Wednesday, December 28, 2011

2011: MWAKA ULIOSHUHUDIA ASILI,IA 80 YA WANAFUNZI WA KIDATO CHA NNE WAKIFELI VIBAYA

Kwa hisani ya gazeti la mwananchi

SIKU nne zijazo mwaka 2011 utafikia tamati.Nini kimejiri kuhusu elimu kwa mwaka mzima? Makala haya yanadurusu baadhi ya matukio muhimu ya kielimu yaliyotokea kuanzia Januari hadi Desemba mwaka huu.
Januari 26
Matokeo kidato cha pili    yatoka
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ilitoa matokeo rasmi ya mtihani wa kidato cha pili uliofanyika mwaka 2010, yakionyesha kushuka kwa ufaulu kwa asilimia 3.52 ikilinganishwa na mwaka 2009.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na wizara hiyo, watahiniwa 171,395 sawa na asilimia  38.20% walishindwa mtihani huo  wakiwamo wasichana 87,593 na wavulana 83,802.
Januari 27
Wasichana waongoza mtihani wa kidato cha nne
Siku moja baadaye, wizara hiyo hiyo ikatangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa  mwaka 2010  yaliyoonyesha wasichana kufanya vizuri kuliko wavulana.
Hata hivyo, huu ulikuwa mwaka  ulioanza na taarifa za kusikitisha kuhusu matokeo hayo, kwani  zaidi ya asilimia 80  ya watahiniwa walipata madaraja ya nne na sifuri, hali iliyochochea  mjadala wa kitaifa kuhusu mustakabali wa elimu nchini.
Machi 16
Wasichana wote wachaguliwa kidato cha tano
Wanafunzi wa kike wote waliofaulu kidato cha nne kwa kupata alama stahiki, walipangiwa kujiunga na kidato cha tano katika shule za sekondari na vyuo vya Serikali.
Aprili 28
Shule za Serikali zangara kidato cha sita
Siku hii ilikuwa siku nzuri kwa viongozi wa elimu serikalini baada ya shule zake za sekondari kung’ara katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2011, huku wanafunzi wake saba wakiwa miongoni mwa wanafunzi kumi bora kitaifa.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), Dk Joyce Ndalichako aliwataja wanafunzi 10 bora kuwa ni Muhagachi Chacha (Kibaha Sekondari), Samuel Katwale, George Felix (Mzumbe Sekondari), Amiri Abdalah, Comman Nduru na Kudra Baruti (Feza Boys), Aron Gerson,  Shaban Omary na Francis Josephat (Tabora Boys), George Assenga (Majengo Sekondari).
Juni 14
UDOM wasababisha taharuki Bungeni
 Taharuki kubwa  ilitawala katika viwanja vya bunge baada ya mabomu kusikika karibu  na ukumbi wa bunge ambapo kikao cha tatu katika mkutano wa nne wa Bunge kilikuwa kikiendelea.
Hali hiyo ilitokana na kitendo cha askari wa kuzuia vurugu wa Jeshi la Polisi, kupiga mabomu kwa ajili ya kuzuia Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma  waliotaka kuvamia ukumbi wa Bunge, ili  kuonana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Lengo la maandamano hayo ilikuwa kumshinikiza Waziri Mkuu,Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa wajiuzulu kwa kile walichodai kuwa wamewadanganya
Julai mosi
CWT yaitega Serikali
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba aliipa Serikali mwezi mmoja kuanzia Julai kuwalipa Sh13 bilioni wanazodai walimu vinginevyo ingetangaza mgomo wa  walimu  nchi nzima.
Hatua hiyo ilitokana na kikao cha dharura cha Baraza la Taifa la CWT, kilichofanyika Morogoro ili kujadili matatizo ya walimu.
Akizungumza na wanahabari, Mkoba alisema fedha hizo ni madeni yanatokana na malimbikizo ya mishahara na madai mengine.
Julai 19
Posho elimu ya juu yapanda
Kilio cha wanafunzi  wa elimu ya juu kilisikilizwa kwa kiasi fulani na Serikali baada ya   kukubali kuongeza kiwango cha fedha  za kujikimu kwa wanafunzi  hao kutoka Sh5,000 iliyokuwa ikilipwa awali mpaka Sh 7,500 kwa siku.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni Julai 19  na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk Shukuru Kawambwa, alipokuwa akisoma hotuba yake ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Wizara yake kwa mwaka 2011/12.
Kawambwa alisema kiasi cha Sh77.8 bilioni  kitatumika kuwapa posho wanafunzi 91,568 wa elimu ya juu wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo.Aidha, alisema kiasi hicho pia kinajumuisha posho kwa wanafunzi wanaosomea shahada za Uzamili na Uzamifu.

Septemba mbili

Maelfu wachaguliwa vyuo vikuu

Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) ilitangaza majina ya wanafunzi 37,924, ambao ni sawa na asilimia 69.3 waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu kwa mwaka 2011/12, kati ya wanafunzi 48,477 walioomba.

Wakati TCU ikitoa idadi hiyo ya wanafunzi waliochaguliwa, Bodi ya Mikopo ya Vyuo vya Elimu ya Juu (HELSB), nayo ikatangaza bajeti ya Sh317.8 bilioni zitakazotumika kwa ajili ya mikopo  kwa wanafunzi hao ambazo ni ongezeko la Sh 80 bilioni ikilinganishwa na Sh 237.8 bilioni  zilizotengwa mwaka 2010/11.

Oktoba
Maadhimisho wa miaka 50 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Sambamba na sherehe za uhuru wa Tanzania bara, Oktoba mwaka huu,   Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kiliadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1961.
Maadhimisho hayo  yaliyozinduliwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, yalifungwa na Rais Jakaya Kikwete pamoja Yoweri Kaguta Museven ya Uganda.
Awali tangu mwanzoni mwa mwaka, vitivo, vyuo, shule  na taasisi mbalimbali za chuo hicho kikongwe nchini,viliadhimisha  tukio hilo kwa kuandaa maonyesho ya aina mbalimbali, mihadhara na mijadala kwa umma.

Desemba 14
Udanganyifu darasa la saba
Desemba 14, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilitangaza matokeo ya mitihani ya darasa la saba ikieleza kuwa wanafunzi 9000 wamefutiwa matokeo kutokana na kugundulika kufanya udanganyifu.
Sambamba na hilo, akitangaza matokeo hayo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema Serikali imeamua kuwapima tena wanafunzi watakaopangiwa katika shule za Serikali ili pamoja na mambo mengine kuwabaini wanafunzi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Mulugo alisema wanafunzi waliofutiwa mtihani huo ni 9,736 na kuwa utaratibu wa kuchuja wale waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza utaanza rasmi Januari mwakani.

1 comment:

Anonymous said...

hi mposso1.blogspot.com blogger discovered your blog via search engine but it was hard to find and I see you could have more visitors because there are not so many comments yet. I have discovered site which offer to dramatically increase traffic to your site http://xrumerservice.org they claim they managed to get close to 1000 visitors/day using their services you could also get lot more targeted traffic from search engines as you have now. I used their services and got significantly more visitors to my site. Hope this helps :) They offer search engine rank optimization latest seo backlinks forum backlinks Take care. Jay