Baadhi ya wanafunzi wasioona wa shule ya msingi wanaotegemewa
kuingia katika mpango huu wakiingia sekondari
WANAFUNZI wasioona wa shule za sekondari nchini wataanza kusoma somo la Hisabati mwaka 2013.
Watapata masomo hayo baada ya walimu 20 kutoka katika shule za sekondari za wasioona kupatiwa mafunzo ya muda mfupi ya jinsi ya kufundisha somo hilo kwa kutumia nukta nundu.
Pia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imeandaa mipango endelevu ya Chuo cha Elimu maalumu cha Patandi na Chuo Kikuu cha Dodoma, viandae walimu wa Hisabati katika ngazi ya Stashahada na Shahada.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya ufundi, Philipo Mulugo alisema; “lengo ni kuwafanya wanafunzi wasioona wa shule za sekondari wafundishwe na kufanya mitihani ya hisabati kama wanafunzi wengine.”
Mipango mingine ya kuwawezesha kusoma hisabati inaandaliwa kupitia Shirika la International Council of Education for Visual Impared (ICEVI).
Shirika hilo limetoa kitabu kinachotoa mwongozo wa namna bora ya kufundisha somo la hisabati na Shirika la Sight Savers (SS) litatoa wataalamu wawezeshaji.
Kwa sasa somo la hisabati linafundishwa katika shule za msingi tu na hiyo inatokana na kuwepo kwa vitabu vilivyoandaliwa kwa nuktanundu na kuwepo kwa walimu wataalamu wanaoweza kufundisha somo hilo.
Mulugo alitoa maelezo hayo alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Margaret Mkanga (CCM) aliyetaka kufahamu lini Serikali itaacha kuwashusha daraja walemavu hao kutokana na kutofanya mtihani wa hisabati.
“Kuanzia mwaka 2009 watahiniwa wasioona waliomaliza kidato cha nne wenye ufaulu wa kuwawezesha kupata daraja la kwanza na la pili walitunukiwa daraja hilo japo walikuwa hawafanyi somo la hisabati kama kanuni inavyoelekeza.
“Baraza la mitihani walisitisha utaratibu huo ambao ulikuwa hauwatendei haki wasioona,” alisema Mulugo.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge huyo la kutaka kufahamu lini wanafunzi hao wasioona watafundishwa masomo ya sayansi sambamba na kwa vitendo, Mulugo alisema “hawa hawaoni tukiwapeleka maabara wataweza kushika kemikali wakaharibu macho yao”.
chanzo (habari leo)
No comments:
Post a Comment