MAHAKAMA YA NUNGE MOROGORO
Morogoro
POLISI mkoani Morogoro linawashikilia watu wawili, mmoja kwa tuhuma ya kumbaka mtoto wake mwenye umri wa miaka (10), huku mwingine akituhumiwa kumpa mimba na kumwachisha masomo mwanafunzi wa darasa la sita mwenye umri wa miaka (12).
Watuhumiwa hao majina yamehifadhiwa ni wakazi wa Kata ya Chamwino, Manispaa ya Morogoro ambao walikamatwa Oktoba 4, mwaka huu katika majira tofauti wakikabiliwa na tuhuma hizo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia Blog hii na kuthibitishwa na polisi zimedai kuwa mtuhumiwa wa kwanza ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya ulinzi ya Moku Security Guard alikamatwa kwa tuhuma za kumbaka binti yake mara nyingi tangu mwaka jana bila kujulikana.
Mratibu wa Elimu Kata katika kata hiyo, Roxana Kilelo alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akimfanyia vitendo hivyo binti yake nyakati za usiku wakati mama yake alipokuwa akienda kazini katika kiwanda cha tumbaku (TTPL).
Alisema siri hiyo imedumu kwa muda mrefu na kwamba kila alipokuwa akimbaka mtoto wake alikuwa akimtishia kwa kisu na kumwoonya kutotoa siri hiyo vinginevyo angemfanyia vitu vibaya.
Mratibu huyo alisema Oktoba 21, mwaka huu alipofanyiwa kitendo hicho alilazimika kumweleza mamayake mzazi kutokana na kusikia maumizi makali chini ya kitovu.
Alisema kuwa baada ya kumwambia mama yake alipeleka taarifa kwa mjomba wa mtuhumiwa huyo ambaye pamoja na mama huyo hawakuchukua taarifa yoyote mpaka hapo taarifa hizo zilipomfikia mjomba wa binti huyo na majirani ambao walizifikisha kwa mwenyekiti wa mtaa, Amina Nassoro.
Kilelo alisema mwenyekiti wa mtaa huo kwa kushirikiana na walimu wa shule ya msingi Jitegemee ambako anasoma binti huyo na diwani wa kata hiyo, Joramu Masienene walimhoji binti huyo na kukiri baba yake mzazi alikuwa akimbaka kwa muda mrefu.
Baada ya mahojiano hayo mtuhumiwa alikamatwa na kufikishwa kituo kikuu cha polisi huku binti huyo akifikishwa katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kufanyiwa vipimo ikiwa ni pamoja na kupima vinasaba (DNA) na vipimo vingine vilavyotarajiwa kufanyika jana.
Katika tukio lingine, mratibu elimu kata hiyo alisema mtuhumiwa mwingine aliyefikishwa kituo kikuu cha polisi kwa tuhuma za kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kambarage, Manispaa ya Morogoro.
Alisema mtuhumiwa huyo alibainika kutenda kosa hilo baada ya uongozi wa shule hiyo Julai mwaka huu kuendesha msako mkali wa kuwasaka wanafunzi watoro na taarifa kutoka kwa wanafunzi wengine walibainisha kuwa binti huyo haendi shule kutokana na kupewa mimba na dereva wa bodaboda.
Mratibu huyo wa elimu kata alisema uongozi wa shule hiyo wakishirikiana na ofisi yake walimhoji kwa kina mwanafunzi huyo na kukiri kuwa ana mimba na baada ya kupimwa alibainika kuwa ni mjamzito.
Ilidaiwa kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa na mahusiano ya muda mrefu na mwanafunzi huyo.Alisema kwa kushirikiana na uongozi wa shule, polisi jamii walimwekea mtego mtuhumiwa huyo katika kituo cha Mziwanda na polisi jamii kujifanya abiria ambaye alimchukua moja kwa moja mpaka kituo cha polisi cha Chamwino kabla ya kufikishwa kituo kikuu.Watuhumiwa wote wawili wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya polisi kukamilisha upepelezi wao.
No comments:
Post a Comment