Saturday, November 19, 2011

UTARATIBU WA KUDAHILI WALIMU WABADILISHWA



UTARATIBU wa wanafunzi kuingia katika mafunzo ya ualimu katika vyuo vya serikali, sasa umebadilishwa ambapo badala ya kuchukuliwa kiujumla wanachukuliwa kutoka kila mkoa.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alisema lengo la kubadili utaratibu huo ni kuwafanya watoto wa mkoa husika wa mjini na vijijini wapate nafasi ya kusoma ualimu.

Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama (CCM), aliyesema ana ushahidi wa watoto wa vijijini kwa miaka miwili mfululizo wanaachwa kusomea ualimu wakati katika maeneo yao kuna uhaba wa walimu. Serikali ina vyuo vya ualimu 34 na pamoja na vya watu binafsi jumla vipo 103 kwa nchi nzima.

Akijibu swali la msingi la Mbunge huyo, aliyetaka kufahamu idadi ya wanafunzi waliomaliza sekondari kukosa nafasi ya kusomea ualimu wa Cheti na Stashahada kwa miaka miwili mfululizo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema mwaka 2011/2012 walioomba wenye sifa walikuwa 41,787 na waliochaguliwa walikuwa 17,722 sawa na asilimia 42.41.

Kati yao wanafunzi 7,138 wa ngazi ya Cheti walikwenda Vyuo vya Serikali na 10,594 walikwenda vyuo binafsi.

Waombaji wa mafunzo ya ualimu ngazi ya Stashahada waliokuwa na sifa walikuwa 10,345 na kati yao waliochaguliwa walikuwa 8,876 sawa na asilimia 85.79 .

Alisema katika uchaguzi huo, kwa wanafunzi wa ngazi ya cheti kipaumbele kimetolewa kwa waliofaulu masomo ya Hisabati, Sayansi na Kiingereza kwa kiwango cha ufaulu wa daraja la kwanza mpaka la nne (alama 28).

Alisema kwa upande wa Stashahada kipaumbele kimetolewa kwa wenye ufaulu wa kidato cha sita, daraja la tatu katika masomo yanayofundishwa katika shule za sekondari.

Naibu Waziri huyo alisema idadi ya waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya ualimu inazingatia nafasi zilizopo na bajeti iliyotolewa na serikali kuendesha mafunzo hayo.

No comments: