Saturday, November 12, 2011

WANACHUO 46 WAKAMATWA MLIMANI

WANAFUNZI 46 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wanashikiliwa na polisi baada ya kuandamana bila kibali kushinikiza Serikali kuwapa mikopo wenzao 1,000 waliokosa. Kabla ya kukamatwa,  Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kililazimika kutumia mabomu ya machozi na vipigo dhidi ya wanafunzi hao waliokuwa wakiandamana kuelekea Ubungo.

 Maandamano hayo yalianza saa 3:30 asubuhi kwa wanafunzi hao kupita madarasani kuwalazimisha wenzao kujiunga nao, huku waliopinga wakipigwa. Hatua hiyo, ilisababisha wengi wa wanafunzi hao kulikimbia huku na kule kuwakwepa waandamanaji hao waliokuwa na hasira, wakitumia fimbo ndefu kuwaadhibu walioktaa kujiunga nao. Baadaye safari ya kuelekea Ubungo ilianza lengo likiwa kufikisha ujumbe wao nje ya chuo hicho.
Baada ya kufika lango kuu la kuingilia chuoni hapo karibu na Ubungo, kulikuwa na magari ya FFU aina ya Landarover 110 na malori mawili yenye maji ya kuwasha.

 Waandamanaji hao hata baada ya kuyaona magari hayo hawakusita, waliendelea kusonga mbele. Walipofika langoni hapo mabomu ya machozi yalianza kurushwa na walianza kukimbia na wengine wakipigwa na kukamatwa. Katika muda usiozidi dakika 10, zoezi lilikuwa limemalizika, magari yalikuwa yamejaa wanafunzi waliokamatwa huku wengine wakikimbia.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Pamillius Wambura, alithibitisha kushikiliwa wanafunzi hao Kituo cha Oysterbay. Wambura alisema wanafunzi hao wanatuhumiwa kuandamana bila kibali.

Katika taarifa iliyotolewa na Naibu Makamu Mkuu UDSM (Utawala), Profesa Yunus Mgaya, alisema zaidi ya wanafunzi 1,000 hawajapata mikopo. Profesa Mgaya alisema suala la mikopo halikihusu chuo hicho, bali Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Aliwataka wanafunzi hao kufuata sheria ndogondogo zilizopo chuoni hapo na kuendelea kuwa watulivu wakati suala lao likiendelea kushughulikiwa na taasisi hizo. 

No comments: