Thursday, December 1, 2011

PINDA: OFISI YA ELIMU MOSHI VIJIJINI ICHUNGUZWE HARAKA

Mh. Mizengo Kayanza Peter Pinda
Habari na Rehema Matowo, Moshi
WAZIRI  Mkuu, Mizengo Pinda, ameagiza sekretarieti ya mkoa kuvamia ofisi ya elimu ya Moshi vijijini kufanya ukaguzi kubaini matatizo yaliyopo kutokana na kuwapo kwa madai mengi ya rushwa na unyanyasaji.

Pinda, alitoa agizo hilo juzi wakati akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama, sekretarieti ya mkoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi alipokuwa akipokea taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama.

Alisema licha ya taarifa ya mkoa kutolewa kwa usahihi, liko tatizo ofisi ya elimu ya wilaya hiyo na kumtaka Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Anna Muhalende, kusimama na kueleza sababu za ofisi hiyo kujaa matatizo kila mara.

Mahalande aliikiri kuwapo kwa udhaifu kwenye ofisi hiyo na kwamba, watendaji wake wamekuwa wakificha kwa makusudi nyaraka za walimu na majalada yao ingawa anakuwa tayari amesaini kwa muda mrefu.

Alisema ofisa elimu sekondari wilaya ni mgonjwa, aliyopo anakaimu na amekua akitoa maelekezo lakini hayatekelezwi.Kauli hiyo ilionyesha kumkera Pinda na kulazimika kutoa maagizo kwa sekretarieti ya mkoa kwenda kwenye ofisi hiyo na kufanya ukaguzi, kwani kuna malalamiko mengi ya walimu yamemfikia yakimtuhumu mkurugenzi na idara yake.

“Walimu wanatuma ujumbe kwangu juu ya unyanyasaji wanaopata kwenye hii ofisi, wanasema huwezi kuhudumiwa kama hutoi rushwa , ili faili lako lipite lazima utoe rushwa tena siyo kidogo,” alisema.

Alitaka sekretarieti ya mkoa kuhakikisha wanachunguza na kusafisha upya kwa kuwatoa watendaji wabovu na kuwawajibisha kwa mujibu wa sheria.



No comments: