Wednesday, November 9, 2011

SHEREHE, ANASA VILIVYOGEUKA ADA KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU




wanafunzi wakiwa club
     
KUFUNGULIWA kwa vyuo vikuu mbalimbali nchini huambatana na matukio mengi ya burudani kwa wanafunzi.
Huu ndio wakati ambao mbao nyingi za matangazo, kuta za majengo na hata miti inapotumika kutangaza yale yanayojulikana kwa Kiingereza kwa majina ya Fresher’s Ball, Welcome First Year, Fresher’s Night, Bashes  na majina mengine kadhaa
Aghlabu waandaaji wa matukio haya yanayojumuisha mabonanza, matamasha na mikusanyiko ya aina mbalimbali  hutoa hoja  kuwa matukio hayo yanalenga kuwakaribisha wanafunzi wapya wanaojiunga na vyuo.
Lakini uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa matukio yenye mtazamo wa kutoa burudani au starehe kwa wanafunzi ni mambo ya kawaida yanayoandaliwa mara kwa mara vyuoni kiasi cha kuteka fikra za idadi kubwa ya  wanavyuo.
Walengwa wakuu wa matukio haya ni wanafunzi wanaotumia fursa hiyo kama sehemu ya kile wanachikiita “ kupumzisha akili” baada ya mchakamchaka wa masomo katika kipindi fulani.
Hata hivyo,  kwa baadhi ya wanafunzi, mapumziko haya ya akili yamevuka mipaka baada ya kugeuka mateka wa anasa na starehe zisizo na ukomo.Kwao,  vyuo siyo tena mahala pa kusoma bali kufanya starehe
zinazojumuisha ulevi wa pombe, dawa za kulevya,  uzinzi na hata umalaya.
Gideon Joseph, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) anayeishi katika hosteli za Mabibo anasema matukio ya wanafunzi kwenda katika mikusanyiko ya kistarehe ndani na hata nje ya chuo hicho yamekuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa baadhi ya wanafunzi anaowaita kwa majina ya malimbukeni na wageni wa jiji la Dar es Salaam.
“ Kuna watu humu ndani (hosteli ya Mabibo) wamekuja mjini kwa mara ya kwanza, so (hivyo) wako tayari kwenda katika jambo lolote linalotangazwa. Hizi pati wao ndio wanaozijaza, wanafurahia maisha ambayo awali hawakukutana nayo kwa kuwa wanatoka vijijini,’’anafafanua.
Joseph anaongeza kusema kuwa kwa aina hii ya maisha, siku zote wanafunzi wataililia Serikali iwaongeze posho ambazo asilimia kubwa ya fedha zake anasema zinatumiwa na wanafunzi nje ya masuala ya taaluma ikiwamo kufanyia starehe na anasa.
Pia anasema kwa jumla  maisha ya wanafunzi vyuoni yamejaa ukiukwaji mkubwa wa maadili. Wanafunzi wengi aidha kwa kujitakia ama kwa sababu za kimazingira wamekuwa waathirika wa matendo maovu ukiwamo hata umalaya.
Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Magdalena Sebastian anasema chanzo kikuu cha hali hiyo ni uhuru mkubwa walio nao wanavyuo na kukosekana kwa taratibu maalumu za kuwabana kimaadili.
“ Chuo Kikuu huwezi kufukuzwa eti kwa kuwa umelewa  au sijui umelala wapi.Ninachokijua utaondoka mwenyewe chuo kama huja meet (hujafikia) mambo yao ya taaluma kama vile kufeli mitihani au kuwa mtoro wa vipindi. Hivi vinaweza kukufukuzisha chuo,’’anasema.
Hata hivyo, Rais wa  Serikali ya Wanafunzi ya chuo hicho (Daruso),  Simon Kilawa anasema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakina matukio mengi ya starehe na yaliyopo hutokea kwa
kwa shughuli mahsusi.
Anatoa  mfano wa  Fresher’s Night kwa kusema mkusanyiko huo huandaliwa kwa sababu maalumu ya kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza.
 “Hizi bash (matamasha)  ambazo huwa zinaandaliwa na serikali ya wanafunzi, kwa kiasi kikubwa hata chuo  kinakuwa na taarifa nazo. Kwa   mfano tulivyofanya hii ya   Fresher’s night hata askari  polisi wa chuo walikuwepo,” anasema Kilawa.
Hata hivyo, Kilawa ana shaka na mikusanyiko inayoandaliwa na wanafunzi na kufanyika nje ya mipaka ya chuo akisema inaweza ikahusisha mambo yasiyopendeza kwa kuwa haina usimamizi wa serikali ya wanafunzi na uongozi wa chuo.
 “Wanafunzi wa chuo ni watu wazima, huwezi kuwakataza kukutana kufanya jambo wanalotaka. Hizi bash zinazoandaliwa nje ya chuo ni sawa tu na kwenda club,  huwezi kumkataza mtu,” anaeleza.
Kwa upande wake, Noelia Gatera anayesoma mwaka wa pili chuoni hapo anasema: “Faida kubwa ya hizi bash(matamasha) ni kujuana miongoni mwa wanafunzi hasa  wale wa mwaka wa kwanza pia kubadilishana mawazo na kupumzisha akili baada ya pilikapilika za mitihani na  kuagana kwa wale wanaomaliza masomo yao.’’
Lakini vipi kuhusu hasara zake?  anabainisha kwa kusema: “ Hasara ni pale starehe hiyo inapokuwa too much (inapozidi),  kwani kama inavyojulikana mwaka wa kwanza wengi ndio wametoka mikononi kwa wazazi,  kwa hiyo hapo wengi wanajisahau na mara nyingine inaweza  kutokea vurugu lakini  viongozi mara nyingi huwa wanajipanga na kuweka mikakati ya kukabili vurugu hizo.”
Kuhusu kukithiri kwa vitendo vya kihuni katika mikusanyiko hiyo, Gatera anasema: “Hizo ni tabia za mtu ambazo hata kama isingekuwa bash angezifanya kama amedhamiria kufanya hivyo.”
Naye  mhitimu wa Chuo cha Elimu ya Biashara cha Dar es Salaam  (CBE),  Edward Nyangari anaeleza kuwa mara nyingi matukio hayo hulenga kutoa burudani tu kwa wanafunzi ambao baadhi anasema hutumia mikusanyiko hiyo kufanya matendo ya kihuni. Kwa mtazamo wake anasema hafikiri kama mikusanyiko hiyo ina faida yotote katika taaluma.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  (Taaluma), Profesa Yunus Mgaya  anasema kuwa mikusanyiko hiyo ni sehemu ya maisha kwa vijana hao ambao ndio wengi chuoni hapo.
 “Hapa chuoni kuna  wanafunzi wenye miaka 17, 20 na kuendelea, mikusanyiko kama hii ipo  na ni kama sehemu ya maisha yao. Chuo kikuu ni sehemu ya kukua, siyo mambo ya darasani tu yanafanyika hapa, kuna mambo ya kijamii, kimaadili na kitaaluma, sasa hiyo mikusanyiko ni sehemu ya mambo ya kijamii, ”anaeleza.
Pamoja na kukiri kuwa mikusanyiko ya nje ya chuo inaweza kuwa na madhara kwa wanafunzi, Profesa Mgaya anaongeza kusema kuwa mikusanyiko ya ndani ya chuo ambayo aghlabu huendeshwa kwa usimamizi maalumu ina matokeo chanya kwa wanafunzi.
“Ili ufanikiwe darasani ni lazima ufanikiwe pia kwa kujichanganya na wenzako. Kama una msongo wa mawazo, hata darasani huwezi kufanya vizuri,  kwa hiyo mimi naona zina faida chanya kwenye elimu,” anafafanua.
Kwa upande wake, Mshauri wa Wanafunzi wa  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Martha Qorro  hadhani kama viongozi wa vyuo wanapaswa kubeba jukumu la kuwalea wanafunzi watu wazima ambao kimsingi wanajua mbivu na mbichi kuhusu maisha.
Akizungumza na The Citizen , ambalo ni gazeti dada na Mwananchi hivi karibuni, Dk Qorro alisema wanachokifanya wao ni kutoa ushauri hasa kwa wanafunzi wapya kuhusu namna wanavyoweza kutumia vizuri fursa za maisha huru ya wanafunzi vyuoni.
“ ….tunawachukulia kama watu wazima, wajibu wetu ni kuwashauri namna ya kuhimili maisha ya chuon, mwishoni uchaguzi ni wao kuamua njia ipi ya kufuata,’’anasema.

No comments: