Tuesday, November 29, 2011

KUPITIA Dr. BILLAL CHUO KIKUU HURIA CHAOMBA PUNGUZO LA VAT


Makamu wa Rais Mh. Dr. Gharib Billal

Na Sanjito Msafiri
SERIKALI imeombwa kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kwa majengo yanayotumiwa na Chuo  Kikuu Huria cha Tanzania  (OUT) ili kupunguza gharama za uendeshaji.

Ombi hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Baraza la OUT, Profesa Samweli Wangwe   mbele ya Makamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal, wakati wa mahafali ya 23 ya chuo hicho
yaliyofanyika mwishoni katika Kijiji cha Bungo, kilichoko Kibaha mkoani Pwani.

Wangwe alisema kuwa chuo hicho kwa sasa kinakabiliwa na changamoto nyingi katika uendeshaji wa kutoa elimu kwa wanafunzi wake jambo ambalo linakwamisha uharakishaji wa kuleta ukuaji wa elimu katika nyanja mbalimbali.

Alizitaja baadhi ya changamoto zinazokikabili chuo hicho kuwa ni pamoja na ukosefu wa wahadhiri wa ndani , gharama za malipo kwa wahadhiri hao na fedha kwaajili ya uboreshaji wa miundo mbinu ya majengo.

Aidha alisema ili kuboresha utoaji wa elimu kwa haraka pamoja na mambo mengine,  chuo hicho kina mpango wa kutoa elimu kwa njia ya kielektroniki ili kupunguza gharama za machapisho.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais Dk Bilal, alisema Serikali ina mpango wa kuweka miundombinu mizuri ya  kukiendeleza Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) ili kiweze kutoa elimu bora ndani na nje ya nchi.

Dk Bilali alisema kuwa mchango wa chuo hicho ni mkubwa katika kutoa elimu ya juu hapa nchini na nje ya nchi ya Tanzania hivyo lazima mazingira ya utoaji elimu huria na masafa yaboreshwe.

Alisema changamoto zinazokikabili chuo hicho zinafanana na za vyuo vikuu vya umma ikiwa ni pamoja na uhaba wa wahadhiri hali inayosababisha kutotolewa elimu bora.Katika mahafali hayo zaidi ya wahitimu 2000 walikabidhiwa vyeti na shahada mbalimbali.

No comments: