Wazo mbadala: na mdau wa elimu Joster Mwangulumbi
NCHINI Liberia, nchi iliyokumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu, ilitoa kioja mwaka jana.
Baraza la Mitihani liliteua walimu wa kusahihisha mitihani ya wahitimu wa elimu ya sekondari, lakini kabla ya kuanza kusahihisha, walimu hao walipewa mitihani hiyo ya wanafunzi kupima uwezo wao.
Walimu waliumbuka. Taarifa zinasema kuwa zaidi ya nusu ya walimu walipata chini ya asilimia 50, na kwa matokeo hayo Baraza likateua walimu wengine.
Mazingira hayo ya Liberia yanaweza yawe sawa na ya hapa nchini, labda kwa vile Baraza la Mitihani la Taifa halijaamua kuwashtua walimu.
Hivi ni kweli walimu wote wana uwezo mkubwa na kazi hiyo? Hivi hakuna ambao uwezo wao sasa umeshuka kupita kiasi kutokana na ulevi, uzembe na kutojijali?
Mdudu huyo yumo nchini. Malalamiko ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Nimrod Mkono ni ushahidi tosha kuwa baadhi ya walimu wakipewa mtihani ule ule wa wanafunzi watafeli.
Wasiolijua Jimbo la Musoma Vijijini, Mkono kupitia kaulimbiu yake ya Mkono kwa Mkono, mwanasheria huyo maarufu nchini, kwa nguvu zake na kwa ushirikiano na wananchi amejenga shule za sekondari zaidi ya 30.
Hadi kufikia mwaka 2008, Musoma Vijijini ilikuwa na shule za sekondari zaidi 51 huku saba nyingine zilikuwa katika hatua mbalimbali.
Kati ya shule hizo, tatu alizojenga yeye mwenyewe kwa ushirikiano na marafiki zake ni za kisasa zaidi kuliko shule nyingi zinazojengwa leo.
Shule ya sekondari ya Chifu Wanzagi aliijenga na kuikabidhi kwa Kanisa Katoliki, halafu shule mbili Chifu Mang’ombe kwa ajili ya wavulana) na nyingine kwa ajili ya wasichana alizikabidhi serikalini.
Awali Chifu Wanzagi ilikusudiwa kuwa shule ya msingi na msingi uliwekwa na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, lakini aliendeleza na kuifanya shule ya sekondari.
Mkono hakujenga majengo ya madarasa tu bali pia maabara zenye vifaa vya sayansi, mabwalo yenye meza na viti na mabweni. Vile vile alijenga nyumba za walimu na akaweka samani.
Mwalimu anayeanza kazi anayepangwa katika moja ya shule hizo, anaweza asifikirie haraka kununua kitanda na vitu vingine kwa vile atavikuta humo kama ilivyokuwa shule za zamani.
Inashangaza kwamba viongozi wa ngazi ya juu wa elimu hawajazitembelea, na kwamba hata wakati Mkono anazikabidhi serikalini, hakuna waziri wa elimu aliyetembelea.
Kutembelea au kutotembelea shule hizo si nongwa lakini kilichonishtua hadi nikaandika makala hii ni kusikia malalamiko ya Mbunge huyo tena bungeni kwamba walimu wa sayansi waliopelekwa kwenye shule hizo hawana uwezo wa kutumia vifaa vya kisayansi vilivyopo. Je, ni aina ya walimu wa Liberia?
Haraka jibu linaweza kuwa hapana. Lakini Baraza liliwahi kuwashtua walimu wanaoteuliwa kwa kazi ya kusahihisha kufanya mitihani hiyo hiyo kwanza?
Baraza linaweza kusema si kazi yake, lakini halioni kwamba inawezekana viwango vya walimu hao sasa vimeshuka japokuwa nje wanaonekana maarufu?
Katika shule nyingi walimu hulalamikiwa kwa ulevi wa kupindukia, wizi wa mitihani, utoro na uzembe. Hayo si ndiyo baadhi ya mambo ambayo yanadhoofisha uwezo wa kufikiri na kusababisha kushindwa kutumia vifaa vilivyopo?
No comments:
Post a Comment