Wednesday, November 16, 2011

CWT WAUZA BENKI KWA WALIMU


Raisi wa cha walimu Gratian Mkoba

na Mdau Lilian Lugakingira

WALIMU nchini wametakiwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na chama chao za kuanzisha benki kwa ajili ya kuwainua.Akizungumza na walimu Wilaya ya Missenyi juzi, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, alisema wadau wakuu wa benki hiyo watakuwa ni walimu wenyewe na watatakiwa kununua hisa.

Mkoba alisema  benki hiyo itakayoanzishwa, itakuwa na matawi kila mkoa na baadhi ya masharti ya kuanzishwa tayari yametimizwa, ikiwamo kuwa na mtaji wa Sh2 bilioni.

Alisema walimu wamekuwa wakinufaisha benki mbalimbali kupitisha mishahara yao na kuchukua mikopo, wakati kama wangekuwa na benki yao wangeweza kunufaika zaidi, maana faida ambayo zinapata benki nyingine, itabaki katika benki yao kwa maendeleo yao wenyewe.
Rais huyo alisema hatua ya kwanza ilikuwa ni kujenga ofisi za CWT kila mkoa na kwamba, hawataingia gharama nyingine ya kujenga benki, badala yake majengo hayo ya ofisi ndiyo yatakayotumika.

Pia, Mkoba aliwataka walimu kuacha kujiingiza katika migogoro isiyo na faida kwao, ikiwamo kudhamini watu wasio na undugu nao mahakamani kutokana na tamaa ya fedha wanazopewa kwa ajili hiyo.

“Kesi za walimu kudhamini watu zimekuwa kero, mnawadhamini wanatoroka mnakamatwa, acheni tamaa ya hela, chama hakitajihusisha na kesi yoyote ambayo mwalimu amemdhamini mtu asiye na undugu naye, iwapo atamtoroka,” alisema Mukoba.

Aliwataka walimu kuelewa vizuri mazingira yao ya kazi, kuheshimu kazi yao na kuepuka kuishi kwa vitisho ili wafanikiwe.Mkoba yupo ziarani mkoani Kagera, atatembelea wilaya zote kuzungumza na walimu kuhusu maendeleo ya chama chao na kusikiliza matatizo yanayowakabili, ili yatafutiwe ufumbuzi.

No comments: