Thursday, November 17, 2011

WABUNGE MTWARA NA LINDI KUCHANGIA ELIMU


Jenerali mstaafu Makame Rashid
TAASISI ya South Eastern Development Organization (SEDO) kwa kushirikiana na wabunge wanaotoka mikoa ya Mtwara na Lindi, wameandaa hafla maalumu ya kuchangisha fedha kwa ajili ya maendeleo ya elimu. Akizungumza na waandishi wa habari jana Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Jenerali mstaafu Makame Rashid, alisema hafla hiyo inatarajiwa kufanyika Ijumaa wiki hii. Rashidf alisema hafla hiyo itafanyika katika ukumbi wa Karimjee mjini Dar es Salaam, na kwamba mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo.
Alisema lengo la kuchangisha fedha hizo ni kusaidia mpango maalumu wa elimu wa kugharamia walimu wanafunzi kutoka vyuo Vikuu kwa nia ya kufundisha shule za sekondari zenye uhaba wa walimu wanapokuwa likizo.
Alisema mpango huo unalenga shule za kata zilizo katika mikoa hiyo zenye uhaba mkubwa wa walimu, ambapo takwimu zinaonyesha shule nyingi zina walimu wawili ambao hufundisha kidato cha kwanza hadi cha nne.
Mwenyekiti huyo alisema mpango huo ni endelevu na unatarajiwa kuchukua muda wa miaka mitano, na kwamba utagharimu sh. milioni 150.
"Mpango huu unadhamiria kuziba pengo la upungufu wa walimu na kuongeza ufaulu wa watoto wa mikoa yetu," alisema Rashid.
Aliongeza mpango huo pia unalenga kukabiliana na changamoto ya kupungua kwa mwamko wa wanafunzi kuhudhuria masomo, utoro wa wanafunzi pamoja na ongezeko la mimba kwa wasichana.
"Hali duni ya wananchi kugharamia elimu, kushuka ari ya kufanya kazi miongoni mwa waalimu pamoja na upungufu wa majengo ya shule ni sababu kubwa inayochangia kushuka kwa elimu katika mikoa hiyo," alisema Rashid.
Aliwataka wananchi, hususan wanaotoka katika mikoa hiyo kujitokeza kwa wingi katika hafla hiyo ili waweze  kuchangia ili kufanikisha lengo lao.
SEDO shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa Agosti 23, 2003 na umoja wa wananchi wa mikoa hiyo kwa lengo la kushughulikia masuala ya kijamii.

No comments: