Thursday, November 17, 2011

KUFUNDISHA SHULE ZA WASICHANA YAHITAJI MOYO




Na Fredy Azzah
UALIMU ni miongoni mwa taaluma zenye changamoto lukuki hasa nchini Tanzania ambako uzoefu unaonyesha mwalimu hana thamani katika jamii.Ni kwa sababu hii na nyinginezo, ualimu unakimbiwa na walio wengi. Wanaousomea aidha hawana chaguzi za kusoma fani nyingine au wanatumia ualimu kama daraja la kuwafikisha katika malengo yao.

Kwa wanaoamua kuwa walimu kwa sababu ya utashi wao, nao wanakiri kuwa unahitajika moyo na wito kudumu katika kazi hiyo.

Kwa mfano, mwalimu wa elimu maalumu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani, Ayoub Msuya, anasema walimu wa kiume hasa vijana aghlabu wamekuwa wakijikuta katika wakati mgumu wanapopangiwa kufundisha katika shule za wasichana pekee.

“Sisi walimu wa kiume ambao umri wetu ni mdogo na tunafundisha shule za wasichana, tunatazamwa kwa jicho la ajabu na jamii,” anaanza kutaja sababu ya kuwa katika wakati mgumu na kuongeza: 

 “Mwanafunzi akifanya kosa ukampa adhabu, anaweza kusema unamuonea kwa sababu umemtongoza akakukataa na jamii ikakubali.  Mimi hali kama hiyo haijawahi kunitokea,  lakini kuna wenzangu yamewahi kuwakuta haya.’’

Kwa uzoefu wake,  Msuya anasema wanafunzi wengi wa kike wamekuwa wakipenda kuwaomba walimu wa kiume ushauri kuhusu elimu na hata maisha kuliko wanavyofanya kwa walimu wa kike.

Kwa sababu hii anashauri  kila shule kuwa na kitengo maalumu cha ushauri anachosema kitasaidia kutambua na kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wanafunzi.

“Sisi hapa  tuna hiki kitengo, kinasaidia sana kutambua matatizo ya wanafunzi. Kwa mwalimu,  usikimbilie tu  kuwapa wanafunzi adhabu pale wanapofanya kosa la utoro ama jingine. Baadhi ya matatizo ya wanafunzi yanahitaji ukae nao ili uyatatue kwa manufaa yao, ” anasema.

“Ukikaa naye atakueleza kwa kina kwa nini haji shule, hivyo unaweza kumsaidia kuliko kukimbilia tu kumchapa. Pia kuna mambo mengi tu utakayoyajua ukikaa na mwanafunzi na kuzungumza naye kirafiki, ”anaongeza kusema.

No comments: