Rais Jakaya Kikwete amesema walimu wa Tanzania wanao uwezo wa kufundisha somo la Kiingereza vizuri kama wakiwezeshwa kwa kupatiwa vitabu vya kiada vilivyojaribiwa, kutahiniwa na kupimwa kwa ubora wake kama moja ya njia muhimu za kuinua kiwango cha elimu nchini.
Aidha, amewataka wadau wa elimu kushirikiana ili kubaini vitabu hivyo ambavyo alisema kwa miaka mingi vimethibitika kuwa bora zaidi katika kuwafundishia watoto na wanafunzi wa Tanzania.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana Ikulu, Dar es Salaam wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Katy Allen, mtunzi wa vitabu vya lugha ya Kiingereza vya Oxford.
Katy alikuwa anamwelezea Rais Kikwete kuhusu jitihada ambazo shirika lake lisilokuwa la kiserikali la Village Education Project Kilimanjaro (VEPK) limekuwa linafanya kuchapisha na kuboresha kutunga vitabu vya kufundishia na kujifunza lugha ya Kiingereza vya Oxford English Books vilivyokuwa vinatumika kufundishia lugha hiyo nchini katika miaka ya nyuma.
Katy alisema shirika lake linaamini kuwa kama vitabu hivyo vikianza kutumika tena katika shule za Tanzania, ufundishaji wa lugha ya Kiingereza unaweza kuboreka haraka zaidi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment