KATIKA dunia ya leo, elimu inatajwa kuwa ndiyo nyenzo kubwa na muhimu katika kuyakabili maisha yaliyojaa kila aina ya changamoto.
Elimu inatuwezesha kujitambua, kujimiliki kuyakabili na kuyatawala mazingira yanayokamilisha ubinadamu wetu.
Hata hivyo kwa muda mrefu, baadhi ya makundi ya kijamii, wakiwemo wanawake yalikoseshwa na yanaendelea kukoseshwa haki yao ya kupata elimu.
Kwa sababu hii, idadi kubwa ya wanawake wameshindwa kujitambua, kujiamini na pia kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Pamoja na mambo mengine, elimu inabaki kuwa muhimu katika kuwawezesha wanawake kushiriki ipasavyo katika maendeleo ya jamii.
Tanzania kama zilivyo nchi nyingine zinatambua hali hii na ndiyo maana mikakati na mipango kadhaa imekuwa ikibuniwa ili kuwasaidia wasichana kupata elimu. Kwa mfano, katika miaka michache iliyopita idadi ya wasichana wanaoandikishwa katika madaraja ya elimu ya msingi na sekondari imeongezeka.
Bila shaka haya si mafanikio madogo.Lakini je wanafunzi hawa wanapata fursa ya kumaliza masomo? Kimsingi wasichana bado wanakabiliwa na vikwazo lukuki vinavyowazuia baadhi yao kushindwa kukamilisha ndoto zao.
Mimba za utotoni kwa mfano zinatajwa kuwa miongoni mwa vikwazo vikubwa vinavyowarudisha nyuma watoto wa kike kielimu. Edina Kashaija(20) mkazi wa kijiji cha Nyakazinga, wilayani Karagwe mkoa wa Kagera, ni mwathirika wa matukio ya mimba ambayo kila siku yamekuwa yakiongezeka shuleni.
Edna anasema alikutana na mtu aliyempa mimba muda mfupi baada ya kuhitimu darasa la saba, wakakubaliana kuoana , lakini alipojifungua mwanaume huyo alimfukuza.Bila shaka kisa chake kinasadifu ukweli wa mambo katika maeneo mengi ya nchi hii.
Sababu za kukosa elimu
Asasi ya HakiElimu iliwahi kufanya utafiti kuhusu elimu kwa wasichana na kubaini sababu mbalimbali zinazochangia wao kukosa elimu, ikiwemo hali duni za familia wanamotoka wasichana
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti huo uitwao “Mbinu za kufanikisha elimu kwa wasichana” uliofanyika mwaka 2010, karibu asilimia 31 ya wadau wa elimu wakiwemo walimu na wanafunzi waliohojiwa, walisema familia nyingi nchini ni maskini hivyo zinashindwa kuwatimizia wasichana mahitaji yao.
“Wazazi wanaamua kuwatumia katika shughuli za uzalishaji na biashara ndogo ndogo au kuwaoza wakiwa na umri mdogo.Kutokana na hali ngumu kiuchumi nyumbani, wasichana wenyewe hushawishika kufanya ngono ili wapate angalau sabuni ya kufulia,’’ inasema sehemu ya ripoti.
Sababu hii inatolewa ushuhuda na Swaumu Abdala (20) mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, aliyelazimika kuacha masomo akiwa darasa la tatu mwaka 1983 ili afanye biashara ya wazazi wake.
Anasema: “Niliacha shule nikiwa darasa la tano kwa sababu wazazi wangu walikuwa wanashindwa kukidhi mahitaji muhimu ya shule, ikiwemo kunilipia ada,kuninunulia madaftari na sare za shule.Nikawa nikitoka shule badala ya kujisomea, naambiwa nikauze sambusa barabarani”
“Kadri siku zilivyozidi kwenda, nikawa natoka kwenye biashara usiku sana. Kwa sababu ya kutolala vizuri,nikaamua kutokwenda shule na baadaye nikaacha rasmi mwaka 1998.Nikashindwa kuhitimu darasa la saba lakini kiukweli, nilikuwa napenda sana nifike hadi ngazi ya juu, ”anaongeza.
Sababu nyingine ni kuwepo kwa mila kinzani dhidi ya haki ya elimu kwa watoto wa kike.Huu ndiyo mtazamo wa James Mcharo, Mdau wa elimu na mhitimu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) anayeifafanua sababu hii kwa kusema:
‘Kuwepo kwa mila za jando, unyago na ngoma za asili zinazofanywa kwa ajili ya kumuandaa mtoto wa kike kufanya matendo ya ngono, kuolewa au kuwa mama wa familia mtarajiwa, inawafanya mabinti wengi kushindwa kutilia mkazo masomo yao na kuanza ngono wakiwa na umri mdogo, kitu kinachowasababishia kusitisha masomo yao.”
Tamaa anaitaja kuwa sababu nyingine akieleza kuwa wasichana wengi wana tamaa ya kutaka vitu vizuri bila kuwa na uwezo wa kuvipata, hivyo hujiingiza katika vitendo viovu kama ujenzi wa urafiki na wanaume.
Anataja sababu nyingine kuwa ni kutokuwepo kwa ukaribu kati ya mzazi wa kiume na mtoto wa kike hali inayotokana na wazazi wengi kushughulishwa na utafutaji wa maisha.Wasichana wanakosa fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu changamoto za kimaisha na jinsi ya kupambana nazo.
“Hii ni tafsiri tosha kwa binti kujua amekosa upendo wa baba, hivyo atajiamulia kufanya baadhi ya mambo yaliyo kinyume na maadili kutokana na kukosa malezi ya baba,’’ anabainisha Mcharo.
Mmomonyoko wa maadili uliochangia ongezeko la wanaume wakware katika jamii nao unasababisha watoto wa kike kukosa elimu.Wanaume hawa maarufu kwa jina la mafataki, huwarubuni wasichana na kuwatumia kama vyombo vya starehe.
Lakini pia mazingira ya shule nyingi nchini hayawapi uhuru wanafunzi wa kike ambao kwa sababu za kimaumbile wanalazimika kuwa watoro au kuacha kabisa shule.Akilifafanua hili, Mcharo anasema:
“ Shule nyingi za vijijini hazina mazingira rafiki kwa watoto wa kike, hakuna huduma za choo, maji, vyumba vya siri kiasi kwamba mwanafunzi anapokuwa katika hedhi, inamuwia vigumu kupenda shule.”
Kama mzazi , Specioza Maugo mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, anawashukia wazazi hasa wa kike kwa kukosa elimu ya malezi na kushindwa kutekeleza majukumu ya ulezi ipasavyo.
“Mzazi wa kike ana mchango mkubwa wa maendeleo ya mtoto katika nyanja zote ikiwemo elimu. Mama mwenye elimu ana uwezo mkubwa wa kumkazania mtoto wake kusoma kwa bidii ili afanikiwe katika elimu na maisha yake,”anaeleza na kusisitiza:
”Ukiwa kama mzazi, tambua una jukumu na wajibu katika malezi ya mtoto wako kwa kumuandaa na kumjengea utayari wa kupokea maarifa , kujifunza na kuyafanyia kazi yale anayojifunza kwa manufaa yake.”
No comments:
Post a Comment