Tuesday, November 1, 2011

MAONI YANGU JUU YA MWALIMU MIAKA 12 YA KUMKUMBUKA


Ni vigumu kumsahau Nyerere kirahisi, mtu ambaye sina shaka kwamba aliwaacha Watanzania wengi wakilia.

Kwa ubashiri wake kwamba atawaombea Watanzania kwa Mungu na hasa wale ambao wanaamini na kusaidiki katika maisha baada ya kifo katika ulimwengu ujao, wanaamini kuwa Nyerere anawaombea Watanzania mbele ya Mungu.

Ndiyo maana hata ule mchakato ulioanzishwa mwaka 2006 na Kanisa Katoliki, Jimbo Katoliki la Musoma, ambalo sasa limegawanywa na kuwa na pia na Jimbo la Bunda, ambako sina shaka kwamba eneo la Butiama ndiko liliko kiutawala, watakuwa wakiuendeleza mchakato huo, wakiamini kuwa ipo siku kiongozi huyu atatangazwa kuwa mwenyeheri.

Lakini, ujasiri wake wa tangu kuzaliwa kwake ambao tunaambiwa kwamba ndio uliomwezesha kusoma na kuwa Mtanganyika wa kwanza kuhitimu Shahada ya Uzamili (MA) kule Edinburgh, Scotland miaka michache kabla ya uhuru, naamini bado upo.

Pia, Nyerere ambaye simulizi za kihistoria zinaeleza kuwa aliwahi kuwa mwanafunzi bora kitaifa katika mtihani wa darasa la nne zama zake, hakuna shaka aliiachia mengi Tanzania, yakiwamo ya kukumbukwa iwe katika nyanja za siasa, uchumi, utamaduni na kadhalika.

Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa kiongozi halisi wa watu aliamini katika utu, jambo ambalo limeanza kupotea kutoka msamiati na pengine istillahi za Kitanzania.

Wengi watakumbuka jinsi ambavyo aliacha kazi ya ualimu katika shule ya St Francis (Pugu) alikokuwa akifundisha na kupata mshahara na kuamua kuzama katika siasa akijitolea na kusaidiwa na wenzake kwa lengo la kuwakomboa katika minyororo ya ukoloni Watanzania, jambo ambalo haliwezekani leo kwa wengi.

Jukumu hilo la kujitoa sadaka kwa ajli ya wengi, limepotea machoni mwa Watanzania hasa wa kizazi hiki ambacho alikiacha mwenyewe, baadhi yao wakiwa wale ambao walinufaika na elimu ya bure tangu ile ya awali hadi chuo kikuu, lakini ambao sasa ndio hao hao ambao wanaubeza mchango wake katika kuinua ustawi wa nchi yake.

TUMTAFAKARI MWALIMU

No comments: