BODI YA SHULE YA IST
BODI ya Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) ya jijini Dar es salaam, imetoa msaada wa Kompyuta 20 zenye thamani ya Sh30 milioni kwa shule za msingi za Jimbo la Songwe mkoani Mbeya.
Akikabidhi msaada huo kwa Mbunge wa Jimbo la Songwe Philipo Mulugo, Mkurugenzi wa IST, David Showaver alisema kuwa hiyo ni sehemu ya mpango wao wa kuisaidia jamii katika kukuza kiwango cha elimu na somo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa wanafunzi mkoani humo.
“Huu ni utaratibu wa uongozi wa shule hii kuisaidia jamii hasa katika harakati za kupanua kiwango cha elimu, hasa pale tunapoona mtu mwenye nia ya kujiendeleza inakuwa rahisi kumsaidia. Kama alivyofanya mbunge wa Songwe kugawa kompyuta katika jimbo lake tumeona tumuunge mkono,”alisema Shawver.
Alisema kuwa wameamua kutoa Kompyuta hizo baada ya kuhamasika kwa kumuona Mulugo akigawa Kompyuta ndogo 40 katika jimbo lake mwezi uliopita hivyo kuamua kumuunga mkono katika jitihada za kukuza elimu.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya jimbo lake, mbunge wa jimbo hilo Philipo Mulugo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, aliushukuru uongozi wa shule hiyo kwa msaada huo akieleza kuwa atazigawa kompyuta hizo katika shule zilizo na huduma ya umeme ili wanafunzi waweze kujifunza Kompyuta na kurahisa kazi za ofisini katika Jimbo lake.
“Napenda kuwashukuru viongozi wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika kwa msaada huu, mara baada ya kuona jitihada zangu za kugawa ‘Laptop’ 40 katika jimbo langu la Songwe. Wadau wengine wakilipa kipaumbele somo la Tehama shuleni ni dhahiri linaweza kupata mafanikio,”alisema Mulugo
No comments:
Post a Comment