Friday, November 11, 2011

KIJANA AOMBA MSAADA KUSOMA

Na Joyce Mmasi
NDOTO yangu ya kuwa daktari imekoma, nimepambana katika masomo yangu ya sekondari tangu kidato cha kwanza mpaka cha sita, nimefaulu vizuri kwa mategemeo ya kuwa daktari, lakini nimegonga ukuta.
Watu wa Bodi ya Mikopo wameninyima mkopo, Hii ni kauli ya Msafiri Twaibu, yatima ambaye amefiwa na wazazi wake wote wawili.
Kila anapokwenda anatembea na hati za vifo vya wazazi wake ambapo mama yake alifariki mwaka 1996 na baba 2006, anatembea na hati hizo za vifo si tu kwa ajili ya kuthibitisha kuwa ni yatima na anastahili huruma, lakini pia ni kama amechanganyikiwa na hajui pa kupata msaada.
Alipowasili ofisi wa Mwananchi jijini Dar es Salaam alizungumza huku akitokwa na machozi, kilio chake kikubwa ni kuomba asaidiwe mkopo ili aweze kuendelea na masomo ya udaktari katika Chuo Kiikuu Cha Dodoma (UDOM) ambapo amechaguliwa baada ya kufaulu kwa daraja la pili mtihani wake ya kidato cha sita.
Twalib ametokea wapi?
Alizaliwa miaka 21 iliyopita katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam akaishi na mama yake na ndugu za mama kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri kati ya wazazi wake.
Anasema mama yake alifariki akiwa bado hajaanza shule ya msingi na kwamba alianza kusoma shule ya msingi huko Temeke akiwa anaishi na bibi yake .
Anasema alisoma kwa bidii na alipomaliza darasa la saba alifaulu na kuchaguliwa kujiunga na  Shule ya Sekondari ya Kata ya Temeke ambapo anasema akiwa huko alisoma kwa malengo ya kufaulu ili aendelee na masomo ya kidato cha tano na sita.
Nilikuwa na ndoto ya kuwa daktari...hivyo nilizingatia masomo ya sayansi na katika shule nzima ni mimi peke yangu niliyefaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza, anasema.
Anaongeza kuwa alipotokea shule  hiyo ya kata alichaguliwa kwenda Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tambaza kwa masomo ya kidato cha tano na sita ambapo anasema akiwa huko lengo lake lilikuwa moja kusoma kwa bidii na kufaulu vizuri ili achaguliwe katika chuo cha utabibu.
“Namshukuru Mungu, nilifanikiwa kupata daraja la pili kwa mchepuo wa PCB niliokuwa nikichukua na kubahatika kuchaguliwa kwenda UDOM ili kutimiza ndoto yangu ya udaktari anasema
Nini tatizo lake sasa
“Tatizo langu sasa limerudi palepale. chuo nimepata, lakini mkopo nimekosa......nimekuta mimi ni miongoni mwa wanafunzi ambao hatutapewa mikopo, nimefuatilia  hadi Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa zaidi ya miezi miwili nikiomba nionane na mkurugenzi nimweleze tatizo langu, nimuonyeshe hati hizi za vifo vya wazazi wangu wote ili aagalie uwezekano wa kunisaidia ili nipate mkopo, yote bila mafanikio,” anasema.
Changamoto alizokutana nazo katika masomo
Tangu kuanza kwake, shule za kata zimekuwa na tatizo la uhaba wa walimu, lakini Msafiri anasema aliiichukulia hali hiyo kama changamoto na kuwasumbua walimu kumsaidia pale alipokwama.
“Kama unavyojua uhaba wa walimu ni jambo la kawaida katika shule za kata, mimi hiyo haikunisumbu, kwani kwa kuwa malengo yangu yalikuwa kuwa daktari nilitumia kila nafasi niliyopata kusoma na kutafuta msaada wa kimasomo,” anasema.
Msimamo wa Serikali katika utoaji wa mikopo 
Serikali imetangaza mara kwa mara kwamba wanafunzi wa Sayansi ya tiba waliopata udahili kwa ufaulu wa daraja la kwanza na la pili watasomeshwa bure.
Mbali ya wanafunzi wa madaraja hayo, hata wale  wenye ufaulu wa daraja la tatu kutokana na kushindwa kwa somo la stadi za maendeleo, watasomeshwa bure kwa kupewa ruzuku badala ya mikopo.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa anasema kuwa: “Ruzuku zitatolewa kwa wanafunzi wa sayansi za tiba waliopata udahili kwa ufaulu wa daraja la kwanza na la pili kulingana na ukomo wa bajeti.
Anasema kwa msimamo na kauli hiyo ya Dk Kawambwa  ambaye piua  anafafanua kuwa wanafunzi hao hawatawajibika kuzirejesha kwa kuwa siyo mkopo, haoni kwanini yeye anyimwe mkopo.
Kama Waziri Kawambwa anasema utaratibu huo wa utoaji ruzuku kwa wanafunzi wa sayansi za tiba utaanza katika mwaka wa masomo wa 2011/2012, kwanini nimekosa, anaeleza huku akilia.
Mbali na hatua hiyo, Waziri Kawambwa amewahi kusema, “Kuanzia mwaka wa masomo 2011/12, fedha zote za mikopo zitapelekwa vyuoni ili viwalipe wanafunzi baada ya kuwahakiki. Maelekezo na utaratibu utakaotumika utaandaliwa na HESLB kwa kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu na wadau wengine.”
Anasema chini ya utaratibu mpya, waombaji wa mikopo wanaosoma ualimu wa sayansi, hisabati na sayansi za tiba watapatiwa mikopo kwa asilimia 100 na kwamba wale ambao si wa taaluma hiyo watapewa asilimia 50 ya mkopo.
Tamko hilo la Serikali ni matokeo ya tume iliyoundwa kuchunguza na kutoa mapendekezo ya kuboresha utoaji wa mikopo ya elimu ya juu iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete, Februari 14, mwaka huu.
Bodi ya mikopo inasemaje kuhusiana na suala la Msafiri?
Alipotafutwa mara kadhaa kwa simu yake namba 0754 300169, msemaji wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, mara zote hakupokea simu yake hiyo.
 .
Hata hivyo, Msafiri anamwomba Waziri Kawambwa, wafadhili na wahisani na watu wengine wenye mapenzi mema wajitokeza kumsaidia ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari na kuisaidia jamii kwani kuwa yatima siyo mwisho wa safari

No comments: