Monday, October 31, 2011

HALMASHAURI ZATAKIWA KUENDELEZA WALIMU

Image

HALMASHAURI za manispaa, miji na wilaya nchini zimetakiwa kuhakikisha zinawaendeleza walimu na wakuu wa idara katika sekta ya elimu, ili kufanya kazi kwa urahisi zaidi, kujiamini na kuwa chachu ya mabadiliko kwenye nyanja ya elimu.
Akizungumza kwenye mahafali ya Chuo cha Uongozi na Uendeshaji Elimu (Adem) juzi, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, alisema ili sekta ya elimu nchini ipate viongozi bora, lazima wanataaluma hao wapate mafunzo yatakayowawezesha kutekeleza sera na sheria mbalimbali za Serikali.

Mulugo alisema kutokana na suala hilo ni muhimu kwa halmashauri zote kuwa na utaratibu wa kutoa ruhusa kwa viongozi wanaotaka kwenda kujiendeleza katika fani hiyo, sambamba na kutenga bajeti zao za kuwezesha idadi kubwa ya walimu kwenda kuongeza ujuzi zaidi.

“Serikali itaangalia uwezekano na kuwapo kwa bajeti hata ndogo ya kuwezesha watu watoke huko kwenye halmashauri waje hapa Adem kujiendeleza, najua hapa ada zake ni ndogo kwa sababu ni chuo cha Serikali tutachangia, tutajitahidi kwa kushirikiana na halmashauri zetu nchini tutazishawishi kila mara zijitahidi kutenga bajeti kwa ajili hiyo,” alisema Mulugo.

Mkuu wa Adem, Dk Samwel Nguni, aliomba Serikali kutoa mapendekezo ya kila kiongozi idara ya elimu kupata mafunzo ya uongozi ili kuleta chachu ndani ya idara zao, halmashauri, mkoa na taifa.

“Nashauri Serikali itoe maelekezo au sheria itakayoshawishi kila viongozi wa elimu kuona sehemu ya uongozi wake, lazima kujiendeleza zaidi katika mafunzo ya uongozi, maana mafunzo haya yana uwezo mkubwa wa kuinua taasisi yake anayoiongoza kitaaluma zaidi, hivyo kila anayepangiwa kuongoza idara aweze kufika Adem kupigwa msasa wa uongozi,” alisema Dk Nguni.

Kwa upande wao, baadhi ya wahitimu wa chuo hicho walisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kupata mafunzo ya uongozi, ikiwamo kunyimwa ruhusa na viongozi wao kwenda kujiendeleza na wanapokuwa masomoni halmashauri na manispaa haziwalipii gharama za kukidhi mafunzo.

Zaidi ya wahitimu 100 wamepata mafunzo ya uongozi na kuahidi kuleta mabadiliko katika nyanja ya elimu, kuanzia ngazi za kata hadi mkoa ikiwamo kupambana na changamoto mbalimbali zilizopo.

No comments: