Friday, November 4, 2011

NI KWELI SHULE HIZI HAZIJULIKANI? WAHUSIKA WANAFANYA NINI?


Na Mdau wa Elimu
Juzi Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi aliifunga shule moja jijini Dar es Salaam iliyokuwa inaendesha shughuli zake kienyeji. Shule hiyo inadaiwa kuendesha shughuli zake kwa miaka 12 bila kusajiliwa.
Mbali na kutokusajiliwa, shule hiyo ambayo ni ya msingi na sekondari, pia haikuwa na walimu wenye vigezo vya ualimu, mazingira mabaya, majengo yasiyokuwa na hadhi ya kuitwa shule na haina hati miliki ya eneo ilipo kama sheria, kanuni na mwongozo wa serikali katika endeshaji wa shule vinavyoelekeza.
Hii ni shule ya pili kukutwa katika kadhia ya kutokutimiza vigezo vya kuitwa shule kwa mujibu wa taratibu za elimu nchini, wiki iliyopita Waziri huyo tena aliifunga shule nyingine jijini Dar es Salaam ambayo pia haikuwa na vigezo vya kuitwa shule; kibaya zaidi wanafunzi wa kidato cha nne waliokuwa wanasoma katika shule hiyo walishindwa kufanya mitihani licha ya wazazi wao kulipa ada za mitihani kwa mujibu wa ratatibu za Baraza la Mitihani la Taifa.
Fedha hizo za mitihani inaelezwa kuwa hazikufikishwa Baraza la Mitihani, na kwa maana hiyo wanafunzi hao hawakupata namba kwa ajili ya kufanya mitihani wa taifa wa kidato cha nne. Baadhi ya wazazi waliohojiwa juu ya watoto wao kushindwa kufanya mtihani, walisikitika na kulaani uongozi wa shule hiyo kwa kuendesha mambo kienyeji.
Hatua hizi zinachukuliwa na Naibu Waziri huyo wakati wakaguzi wa shule wako, lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kukabiliana na wimbi la shule za kiujanjaujanja zilizoanzishwa si kwa madhumini ya kutoa elimu, ila kama vitega uchumi vya watu wasiokuwa na huruma na watoto wa taifa hili.
Hata siku Waziri huyo anatangaza kuifunga shule hiyo wiki iliyopita baada ya kuitembelea, alipoulizwa juu ya kazi za wakaguzi wa shule, hakuwa na majibu ya kuridhisha hasa alipoelezwa kuwa kama hapa Dar es Salaam mbele ya macho ya wizara mambo yako hivi, je, huko mikoani hali itakuwaje na ni nini kazi na wajibu wa wakaguzi wa shule?
Hakika taifa linaloruhusu elimu ya watu wake ichezewe linajichimbia kaburi lenyewe na litajifukia humo ndani muda si mrefu, ni kwa jinsi hii tunasema hatua zinazochukuliwa na Naibu Waziri huyu ni za kuungwa mkono, ili kurejesha umakini na usimamizi thabiti katika mfumo mzima wa utoaji wa elimu kwa watoto wa taifa hili.
Ni kwa jinsi hii tunampongeza na kumuunga mkono kwa hatua hizi za kuzifungia shule za kibabaishaji, hata hivyo, kwa kuwa hizi ni juhudi binafsi, tungependa sasa kuona mfumo ukifanya kazi; wapo wakaguzi wa elimu wa wilaya, mikoa na kanda, hawa ni watumishi wa umma ambao wamepewa wajibu wa kusimamia ubora wa shule, tungependa kuona Waziri akiwafurusha watumishi hawa kwenda kufanya kazi walioyopewa na si kukaa ofisini kupiga domo wakati elimu ya watoto wa taifa hili inavurugwa.
Pamoja na juhudi hizi, tunajua Waziri amekwenda kwenye shule binafsi tu; zote mbili zilizofungwa jijini Dar es Salaam ni za watu binafsi, tunasema ni kuthubutu kuzuri, lakini tunajiuliza mbona hatuoni hatua kama hizi zikichukuliwa kwa shule za serilali? Tunajua, zipo shule nyingi za serikali, hasa za kata, ambazo zina matatizo makubwa pengine sawa na haya au kuliko haya yaliyobainika kwenye shule hizi mbili za Dar es Salaam.
Tumeona, kushuhudia na kusoma juu ya shule za sekondari za kata zenye mwalimu mmoja, zisizo na vifaa muhimu, na kwa kweli ambazo hazistahili kuitwa shule kwa maana ya sifa halisi ya shule. Na hizi tungependa kuona rungu za Waziri likishuka juu yake kwa kuwa wanaoathirika ni watoto wa Kitanzania kama hawa wanaoathirika kwenye shule hizi za watu binafsi.
Ni kwa kutambua juhudi hizi, tunamtaka waziri akaze kamba ili kurejesha uwajibikaji wa kweli katika uendeshaji, usimamizi na uratibu wa shule nchini kwa nia ya kuokoa elimu ya watoto wa taifa hili kwa ajili ya mustakabali mwema wa kizazi cha sasa na vile vijavyo. Hakika umma umechoshwa na ubabaishaji katika sekta za umma na sasa unataka uwajibikaji uliotukuka.

No comments: