Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimeahidi kuendelea kupambana na serikali mpaka kihakikishe walimu wanalipwa zaidi Sh. bilioni 24 kama malimbikizo ya madai yao bila masharti yoyote kwa kuwa ni haki yao.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Rais wa CWT, Gratian Mukoba, alipozungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuanza kikao cha viongozi wa vyama vya walimu kutoka nchi mbalimbali.
Alisema serikali inadharau walimu na kuwaona kama watu, ambao hawana umuhimu na imeendelea kufanya hivyo licha ya watumishi hao kutaka kufanyika mazungumzo ya kumaliza tatizo hilo.
Aliitaka serikali kuacha mchezo wa kukimbia mazunguzo ya mezani na badala yake ikubali kukaa na walimu na kutatua kero zilizoanishwa kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma.
Kuhusu kuwapo tetesi kuwa kuna baadhi ya walimu wanaotaka kugoma mkoani Simiyu, alisema jambo hilo haliwezi kuepukika na kwamba, Mkuu wa Mkoa huo hana uwezo wa kuwazuia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vyama vya Walimu Duniani (EI), Fred Leeuwen, alisema, baadhi ya nchi zinawanyima haki walimu.
Rais wa Chama cha Walimu nchini Uganda (Unatu), Rwabushaija Margaret, alisema maslahi ya mwalimu ni muhimu na kwamba, hatua hiyo itasaidia kuboresha ubora wa mwalimu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment