA NDOA YA LAZIMA NATAKA ELIMU - ZAINAB MFAUME

 
Katika simulizi ya maisha yake, Zainabu kutoka Kondoa ambaye hata hivyo anasisitiza kuwa maisha yake yako hatarini wakati wowote na anahisi kifo kinamsubiri.
Msichana huyo kutoka Kijiji cha Mbakose Wilayani Kondoa ambaye licha ya umri wake mdogo anasema amepitia misukosuko na taabu nyingi kiasi kwamba hana uhakika wa maisha wapi na lini  atakapopata kivuli cha kupumzikia.
Anasema: Bado naamini kuwa kama Serikali haitaweza kunisaidia basi ni bora kujiua kuliko kurudi nyumbani kwetu, Kondoa ambako nitakufa wakati wowote tena kifo kibaya.Msichana kutoka jamii ya wafugaji ambaye amemaliza darasa la saba kwa nguvu na juhudi zake binafsi akipata msaada kidogo kutoka kwa walimu wake baada ya mzazi wake (baba) kupokea mahari ya ng’ombe 15 wakati yeye akiwa darasa la tatu ili aolewa katika ndoa ya wake wengi.
Katika ushuhuda wake, Zainabu anasema kuwa mara alipofika darasa la tatu, baba yake anayemtaja kwa jina la Mfaume Masanja alipokea mahari kutoka kwa mzee mmoja kwa lengo la kumuoza binti huyo kwa makubaliano ya ng’ombe 15 na ng’ombe hao wakaletwa nyumbani kwao bila ridhaa yake.
Anasema yeye alikuwa na umri wa miaka 12 (mwaka 2006) na siku ya tukio alitoka shuleni mchana na kuelezwa na ndugu zake kuwa baba yake alishapokea mahari na hivyo alitakiwa kwenda kwa mumewe.
Aliieleza hadhara ile kuwa hakujua ni sababu ipi baba yake aliamua kumtendea jambo hilo ambalo aliamini tangu wakati huo kuwa ulikuwa ni ukatili wa kijinsia kwa kunyimwa haki yake ya kusoma.
Nilijipa moyo wa ujasiri kuwa siwezi kuolewa na nikatafuta namna ya kuhama pale nyumbani, lakini kwa sababu ya umri mdogo sikuweza kuwa na akili ya kwenda mbali zaidi ya kuishia kijijini pale.
Hata hivyo, nilimwambia mwalimu wangu ambaye kwa wakati huo alianza kuonyesha dalili za kutaka kunifuta shule, nikasema usinifute na ukinifuta mimi nitawaeleza polisi,  hivyo kauli ilimwogopesha mwalimu akaniruhusu kuendelea na masomo yangu, anasimulia.
Anaongeza kuwa kitendo cha kukataa kwenda kwa mume aliyechaguliwa na baba yake mzazi kilimsababishia mgogoro mkubwa na kuifanya familia yao kugawanyika hasa baba yake akimtenga mama yake na kuhamia kwa wake wengine kwani alikuwa na wake watatu.
Nini kilitokea
Msichana huyo anasema baba yake aliamua kurudisha ng’ombe wale kwa mwenye mali kitendo anachosema ni aibu kwa kabila lao,  hivyo ulifika wakati ambapo baba yake alichekwa na kudhihakiwa na jamii yao huku wakimwona kama mtu aliyeshindwa na mtoto wake wa kumzaa.
Hata hivyo hali, hiyo ilijirudia tena alipofika darasa la sita ambapo hali ilikuwa ni mbaya zaidi na maisha yake kuwa magumu nyumbani kwa baba yake ambako aliishi kama mtumwa.
Ni wakati huo ambapo baba yake mzazi alishachukua ng’ombe wapatao 18 kwa lengo la kumwozesha tena katika familia ambayo aliamini kuwa mwanawe asingeweza kukataa na safari hii akipata mtu wa umri mdogo ingawa hakuwahi kukaa naye pamoja wakajadiliana juu ya uchumba.
Anasema kwa mara nyingine aliamua kuzungumza na walimu wake ambao walitishia kumshitaki mahakamani  Mzee Mfaume na akafanya makubaliano ya kumsubiri msichana amalize kwanza darasa la saba huku wakiendelea kumbembeleza akubali kwa hiari yake.
Tangu wakati huo hakufanikiwa kuwa karibu na mumewe na wala hakuweza kuzungumza naye jambo lolote kwani hata jamii ilianza kuogopa msimamo wake, lakini ng’ombe waliendelea kuwa nyumbani kwa Mfaume huku yeye ( Zainabu) akibebeshwa mizigo na mrundikano wa kazi bila ya kumpa muda wa kujisomea kwa hofu kuwa angefaulu mtihani wa darasa la saba na kujiunga na kidato cha kwanza kama akiachwa kujisomea.
Siku asiyosahau maishani mwake
Ilikuwa Alhamisi ya Septemba 8, 2011 ambayo itabaki maishani mwake kama siku ya maumivu kwani alitoka shule akiwa na furaha ya kumaliza mtihani wake wa darasa la saba huku akiwa na matumaini ya kuendelea mbele zaidi kwa masomo na hasa ndoto ya kujiunga kidato cha kwanza.
Nilipofika nyumbani ghafla nikaona watu wengi ambao tayari walishajua kuwa tangu jana yake (Septemba 7) tulikuwa katika mitihani ya kumaliza darasa la saba na hivyo ilikuwa ni muda mwafaka wa mimi kuolewa. Kweli nilisema heri kufa ili mimi na baba tukose wote,’’anaeleza binti huyo huku akifuta machozi na kuendelea:
Nilitafuta kisingizio sikupata kwani watu wametoka mbali na wamekuja kwa ajili yangu, lakini nikasema kama ni hivyo itaolewa maiti yangu lakini si mimi! Nikatafuta namna ya kutoroka nyumbani pale jambo ambalo nilifanikiwa

mwananchi.

No comments: