Saturday, December 15, 2012

LOWASA AIBUA TUME YA ELIMU



Baada  ya kuvuma kwa muda mrefu na hadhari juu ya ukosefu wa ajira kwa vijana kuwa ni bomu linalosubiri kulipuka, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, ameibuka na pendekezo jipya la kusaidia sekta ya elimu nchini kwa kupendekeza kuundwa kwa tume ya elimu.

Akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) jijini Dar es Salaam jana, Lowassa alisema kuwa tume hiyo itaundwa na wataalam ili kuchunguza na kutathmini kama mfumo wa elimu nchini unaendana na hali ya sasa na mahitaji yake.

Alisema kuwa ni kosa kusema kuwa mitalaa ya elimu nchini haifai na kuongeza kuwa suala la msingi ni kuundwa kwa tume hiyo.

“Mimi nasema kuwa sasa wakati umefika kama Taifa kuunda tume ya elimu ili kuangalia na kupitia mfumo wote wa elimu, kuangalia mitalaa yetu kuanzia elimu ya awali mpaka vyuo vikuu, kuangalia ubora wa elimu hiyo, vitabu gani vitumike, hali ya maisha ya walimu, yaani kwa ujumla tuangalie upya kuhusu mfumo wa elimu yetu,” alisema Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM).

Alitoa mifano ya nchi zilizoendelea duniani kama Marekani kuwa zimekuwa zikifanya hivyo, na sasa kuna mchakato wa kuangalia elimu inayotolewa kama inaendana na changamoto za karne ya 21.

Akihutubia taifa hilo kubwa lenye nguvu baada ya kushinda uchaguzi wa urais mwezi uliopita, Rais Barrack Obama, alisema kuwa Marekani inakabiliwa na changamoto kubwa ya kujenga mfumo wa kuhakikisha uwekezaji unafanywa Marekani na siyo China ili kutengeneza nafasi zaidi za ajira.

Kauli hiyo ya Obama ilikuwa inajibu maswali ya wapinzani wake kwamba nafasi nyingi za ajira zimekuwa zikihamishiwa China kwa sababu mbalimbali, kama vile mfumo wa elimu, kodi na vivutio vya uwekezaji.

Kwa Tanzania kumekuwa na malalamiko mengi miongoni mwa wadau wa sekta ya elimu kwamba mitalaa ya elimu nchini haimwandai mwanafunzi kukabiliana na changamoto za maisha ya karne hii ikiwa ni pamoja na kuweza kujiajiri.

Hata hivyo, Lowassa aliipigia debe serikali ya awamu ya nne kuwa imepata mafanikio makubwa sana katika sekta ya elimu.

Alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni ujenzi wa shule za sekondari katika kata zote nchini kazi ambayo alipokuwa Waziri Mkuu kati ya Desemba 2005- Februari 2008 aliisimamia kwa nguvu zote.

“Mimi nilipata bahati ya kuongoza juhudi hizo za serikali kwa mafanikio makubwa kujenga shule hizo, lakini mafanikio hayo yamekuja na changamoto zake.”

“Tume hii itaangalia changamoto hizo zote na kutoa mapendekezo ambayo yatajadiliwa na wadau wa sekta hii katika kuboresha mfumo wa elimu nchini.”

Kadhalika, Lowassa aliweka wazi kuwa shule zinakabiliwa na changamoto kubwa kuwa ni ubora wa elimu inayotolewa na shule hizo, uhaba wa walimu, nyumba za walimu, maabara na vitendea kazi vikiwamo vitabu.

Alisema Tanzania ina bahati ya kuwa na wasomi waliobobea ambao wana uwezo wa kuangalia kama mitalaa inayotumika inakidhi haja na matakwa ya karne ya sasa.

CHANZO: NIPASHE

No comments: