Friday, November 25, 2011

KISWAHILI KITHAMINIWE!!


Na Gadi Solomon.
MTALAA wa elimu unaelekeza kwamba mwanafunzi wa kidato cha tatu lazima aanze kusoma vitabu kihakiki, lengo ikiwa ni kujaribu kupima mambo mbalimbali katika kazi za kifasihi pamoja na kubaini ubora na udhaifu uliojitokeza.
Pia, maandiko kama vile vijarida, vipeperushi na magazeti yanaweza kusomwa kihakiki na kuibua maarifa mapya.
Hivi sasa wanafunzi wengi husoma kihakiki ilimradi aweze kujibumaswali ya mtihani na kufaulu huku baadhi ya wanajamii wakijikita zaidi katika kusoma kazi mbalimbali zikiwamo hadithi.
Hata hivyo, tunapoadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika,  Watanzania hivi sasa tunapaswa kuangalia mfumo wa  elimu ya sasa, iwapo inawaandaa watoto wetu kukabiliana na changamoto za sasa na za baadaye katika ulimwengu huu ikiwa ni pamoja na kuwajengea ubunifu hasa katika uandishi wa vitabu.
Pia, katika kuhakikisha jamii inaepuka kuandikiwa vitabu na watu kutoka nje ya nchi kwa mambo yao yanayowazunguka, ambapo msingi unatakiwa kuwekwa ili kuhimiza wanafunzi na jamii kwa jumla kuhakikisha wanasoma kazi mbalimbali kihakiki.

Kwa kuzingatia jambo hilo jamii inabidi kuamka na kuangalia njia mbadala wa namna ya utoaji elimu ambayo itamsaidia mtoto hapo baadaye ili aweze kupenda kujisomea na kuandika mambo yanayomzungukana.
Ipo haja ya kutazama na kusawazisha mitalaa hii miwili ya elimu, baina ya mtalaa ule wa Kiswahili na zile shule Kiingereza,  kwa ngazi ya shule ya msingi.
Hii ni kutokana na wanafunzi wa shule maarufu kama ‘English Medium’ kuwa na ari ya kujisomea kwa kiasi  kikubwa, ukilinganisha na wale wanaosoma wa  shule za mtalaa wa Kiswahili ambapo msingi huo iwapo unafaa katika mbinu za kujisomea ni vyema  kila mwanafunzi akaupata, ili kuinua kiwango cha kujisomea.
Hata hivyo, yameelezwa mengi kuhusu suala la kushuka kwa kiwango cha kujisomea, ambapo hivi sasa kiwango hicho kinaelezwa kushuka mpaka kufikia asilimia 86 tangu taifa lipate uhuru.
Mathalan, uwiano wa vitabu na idadi ya wanafunzi shuleni bado ni ndogo, lakini kwa ngazi ya shule za sekondari ni muhimu wanafunzi wakaelewa umuhimu wa  kusoma vitabu kihakiki katika masomo yao mbalimbali, ili kuongeza kuibua mambo mapya kutikana na  yale ambayo hufundishwa darasani.
Pia, kwa ngazi ya chuo kusoma kihakiki ni suala la msingi ambalo chanzo chake ni kuibua maarifa mapya, ambayo yanaweza kumsukuma mwanafunzi kufanya tafiti za kina,  kutokana na kile alichoona kwamba hakijafanyiwa kazi na mtunzi hata kusababisha kuweza kuandika kitabu kwa manufaa ya jamii na kizazi kijacho.
Kwa mfano, katika muswada wa sera mpya ya elimu, jambo la msingi ni Watanzania kuithamini lugha ya Kiswahili na kuipa nafasi katika kutumika kufundishia kwa ngazi zote za elimu kama nilivyo jadili wiki iliyopita, ambapo kwa kufanya hivyo itatoa fursa kwa Watanzania kujieleza hata kwa kuandika mambo mbalimbali kwa lugha yao, wanayoielewa hivyo  kupata hazina ya vitabu mbalimbali kwa watoto na wakubwa, ziada na kiada.
Vilevile, katika kuhimiza maendeleo katika jamii, upo umuhimu wa kuhimiza wanafunzi na jamii kwa jumla kuacha kusoma vitabu kwa mtindo wa hadithi na kutambua umuhimu wa kusoma kazi kihakiki kwa ngazi mbalimbali za kitaaluma hususan sekondari na vyuo.
Hivi sasa Kiswahili kinatumika katika maeneo mbalimbali, wataalamu wa Kiswahili wanapaswa kutambua jamii hizo na kuweza kuandika mambo mbalimbali yanayohusu tamaduni zao kwa Kiswahili.m

(mwananchi) 25 november 2011
 

No comments: