Tuesday, November 22, 2011

MADHALA YA KUPANGA MITAANI NI MAKUBWA

 

na mdau Pamela Chilongola

SEPTEMBA 28 mwaka huu, baadhi ya vyombo vya habari viliripoti habari ya mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Makoka ya jijini Dar es Salaam aliyeamua kukatisha uhai wake kwa kujinyonga.
Diana Abbas (16) alijinyonga chumbani kwake wilayani Temeke na wala hakuacha ujumbe wowote kuhusu  sababu za kuchukua uamuzi huo wa kikatili.
Ni dhahiri  marehemu alikuwa akiishi peke yake chumbani jambo lililosababisha wepesi wa kukatisha maisha yake.
Kwa muda mrefu sasa  kumekuwapo na utaratibu wa wanafunzi wa shule za sekondari kupanga vyumba mitaani wanakoishi kwa kujitegemea wakikosa usimamizi wa wazazi na hata walimu.
Mkazi wa Magomeni,  Maria Mlugu anaamini kifo cha Diana kingeweza kuzuilika kama angekuwa anaishi na wazazi ama walezi nyumbani.
Huyo binti inawezekana alikuwa akiishi peke yake hivyo ikawa rahisi kujinyonga. Kama angekuwa na wenzake au anaishi nyumbani, labda asingechukua uamuzi huo mzito.
Hata hivyo,  Mlugu anawashukia baadhi ya wazazi akiwalaumu kuwa kichocheo cha wanafunzi hususan wa kike  kupanga mitaani. 
….. Watoto wa sasa wameachwa kuwa huru sana. Siyo wote wanaopanga vyumba hawana wazazi wa kuwatunza. Tatizo ni kuwa baadhi yetu sisi wazazi hatuwajibiki ipasavyo katika malezi.
Sijui huko mikoani lakini kwa mkoa kama Dar es Salaam, mzazi anaishi Kigamboni anampa ruhusa mwanawe kwenda kupanga Kimara, kwa nini asiwe na utaratibu wa kufuatilia maisha yake kama kupanga ni lazima kwa huyo mwanafunzi? anahoji.
Uzoefu kuhusu utaratibu wa wanafunzi kupanga vyumba unaonyesha wako wanafunzi waliopanga vyumba, huku wakiendelea na malezi mazuri waliyopata nyumbani.
Lakini kwa baadhi yao, hii ndiyo fursa pekee ya kufanya wayatakayo hasa vitendo vya kihuni ikiwa ni pamoja na uhusiano wa ngono na wanaume.
Aidha, hii ndiyo fursa inayotumiwa kwa kiasi kikubwa na wanaume wakware kuwarubuni wanafunzi wa kike ambao mwishowe baadhi yao hujikuta wajawazito.
Mtazamo wa mwalimu Alphonce Banda ni kuwa baadhi ya wanafunzi wanaamua kupanga ili wawe huru kufanya mambo yao kama anavyobainisha:
Sio wote wanaopanga wana sababu za maana. Kwa wengine hiyo ndiyo fursa ya kukimbia udhibiti wa wazazi nyumbani… hili ni tatizo katika mfumo wetu wa elimu. 
Anaongeza: Viongozi na wazazi wawe imara kukemea tabia hii kwani hivi sasa watoto wa kike wanaishi kama wake za watu mitaani. Tutafakari hili ni tatizo kubwa, mbona sisi zamani hatukuwa tunaishi mitaani?
Mkazi wa Arusha, Fabian Estomihi  amewapangisha wanafunzi mbali mbali wa shule za sekondari anayelalamika kuwa  pamoja na kuwabana na kuwapa nasaha kimalezi, wanafunzi hao wameshindwa kumsikiliza.

Nyumba yangu haina ukuta, kwa hiyo huwezi kuwabana sana.  Lakini huwa najaribu kuzungumza nao kama mzazi ingawa naona kabisa hawanielewi. Wengi huwa wanafanya umalaya mpaka roho inakuuma, wa kiume na wa kike wote, hakuna afadhali, anasema na kueleza kuwa njia  pekee ya kudhibiti hali hiyo, ni wazazi kuhakikisha wanawalea watoto wao katika maadili.
Huwezi kusema shule zijue kila mahali mwanafunzi anapokaa ili ziwadhibiti, lakini mtoto mwenyewe kama amelelewa katika mazingira ya kuweza kufanya kila jambo na kuchukua uamuzi peke yake hata akikaa mbali na mzazi,  hatohitaji mtu wa ziada wa kumlinda kwa sababu anajua anafanya nini, anasema.
Kwa upande wake, Bosco Antony anatetea wanafunzi kupanga akidai kuwa wanasukumwa kufanya hivyo kwa sababu za kimazingira.
Antony anayesoma katika Shule ya Sekondari Kitunda iliyopo jijini Dar es Salaam anasema wanafunzi wengi wamekuwa wakipangiwa kusoma shule za mbali ambazo hazina mabweni, hivyo kuwalazimu kuishi katika mitaa iliyo jirani na shule kuepuka gharama na adha ya usafiri.

Mimi naishi Ubungo Maji lakini shule ya kata niliyopangiwa iko  Kitunda. Unaweza kuona umbali ulivyo na pia matatizo ya usafiri wa daladala. Mimi siishi mtaani lakini siwalaumu wenzangu wanaopanga kwani wengine wanakaa mbali, hivyo solution (ufumbuzi) kwao ni kupanga, anaeleza.
Kwa upande mwingine walimu akiwamo Augen Mluge anayefundisha katika Shule ya Sekondari Mtombozi iliyoko  Morogoro Vijijini, wanasema hawana sababu ya kuwazuia wanafunzi kupanga vyumba kwa kuwa shule nyingi  hazina mabweni kwa ajili ya kutumiwa na wanafunzi wanaoishi mbali na shule.
 Kama huku vijijini shule nyingi zilizojengwa hazina mabweni.  Utakuta mwanafunzi anakaa eneo la Msalabani, lakini  amechaguliwa Sekondari ya Mtombozi,   huyu mwanafunzi hawezi kutembea umbali mrefu hivyo inamlazimu apange chumba karibu na shule, anaeleza na kuongeza kuwa njia pekee ya kuzuia wanafunzi kupanga mitaani ni ujenzi wa mabweni shuleni.

CHANZO

No comments: