Friday, December 9, 2011

CWT YASISITIZA KAMA HAKUNA MALIPO MGOMO KAMA KAWA KWA WALIMU


Rais wa CWT Gratian Mukoba

PAMOJA na Serikali kutangaza kuwa imeanza kuwalipa walimu malimbikizo ya mishahara yao, Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kimesema walimu watagoma ikiwa hawatalipwa fedha zote wanazoidai serikali.Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema jana jijini Dar es Salaam kwamba wanachotaka ni walimu kulipwa fedha zote wanazodai ifikapo mwisho wa mwezi huu.

“ Hata kama serikali imeanza kulipa malimbikizo ya mishahara ihakikishe inalipa madai yote tunayoidai ifikapo mwishoni mwa Desemba vinginevyo Januari tutagoma,” alisema Mukoba.

Alisema ingawa serikali inasema imeshaanza kuwalipa walimu, chama hicho bado hakijathibitisha kama kweli walimu wameanza kulipwa.“ Tunachosema ni kuwa kama serikali imeanza kulipa tutashukuru lakini tunaishauri kulipa deni lote la Sh49.6  kabla ya kuanza  mwezi  Januari, ikifanya hivyo tutaendelea na kazi kama kawaida,” alisema Mukoba.

Walimu nchini wanaidai serikali jumla ya Sh49.6 yakiwa ni madai mbalimbali ya malimbikizo ya mishahara na nauli za likizo.Aidha, Mukoba alisema uhakiki wa madai ya walimu ulikwishafanyika kupitia Kamati ya pamoja kati ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na CWT.

“ Uhakiki ulikwishafanyika sasa tunashangaa ni uhakiki gani tena unafanywa na serikali,” alisema Mukoba.Juzi Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema walimu wameanza kulipwa malimbikizo ya mishahara lakini bado inaendelea kufanyia kazi stahili zao nyingine.

  “Tumeshaanza kuwalipa walimu malimbikizo ya mishahara lakini madai mengine bado yanafanyiwa uhakiki kwa kuwa ni lazima tujiridhishe kuwa ni madai halali,” alisema Mulugo juzi.Akawaomba walimu kuacha mipango ya kugoma na badala yake wawe na uvumilivu wakati madai yao yakishughulikiwa.

Sakata ya CWT kuitaka Serikali kuwalipa walimu madai yao ni la muda mrefu lakini Julai mwaka huu serikali ilikitaka chama hicho kuorodhesha madai yote ya walimu nchi nzima kwa ajili ya uhakiki.

No comments: