Na Mdau wa blog hii Habiba Swedi
“WANANCHI wanahitaji kupata taarifa sahihi kila mara ili waweze kuzikabili changamoto zao na pia kufahamu sera na programu mbalimbali za maendeleo ya taifa lao ili kukuza uwajibikaji.”
Hii ni kauli yake Mzee Magendo maarufu kwa jina la Kisposi mkazi wa kijiji cha Ushongo kilichopo wilaya ya Pangani mkoani Tanga aliyeamua kuanzisha maktaba jamii kama msaada wake kwa wanakijiji.
Awali hakujua kama wazo lake lingekuja kuwa jambo muhimu na lenye manufaa kwa watu wengi kiasi cha kuivutia hata Serikali ya kijiji iliyoamua kumpa jengo la kuendesha maktaba hiyo.
“Uongozi wa kijiji uliponipa chumba kwa mara ya kwanza, niliweka vitabu vichache tu vya hadithi na machapisho niliyoyapata kutoka shirika la HakiElimu,’’anasimulia Mzee Magendo na kuongeza:
“Ndani ya mwezi mmoja walikuja watu kama ishirini hivi, lakini baadaye waliongezeka na hivyo kuhitaji chumba kikubwa zaidi.”
Anasema wingi wa watu waliokuwa wakihudhuria katika maktaba yake, ulimlazimu kuomba eneo jingine na ndipo uongozi wa kijiji ulipotoa jengo la kituo cha afya ambalo kwa muda mrefu lilikuwa halifanyi kazi
“Jengo hili lilikusudiwa kuwa kituo cha afya hapa kijijini. Lakini kwa kuwa halikukidhi viwango, tulilifunga kwa muda mrefu”, anafafanua.
Anaeleza kuwa kwa sasa maktaba yake inapokea wasomaji zaidi ya 200 kwa mwezi wakiwemo watoto, wanafunzi, vijana na hata watu wazima.
Ili kuifanya iwe hai anasema amemweka mhudumu anayeifungua kila siku, huku akianzisha tena kikundi cha marafiki wa elimu yeye akiwa mwenyekiti wake.
Marafiki hawa anasema ndio wanaowajibika kuifanyia usafi maktaba hiyo huku yeye akilazimika kununua magazeti ya kila siku ili wananchi wapate taarifa za mambo mbalimbali muhimu kwa ustawi wa maisha yao.
Nje ya maktaba hii michezo kwa watoto huendelea na mara nyingi marafiki hawa wa elimu hutumia eneo hilo kuwasomea hadithi watoto wadogo.
Hali halisi inaonyesha kuwa kijiji hiki chenye shule moja ya msingi inayohudumia wanafunzi ambao wazazi wao ni wahamiaji kutoka kisiwa cha Pemba, kinakabiliwa na changamoto ya utoro kwa wanafunzi.
Watoto wengi huacha masomo na kukimbilia Pwani kuvua samaki ili wapate fedha za kujikimu kimaisha. Hata hivyo, tangu kuanzishwa kwa maktaba hii, watoto hao wamepata ari mpya ya kujisomea baada ya kazi zao.
Hata wale waliokuwa hawajui kusoma na kuandika sasa wanaweza kufanya hivyo, kwani katika maktaba hiyo kuna mtu maalumu anayewafundisha kusoma na kuandika.
Nao watu wazima badala ya kupiga soga ama kujilaza ufukweni baada ya kazi, wanakwenda maktaba kujisomea. Wanafunzi nao wamepata mahala tulivu kwa ajili ya kujisomea na kufanya kazi zao baada ya saa za shule.
Kwa mujibu wa Mzee Magendo, changamoto kubwa inayoikabili maktaba hiyo ni uhaba wa vitabu vya masomo ya sayansi, hisabati na sera mbalimbali za taifa. Hata hivyo, anasema anajitahidi kuwasiliana na wadau mbalimbali ili kuvipata vitabu hivyo.
Anaamini kuwa ndani ya miaka mitano ijayo, maktaba itakua na kuweza kutoa huduma kwa jamii pana zaidi.
Anaongeza kusema kuwa maktaba hiyo itakuwa miongoni mwa vivutio vya utalii kwa wageni wanaozuru kijiji hicho kilichopo kando ya bahari ya Hindi huku kikiwa kimejaaliwa vivutio mbalimbali wakiwemo kasa wa kisiwa cha Maziwe.
No comments:
Post a Comment