Wednesday, December 26, 2012

BODI YA MIKOPO YAWADAI WATANZANIA WANAOISHI NJE SHILINGI BILIONI 51

Bodi ya Elimu ya Juu inadai zaidi ya Sh. bilioni 51 toka kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi, ambao walikuwa wakisoma vyuo mbalimbali hapa nchini kwa udhamini wa bodi hiyo.

Hayo yalibainishwa jana na Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa bodi hiyo, Cosmas Mwaisobwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Maonyesho ya Nanenane, mjini hapa.

Alisema ili kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa tayari mikakati imeshaanza kufanywa ikiwemo kuwasiliana na balozi za Tanzania ili kuanza kukusanya fedha hizo toka kwa watu hao. Alisema hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu jumla ya Sh. bilioni 4.2 zilikuwa tayari zimerejeshwa kutoka kwa baadhi ya watu ambao walikopeshwa na bodi hiyo kwa ajili ya masomo.

Hata hivyo, alisema bado kiasi hicho cha urejeshaji wa mikopo ni kidogo ikilinganishwa na fedha ambazo zimekopeshwa kwa watu mbalimbali kwa ajili ya masomo.

Mwaisombwa, alieleza kuwa ili kuhakikisha kuwa mikopo hiyo inarejeshwa, bodi imekuwa ikishirikiana na mawakala wa ukusanyaji madeni katika kanda mbalimbali hapa nchini ambao wamekuwa wakikusanya madeni hayo kwa wadaiwa waliopo ndani ya nchi.

Aidha, alisema kuwa bodi imekuwa ikishirikiana na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na mifuko ya hifadhi ya jamii kuwabaini watu ambao walikopeshwa na bodi hiyo lakini bado hawajaanza kurejesha mikopo hiyo.

Alieleza changamoto kubwa ambayo wamekuwa wakikabiliana nayo katika urejeshaji wa mikopo ni kushuka kwa thamani ya fedha kwa wakati ambao mikopo hiyo inarejeshwa kwa kuwa mikopo hiyo imekuwa haina riba.

Pia aliitaja changamoto nyingine kuwa ni kutopata ushirikiano toka baadhi ya waajiri, ambapo wamekuwa hawatoi ushirikiano ili kuhakikisha kuwa watumishi wao wanalipa madeni.

Kutokana na baadhi ya wakopeshwaji kutokuwa na utamaduni wa kulipa madeni, tayari bodi ya mikopo imeshaanza kuwaandikia baadhi yao barua za onyo na kutoza asilimia 5 zaidi ya deni kutokana na kuwa wazembe katika ulipaji wa mikopo hiyo.

No comments: