Tuesday, November 1, 2011

ELIMU ISIGEUZWE BIDHAA - KIKWETE

RAIS Jakaya Kikwete, amesema elimu ni huduma na si bidhaa ya kuuzwa kwa bei ghali kama zinavyofanya baadhi ya shule binafsi nchini. Ameonya tabia ya baadhi ya shule kuwapa watoto wa Kitanzania elimu ya kigeni, yenye madhara ya kuwafanya Watanzania baadaye wawe wageni katika nchi yao. Rais pia ameishukuru sekta binafsi kwa kuitikia wito wa serikali wa kuitaka kuwekeza katika elimu ili kuunga mkono juhudi za kuimarisha na kusambaza elimu nchini.
Alisema hayo juzi katika mahafali ya 11 ya shule za sekondari za FEZA, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam. Rais Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, yaliyohudhuriwa na wahitimu, walimu, wanafunzi, wazazi na wafanyakazi wa shule hizo, aliishukuru sekta binafsi kwa mchango mkubwa katika utoaji elimu nchini. “Naishukuru sekta binafsi kwa mchango wao muhimu. Nawaomba muendelee kuwekeza katika hatua zote za utoaji elimu,” alisema. Hata hivyo, amezionya baadhi ya shule binafsi ambazo huongeza ada za masomo kupita kiasi.
“Natoa wito kwenu kuangalia upya mifumo yenu ya ada ili kuwawezesha wazazi wengi kuwaleta watoto katika shule. Elimu ni huduma si bidhaa kama zilivyo nyingine, ambazo faida ndicho kichocheo kikubwa cha kuwekeza,” alisema. Akizungumzia aina ya elimu inayotolewa katika baadhi ya shule binafsi, aliwaonya  wale wanaozigeuza kuwa viwanja vya kutolea elimu ya kigeni.
“Inaelekea katika baadhi ya shule kuna tatizo jipya la kutoa elimu ya kigeni kwa watoto wetu. Msiwapatie elimu ya kigeni. “Msiwafanye watoto wetu waje kuwa wageni katika nchi yao kwa sababu ya aina ya elimu wanayoipata katika baadhi ya shule zetu. Baadhi ya shule zimeanza kutoa elimu ya kigeni moja kwa moja,” alisema.

No comments: