Na Mtemi Zombwe
AGOSTI mwaka huu niliandika kwa wiki mbili mfufulizo kuhusu aina ya mtalaa wetu kwa kubainisha udhaifu na uzuri wake.
Wasomaji wengi walituma ujumbe mfupi na baadhi kupiga simu kunitaka nitoe maoni yangu kuhusu aina ya mtalaa unaotufaa Watanzania katika karne ya 21. Makala haya ni sehemu ya mjadala huo. Endelea...
Nianze kwa kurejea tafsiri ya neno mtalaa kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali. Neno hili linatokana na lugha ya Kilatini likimaanisha ‘kuendesha kozi’.
Kwa kuzingatia maana ya asili ya neno lenyewe na kwa mujibu wa mwanazuoni Oliva katika Kitabu chake “The curriculum: Theoretical dimensions”, (1997) anaelezea maana ya mtalaa kwa kuzingatia mambo 12.
Mambo haya yanajumuisha kile kinachofundishwa shuleni, seti ya masomo, maarifa, programu ya masomo, seti ya vitu vya kujifunza, orodha ya kozi, seti ya malengo ya ufanyaji kitu na kozi ya kujifunza.
Pia anasema mtalaa ni kila kitu kinachoendelea shuleni ukijumuisha mambo yanayofanyika nje ya darasa, usimamizi, na uhusiano kati ya mtu mmoja na mwingine na mjumuiko wa uzoefu mbalimbali anaoupata mwanafunzi awapo shuleni. Huo ndio mtalaa.
Ieleweke kuwa mtalaa wa elimu ni suala la jamii ambalo mipango na taratibu zake zinahitaji kushirikisha wadau wote katika jamii. Madhumuni ya elimu kwa jumla ni kuifanya dunia kuwa mahali pazuri pa kuishi watu wa kizazi cha leo na vizazi vijavyo.
Mtalaa unakusudiwa kuwapa watu maarifa na ujuzi watakaoutumia vizazi na vizazi ili kuwasaidia kupata njia mpya na bora zaidi ya kutatua matatizo yao ya kiafya, kiuchumi, kijamii na mengine yanayohusu mazingira wanayoishi.
Kwa Tanzania mtalaa unaotufaa ni ule unaomkomboa Mtanzania kifikra, kiakili na kimwili. Unaomwezesha binadamu kujikwamua kimaisha, kujithamini na kujipenda kama Watanzania ambao ni watu kamili tuliomo katika nchi nzuri yenye thamani kubwa na rasilimali za kutuendeleza.
Mtalaa wa elimu uwaandae Watanzania wawe na uwezo wa kuchambua, kutafakari kuwa wadadisi na wachambuzi wanaouliza maswali na kutafuta suluhu ya matatizo yanayoikabili jamii sio kutegemea wahisani.
Kazi kubwa ya kwanza ya mtalaa bora ni kuwafanya watu wajitambue kuwa sisi sote ni waathirika wa elimu ya kikoloni. Tunahitaji kushirikiana na wadau wa sekta na maeneo mbali mbali ya jamii yetu tueleweshane kwamba tunahitaji kujikomboa.
Ukisoma makala ya wataalamu katika sekta mbali mbali utaona kwamba baadhi wanakubali kuwa tuna mawazo ya utegemezi ambayo nayatafsiri kuwa ni dalili za utumwa.
Kwa hiyo, jambo la uelewa wa pamoja kama jamii katika suala la kujitambua, naliona ni la muhimu na la msingi. Kwanza, jambo la kuelewana, kukubaliana na kuweka mwelekeo halina gharama kubwa zaidi ya rasilimali watu ambayo tunayo kwa wingi.
Pili, bila kuwa na uelewa, makubaliano na ushiriki wa wadau wengi, ni vigumu kupambana na umaskini na maradhi. Kwa hiyo, mtalaa wa elimu itakayotoa ujinga, utatupa mwanga wa kuyafanya hayo mengine kwa manufaa ya jamii.
Tatu, tusipoanza na hili la kuondoa ujinga na kujikwamua kwenye utumwa, ni rahisi kudanganywa na wajanja kwa manufaa yao binafsi au ya jamii zao.
Haya ndio yanayofanyika leo. Wasomi wanalalama ndani ya nchi yao, wageni wajanja wananufaika na chi yetu ilhali wazawa tukibaki masikini. Fikiria! Watanzania kama mume na mke hatuwezi kukaa na kujadili mambo ya familia hadi tuambiwe kwa ‘Hisani ya watu wa Marekani!’
Mtalaa wa elimu uifanye elimu yetu iwe sehemu ya jamii na kamwe isijaribu kuwatenganisha wasomi na jamii zao. Wasomi wapewe changamoto ya kuandaa vitabu na majarida yenye taarifa na maarifa mengi katika lugha rahisi kwa ajili ya shule zetu na watoto wetu ili wasome tunayotaka wayajue kwa ajili ya maendeleo badala ya kutegemea vitabu vilivyoandaliwa na wazungu, tena baadhi vikiwa na maudhui ya kutudhalilisha.
Niliwahi kusema huko nyuma kuwa mtalaa unaotuelekeza tujaribu kujifananisha na wazungu hautufai. Kamwe hatuwezi kuwa kama wazungu na kwanza wao hawatutaki na hawapendi tuwe hivyo.
Ndio maana japo kuna Waafrika wengi Ulaya na Amerika ambao ni maarufu na wana mchango mikubwa kwenye fani mbalimbali kama michezo, miziki na elimu, bado siku zote wanadhihakiwa na kuitwa Nyani!
Japo kuna matatizo mengi katika nchi yetu, wazungu hawaongelei kuleta misaada ya kuwafanya watoto wetu wajue kusoma na kuandika ili wajitambue na wajitegemee. Sasa tunaambiwa watoto wetu wawe mashoga ndiyo misaada ipatikane kwa urahisi.
Mtalaa wa elimu unaotoa wasomi ombaomba wenye fikra tegemezi na wasio na aibu wala soni ya kufedheheshwa na wahisani, ni mtalaa dhaifu. Huwezi kuwa jasiri wa kuomba na ukafikiri sawasawa. Ombaomba yeyote huwa hafikiri sawasawa. Kuwa ombaomba ni ishara ya kugota kufikiri na kubuni.
Mtalaa tunaohitaji ni ule unaochochea fikra za kuitafiti dunia. Tuanzishe tafiti zinazolenga kuendeleza jamii zetu katika maeneo ya sera na mipango endelevu kwa kushirkisha wananchi na matokeo yaandikwe kwa lugha yetu ya Kiswahili ili wananchi wengi wapate taarifa na wazitumie kujiletea maendeleo.
Mtaala unaotufaa ni ule unaotuchagiza kutumia teknolojia kutengeneza fursa mpya na kujiletea maendeleo. Mtalaa wa elimu utuongoze Watanzania kuutumia utandawazi kujielimisha na kunufaika kibiashara, uvumbuzi na mawasiliano sio kulimbukia utandawazi na kutufanya kuwa watumwa wake.
Mathalani, mtalaa wa elimu uwajengee watoto wetu uelewa kuwa utandawazi ni fursa ya kusonga mbele na siyo fursa ya kuibiwa kama vile kupitia teknolojia ya habari na mawasiliano ambapo watu sasa wanadhani maendeleo ni kubahatisha kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya mkononi kisha kushinda nyumba au gari! Itaendelea.....
No comments:
Post a Comment