Tuesday, November 29, 2011


Na Kassim Baruani
Wazazi ni watu muhimu sana katika maisha ya watoto,hasa kuanzia pale wanapoanza kupata akili ya kujifunza mambo mbalimbali kabla ya kufundishwa na walimu shuleni na kujifunza mambo mengine kutoka kwa watu wengine.

Mambo wanayojifunza watoto kutoka kwa wazazi wao yanakuwa na athari kubwa katika maisha yao kwani kwa kiasi kikubwa ndiyo yanayochangia kuwafanya wawe watu wa aina fulani huko baadae.

Ili watoto waweze kujifunza mambo mbalimbali na yaliyo mazuri kutoka kwa wazazi wao inabidi kuwe na ukaribu kati yao na wazazi.Hapa ndipo kinapoingia kipengele cha umuhimu wa wazazi kuwa ndio marafiki wa kwanza wa watoto.Wazazi,hasa akina baba,hawatakiwi kuwa madikteta fulani,au wakali sana kiasi cha kufikia watoto kuwaona kama “magaidi” au maadui.

Wazazi wanapokuwa wakali kupita kiasi hupelekea watoto kuwaogopa na kuwa na nidhamu ya uoga kwao,kitu ambacho hakimaanishi kwamba wanawaheshimu.Matokeo yake ni kwamba watoto hawatajifunza chochote cha maana kutoka kwao ambacho kitawajenga katika maadili mazuri.

Ukaribu kati ya watoto na wazazi unapokosekana ndipo watoto huanza kuutafuta ukaribu huo nje kwa watu wengine ambao mara nyingi huishia kuwapotosha kwa kuwafundisha mambo ambayo si mazuri na kupelekea watoto hao kuwa sifuri katika suala zima la maadili.Wazazi wengi wanapokuja kugundua kwamba watoto wao wanafanya mambo ambayo si mazuri husikika wakisema,"mitoto ya siku hizi bwana,sijui ina matatizo gani?!",na lawama zote hutupiwa watoto wakati ukweli ni kwamba lawama hizo zinawastahili wazazi kwa kutowaongoza watoto hao tokea mapema ili wasiingie katika dimbwi hilo la ukosefu wa maadili.

Kuwa wazazi haimaanishi kwamba jukumu lao pekee ni kuhakikisha kwamba watoto wanakula vizuri,wanavaa vizuri,wanaenda shule na kuwapatia vitu vyote ambavyo vinaweza kununulika kwa pesa.Jukumu kubwa la wazazi pia ni kuhakikisha kwamba watoto wao wanakuwa katika maadili mazuri.Hii itawezekana endapo wazazi watakuwa karibu na watoto wao kwa kucheza nao,kuongea nao ili kujua kinachoendelea katika maisha yao ya kila siku nyumbani, shuleni, n.k.

Wazazi kuwa karibu na watoto haioneshi kwamba wazazi ni dhaifu.Pia si kweli kwamba watoto hawatakuwa jasiri na watakuwa wajinga wajinga kama ambavyo watu wengi husikika wakisema.Ukaribu kati ya wazazi na watoto wao hujenga mapenzi kati yao ambayo ni muhimu sana.Pia huwajengea watoto msingi imara ambao utakuja kuwasaidia katika maisha yao huko baadae,hasa pale na wao watakapokuja kuwa wazazi.

Umefika wakati sasa wa wazazi kubadilika na kuachana na kasumba zisizo na msingi ili kuweza kuhakikisha kwamba watoto wanakuwa katika misingi ya maadili mazuri.Kwa kufanya hivyo itasaidia sana pia kudhibiti wimbi la mmomonyoko wa maadili katika jamii.

chanzo (nifahamishe)

No comments: