Friday, December 9, 2011

Mh MUNGAI ASEMA ELIMU NI JAHAZI LINALOZAMA TARATIIIBU


Mh. Joseph Mungai

Unapo yataja majina ya wanasiasa wachache waliowahi kukaa madarakani kwa muda mrefu kama mawaziri walioitikisa nchi kwa mageuzi ya Kifikra, yamkini huwezi kusahau kulitaja jina la, Joseph Mungai, maarufu kama JJ.
Nyota yake ya kisiasa ilianzia kung’aa katika utawala wa serikali ya awamu ya kwanza ya, Baba wa Taifa,hayati Mwalimu Julius Nyerere, miaka ya 70 alipomteua kwa vipindi viwili tofauti kuwa Waziri wa Kilimo hadi mwaka 1982. Kutokana na ufanisi wake, Mungai alitakaswa na kuendelea kutumika katika serikali ya awamu ya pili ya, Alhaji Hassan Mwinyi, ‘Mzee Ruksa’ .
Hata hivyo, hakuishia hapo bali aliendelea na Serikali ya Awamu ya Tatu ya, Benjamini Mkapa na Awamu ya Nne ya Rais, Jakaya Kikwete.Huyu ndiye aliyekuwa Waziri wa Elimu kati ya mwaka 2000 na 2005 wakati ambako kwa mara ya kwanza karibu watoto wote wa rika lengwa la elimu ya msingi waliongezeka kutoka asilimia 55 mwaka 2005 hadi asilimia 98.7 mwaka 2005.
Huo ndio ulikuwa msingi wa mageuzi ya elimu uliotokana na maelezo kuwa Watanzania wengi walikuwa hawaielewi falsafa ya Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere, kuhusu ‘elimu ya kujitegemea’.Mwandishi wa makala hii, anafanya mahojiano na Mungai.
Swali: Wakati Tanganyika inapata uhuru Disemba 1961, ulikuwa mwanafunzi wa darasa la 11. Je, ulilichukuliaje suala hili la uhuru wa Tanganyika kwani ulikuwa bado kijana mdogo.wakati huo
JIBU: Ni kweli kabisa nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961, mimi nilikuwa mwanafunzi wa darasa la 11, lakini nilielewa sana maana ya uhuru kwa sababu niliyaonja baadhi ya maovu ya ukoloni hata kama nilikuwa mwanafunzi. Kwani wakati wa ukoloni elimu ilitolewa kwa ubaguzi katika shule tofauti kwa watoto; Waafrika,Wazungu na Waasia. Waafrika wachache nikiwemo mimi ,tulibahatika kusoma katika shule duni za Utawala wa wenyeji (Native Administration).
Swali:Unaposema kuwa shule hizo ziikuwa duni zilikuwa na kasoro zipi hasa.
JIbu: Ninacho kimaanisha hapa ni kwamba vigezo muhimu vya utoaji wa elimu bora kama vile wingi wa watoto darasani, ukubwa wa shule na usawa wa umri darasani vilikuwa vinapuuzwa bila kukemewa.
Swali: Ukiwa mmoja wa watu waliopata kuongoza Wizara ya Elimu kama Waziri ,yapo madai kwamba mawaziri wanaoteuliwa kuongoza Wizara ya Elimu, hufanya mabadiliko ya mitaala ya elimu bila kutafakari dhana halisi ya kufanya hivyo, hivi hatua hiyo ina tija yeyote kwa elimu yetu?
JIBU: Hatufanyi hivyo kwa sababuu za kisiasa ila ukweli ni kwamba mitaala hubadilishwa ili kuendana na wakati pamoja na kurekabisha kasoro zinazogunduliwa au zinazojitokeza.
Swali: Ulipokuwa waziri wa elimu kati ya mwaka 2000 hadi 2005, ulibadili mitaala hiyo na kuyapunguza baadhi ya masomo kwa wanafunzi; kulikuwa na sababu ya kufanya hivyo?
JIBU: Nilipokuwa Waziri waElimu wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu, tuligundua kasoro kubwa kwamba falsafa ya Baba wa Taifa,Hayati Mwalimu Julius Nyerere, iliyokuwa ikihusu elimu ya kujitegemea, ilikuwa ikitumika vibaya: Ilikuwa haijaeleweka kwa Watanzania wengi na wala haikuwahi kuingizwa katika mitaala ya elimu. Badala yake ilikuwa imepewa tafsiri finyu ya wanafunzi kwenda mashambani kulima kwa jembe la mkono. Ilikuwa ukiona katika ratiba ya darasani , neno E.K(Elimu Ya Kujitegemea) basi, ujue wakati huo mwanao alikuwa shambani akilima badala ya kuwa darasani.
Swali : Licha ya hatua hiyo Chini ya uongozi wako wakati ule, ilikuwaje wizara iliamua kuyaondoa baadhi ya masomo katika mitaala ya elimu wakati ulitaka falsafa ya Mwl.Nyerere iliyohusu elimu ya kujitegemea ieleweke vizuri?
iJIBU: Kutokana na uchambuzi wa kitaaluma uliofanywa na wataalamu iligundulika kwamba siyo sahihi kuwafundisha wanafunzi masomo ya ufundi,biashara na kilimo katika ngazi ya elimu ya msingi na ya sekondari kabla hawajaiva vizuri katika masomo ya kawaida, yaani Hisabati, Lugha (Kiswahili na Kiingereza) pamoja na Sayansi (Fizikia, Kemia na Baiolojia), Historia na Jiografia.
Uamuzi huo ulifanywa baada ya kushauriana vya kutosha na wadau wote ikiwemo Kamati ya Maendeleo ya Elimu (BEDC) na Taasisi ya Elimu Tanzania. Ilibidi tuanzishe zoezi la kuiingiza elimu ya kujitegemea katika mitaala ya elimu kwa kuyatumia masomo bebezi (carrier subjects) ambayo yaliteuliwa kwa uangalifu mkubwa wa kitaaluma. Mitaala ilirekebishwa ili baadhi ya mambo ya elimu ya kujitegemea yaingizwe katika masomo ya kawaida, mfano Hesabu za kibiashara ziliingizwa katika somo la Hisabati na mambo ya ukulima wa kisasa yaliingizwa katika masomo Baiologia, Kemia na Fizikia.
Swali: Unadhani kwa hatua hiyo mlifanikiwa kwa kiasi gani kupandisha kiwango cha elimu tofauti na ilivyo sasa?
JIBU; Naam; lakini pia niliamua mitihani ya darasa la nne na kidato cha pili irekebishwe ili iwe inapima kwa usahihi zaidi mapokeo ya elimu kwa wanafunzi wanaofeli ili wakariri darasa. Inafahamika kabisa kwamba juhudi za walimu wetu kufundisha na wanafunzi kujifunza viliongezeka sana. Watanzania wanakumbuka kwamba ufaulu kwa wahitimu wa darasa la saba na wale wa kidato cha nne ulipanda na watoto walikuwa wakifaulu tofauti na miaka ya nyuma.
Na wakati huo ndipo Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) ulipoanza kutoa matunda.Kutokana na hatua tulizochukua wakati huo, juhudi ya walimu kufundisha na wanafunzi kujifunza na wazazi kuhimiza ziliongezeka sana na viwango vya kufaulu darasa la saba na kidato cha nne vikapanda sana. Asilimia ya wanaofaulu mtihani wa darasa la saba ilipanda kutoka asilimia 19 mwaka 1999 hadi 62 mwaka 2005.
Swali: Kwa mtazamao wako, uliyoyafanya kwa kipindi hicho, hivi sasa kuna mabadailiko au mafanikio yeyote?
JIBU: Katika mwaka wa kwanza wa serikali ya awamu ya nne, karibu maboresho yote hayo yaliyofanyiwa kazi kwa miaka mitano iliyopita, yamefutwa kwa uamuzi wa kisiasa bila uchambuzi wowote wa kitaaluma na tukaanza safari ya kurudi tulikokuwa kabla ya mwaka 2000. Kwa msingi huo, matokeo ya mwaka jana yanaonyesha wazi tunaelekea huko.
Swali: Nini hasa kinachokufanya useme hivyo?
JIBU:Kiukweli naiona kasoro kubwa katika elimu yetu kwa sababu nafasi nyingi za usimamiaji wa elimu umeshikwa na maafisa kaimu wasio na meno; kwa mfano hajateuliwa Kamishna wa elimu tangu mwaka 2006. Katika msingi huo, dalili zinaonyesha kwamba meli ya elimu inazama pole pole…Kwa hiyo nashauri hali hii irekebishwe ili kuikoa elimu yetu isizidi kudidimia”.

No comments: