Baadhi ya wanafunzi
KAMA kuna shule yenye historia ndefu na inayovutia wilayani Masasi, Mkoa wa Mtwara, ni sekondari ya wasichana ya Masasi.
Shule hiyo ya bweni, ilianzishwa mwaka 1965 na shirika la Kimisionari la Wakatoliki (Salvastorian Fathers). Mwaka 1970 ilichukuliwa na serikali.
Ilianza na kidato cha kwanza hadi cha nne. Mwaka 2007, ikaanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha tano na sita; lengo likiwa ni ifikapo mwaka 2012 kubaki shule yenye sekondari ngazi ya juu (A-Level) pekee – kitado cha tano na sita.
Hiyo maana yake, kwa wale wahitimu wa kidato cha nne waliomaliza mitihani yao mwezi uliopita, wakifaulu wataendelea na kidato cha tano hapo. Kuanzia mwakani, Masasi Girls yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 480, haitakuwa na kidato cha kwanza mpaka cha nne.
Historia inayovutia ya shule hiyo ni ukweli kuwa inajivunia mafanikio kwa kuwa viongozi kadhaa katika taasisi za serikali na binafsi, wamepitia shule hiyo kupata elimu kabla ya kuongeza viwango vya elimu katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Miongoni mwa wahitimu wa shule hiyo ambayo sasa inaongozwa na Mwalimu Renalda Tesha, ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda.
Makinda, ambaye pia ni mbunge wa Njombe Kusini, mkoani Iringa, kiongozi ambaye hapo kabla, alishika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini, alijiunga na shule hiyo mwaka 1965 alipoingia kidato cha kwanza.
Spika Makinda ameikumbuka shule iliyomjenga. Alifika shuleni wiki ya mwisho ya mwezi uliopita. Mkuu wa Shule, mwalimu Tesha anasema Makinda alikwenda kwa ajili ya kuangalia maendeleo yake.
“Mheshimiwa alifika mpaka kwenye kitanda alicholala bwenini. Alijisikia furaha kukuta bado vitanda vinavyotumika ni vya chuma,” anasema mwalimu Tesha.
Lakini, Makinda alijitoa katika lengo kuimarisha zana na vitendea kazi shuleni hapo. Aliahidi kupeleka kompyuta mbili na kuwasaka wahitimu wote waliopitia hapo ili waisaidie hadi kuwa na hadhi nzuri kama ilivyokuwa zamani.
Spika Makinda aliahidi kuwasiliana na Watanzania wengine waliosoma shule hiyo baada ya kuelezwa katika taarifa ya shule maendeleo na changamoto zinazoikabili.
Shule hiyo ina uhaba wa walimu. Wakati mkuu wa shule anasema lengo ni kuwa na walimu 25, lakini kwa sasa wapo walimu 16. Walimu wanaohitajika kuongezwa katika shule hiyo ya mkondo wa Fizikia, Kemia na Baiolojia (PCB), ni wa somo la Kemia.
Mwalimu Tesha anasema wanashindwa kuunganisha mkondo huo na mingine ya Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM) na Kemia, Baiolojia na Jiografia (CBG), kwa sababu ya kukosekana walimu wa Kemia.
Alipokuwa anafurahia kupokea ahadi ya msaada wa kompyuta mbili kutoka kwa Spika Makinda, Mwalimu Tesha alifunua ukubwa wa tatizo la zana hiyo muhimu katika shule inayofundisha masomo ya sayansi.
Usalama wa shule na mali zake pia upo hatarini kutokana na shule kukosa uzio kuzunguka majengo yake ambayo nayo yamechakaa na kuhitajika matengenezo makubwa.
“Tunahitaji msaada wa kifedha tuwezu kukarabati majengo kwa kweli yamechakaa. Fikiria majengo ya tangu shule ilipoanzishwa mwaka 1965, na hayajawahi kufanyiwa matengenezo makubwa,” anasema Mwalimu Tesha.
Ingawa upatikanaji wa umeme katika shule hiyo ni wa uhakika kwa saa 24, miundombinu ya njia za umeme kwenye madarasa, mabweni, jikoni, bwalo na jengo la utawala imechakaa mno na kuhitaji matengenezo ya haraka.
Ukosefu wa uzio shuleni ni tatizo jingine sugu shuleni hapo ambako kumetokea matukio mengi ya uhalifu kwa watu kuingia ndani ya shule. Mwalimu Tesha anasema mwaka 2008 mlinzi wa shule aliuawa baada ya kunyongwa na majambazi walioingia shuleni kwa nia ya kuiba.
Hawakuiba kitu baada ya kuona wamemuua mlinzi katika harakati za kumdhibiti ili kutekeleza uhalifu wao.
Pia kutokuwepo kwa uzio kumewapa viongozi wakati mgumu kudhibiti nyendo za wanafunzi kwa kuwa baadhi yao hutoka kinyume na ratiba. “Unajua kwa sababu hatuna uzio wanafunzi hawa ambao ni wasichana wanajitokea tu na ndio maana baadhi wanakumbwa na mimba,” anasema.
Akipitia kumbukumbu za tatizo hilo katika miaka mitatu kuanzia 2009, Mwalimu Tesha anasema wanafunzi 11 wa shule hiyo wamethibitishwa kukabiliwa na ujauzito.
Mwalimu Tesha anasikitika kwamba wasichana wote hao walikimbia shule. “Tuna mpango wa kupunguza tatizo la kutoka na kuingia maeneo ya shule bila utaratibu. Jitihada zetu ni pamoja na kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kutafuta wafadhili,” anasema.
Anakumbuka ahadi aliyowahi kuitoa Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, akisema angesaidiana na uongozi wa shule kutafuta misaada.
Shule ya Masasi Girls haina maji safi na salama ya kutosheleza mahitaji. “Tuna visima viwili, kimoja cha mkono na kingine cha mashine, lakini mahitaji ni makubwa… wananchi wa jirani na shule yetu wanategemea maji hayahaya,” anasema.
Mwalimu Tesha analalamikia uhaba wa vyoo. Vyoo vilivyopo ni 46 vya matundu lakini vingi vimebomoka kutokana na mvua nyingi za masika zilizonyesha mapema mwaka huu.
“Tunahitaji matundu 36 ya vyoo; mabwenini matundu 24 na madarasani matundu 12 kwani vyoo 20 vya kuvuta vilivyopo kwenye mabweni na 26 katika jengo la madarasa havifanyi kazi,” anasema.
Shule hiyo inakabiliwa na tatizo la usafiri. Haina chombo chochote cha usafiri na kuwawia vigumu kutoa msaada kwa wanafunzi au wafanyakazi wanapougua.
“Hali inakuwa ngumu sana tukipata mgonjwa usiku… hospitali ya wilaya iko mbali (kilomita nane hivi),” anasema.
Yapo maendeleo Masasi Girls. Kitaaluma, Mwalimu Tesha anasema mwaka 2009 walipoanza kutoa wahitimu wa kidato cha sita, walitoa wanafunzi saba wa daraja la kwanza, 14 wa daraja la pili na kumi daraja la tatu. Hakukuwa na aliyepata sifuri.
Mwaka 2010 walifaulisha wanafunzi wanne wa daraja la kwanza, 14 la pili, 36 la tatu na mwanafunzi mmoja tu daraja la nne. Kwa mara nyingine hakuna aliyepata sifuri.
Kwa mwaka huu, anasema shule ilitoa vijana wanne wa daraja la kwanza, 17 la pili, 83 la tatu na 14 wa daraja la nne. Kwa mara ya kwanza walipata wahitimu wanane waliofeli.
Nimekuta mazingira mazuri ya maandalizi ya chakula jikoni. Vyombo vya kisasa vya kupikia kama vile masufuria na sehemu za kupakulia chakula; meza na mabenchi kwenye bwalo la kulia chakula. Hakuna foleni wakati wa chakula.
Mwalimu Tesha anasema wanatarajia kuongeza vitabu vya kufundishia na vifaa vingine vya kutolea taaluma huku wakifikiria kuanzisha utaratibu wa kutoa huduma ya chai na chakula cha mchana kwa wafanyakazi wao.
chanzo mwanahalisi
No comments:
Post a Comment