Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, ameitaka serikali itoe tamko kuhusu wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na elimu ya juu ambao bado wako mtaani kwa kukosa ada.
Mnyika aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya darasa la saba katika Shule ya Mountain Hill.
"Naomba serikali itoe tamko kwa vijana hawa ambao wamefaulu vizuri kujiunga na vyuo vikuu lakini wanashindwa kwenda kwa sababu ya ada. Nakumbuka Rais alishasema kuwa hakuna mtoto wa maskini atakayeshindwa kusoma kwa sababu ya kukosa ada, Sasa hii leo mbona wamejaa mitaani?" Alihoji.
Aidha, Mnyika aliitaka serikali kuboresha mfumo wa huduma mbalimbali za kijamii ili mwanafunzi au mtu yeyote akikwama apate kwa kukimbilia.
Akijibu moja ya changamoto kubwa zinazoikabili shule hiyo ambayo ni wazazi kutolipa ada za wanafunzi kwa wakati, alisema nchi ina ugumu mkubwa wa maisha lakini wazazi wajitahidi kulipa ada hizo na waziweke kama ni jambo la lazima.
"Kama tunavyojua, nchi nzima kila mtu anazungumzia ugumu wa maisha na sekta hii ya elimu, nguvu ya umma na wadau wengine sio wa kutosha hivyo wazazi mtazame suala la kulipa ada kwa wakati kwa watoto wenu na kulifanya kama ni jambo la lazima kwani ni aibu kwa taifa ikiwa shule itakufa kwa sababu ya wazazi kutotimiza wajibu wenu na mkishindwa washirikisheni walimu," alisema Mnyika.
Mnyika aliongeza kuwa kwa ajili ya ukombozi wa taifa kwa ujumla, ni vyema kila shule ikaweka mkazo kwenye imani ya dini kama ambavyo shule hiyo inafanya.
Changamoto nyingine zinazoikabili shule hiyo ni pamoja na maji, umeme, maabara, bwalo la kulia chakula na madarasa.
No comments:
Post a Comment