.jpg)
Walimu wanaofundisha somo la Hisabati nchini ambao wanakutana mjini Iringa wamesema wazi kwamba matokeo ya somo hilo kwa mtihani wa taifa wa kumaliza elimu ya msingi, yatakuwa balaa kutokana na uamuzi wa serikali kupitia Baraza la Mitihani kutunga mtihani wa kuchagua jibu sahihi miongoni mwa majibu mengi.
Kauli ya walimu hao ilitolewa mbele ya Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kusisitiza kwamba kilichofanywa na serikali kwa kutungwa kwa mtihani wa namna hiyo hakika hautatoa picha halisi ya uelewa wa wanafunzi, na badala yake kutakuwa na ubahatishaji mwingi.
Huu ni utaratibu mpya wa kupima wanafunzi katika somo la Hisabati kwa mfumo wa majibu ya kuchagua badala ya utaratibu wa zamani wa kukokotoa kwa kuonyesha njia ya kufikiwa kwa jibu sahihi. Mfumo wa ukokotoaji ndio umekuwa ukitumika miaka na miaka katika ufundishaji wa somo hilo ambalo linakabiliwa na changamoto nyingi nchini.
Walimu hawa ndiyo wadau wakuu wa somo hili, hakika katika mazingira yanayofanya kazi vizuri isingewezekana kwa vyovyote vile serikali au chombo chochote cha kusimamia elimu nchini kufikia maamuzi mazito ya kubadili mfumo wa mitihani bila kushirikisha wadau wakuu. Katika suala hili, ni walimu wa Hisabati.
Tunasikitika kwamba kwa mara nyingine serikali imeruhusu majaribio mabaya kwa mfumo wa elimu ya watoto wa taifa hili, wakati ikijua fika kwamba juhudi za makusudi zinahitajika kuokoa elimu ya watoto wa taifa hili, hasa Hisabati na masomo mengine ya sayansi. Tunaungana na walimu hawa kuwa maamuzi ya kutumia mfumo mpya wa mtihani kwa somo la Hisabati ni janga linalostahili kudhibitiwa sasa kabla hatujafika mbali na gharama ya kurudi nyuma ikawa kubwa zaidi.
Ni jambo la kusikitisha kwamba mfumo wa elimu ya nchi hii hasa elimu ya msingi na sekondari imekuwa ni ya kufanyiwa majaribio mengi kama si masihara kwa vipindi mbalimbali. Imekuwa ni ada kila waziri anayeingia katika wizara hii kuja na mbwembwe zake; tunakumbuka mengi, lakini baadhi ni kama vile kuondolewa kwa masomo ya kilimo, uhasibu na ufundi katika mitaala wakati wa awamu ya tatu; kadhalika kufutwa kwa michezo shuleni na maamuzi mengine yanayofanana na hayo.
Baada ya wadau mbalimbali kupiga kelele, serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani ilibadili yote yaliyokuwa yamefanywa na waziri mtangulizi katika wizara hiyo; hata hivyo, nayo imeibuka na mbwembwe zake katika kutafuta njia ya kuongeza ufaulu kwa somo la Hisabati.
Tumekaa na kutafakari njia hii mpya ya kutaka kuongeza kiwango cha ufaulu kwa somo la Hisabati na kufikia hitimisho kwamba ni mkakati wa zima moto ambao umekosa mbinu za kisayansi kutatua tatizo; inajulikana wazi Hisabati halijawahi kuwa somo jepesi kwa wanafunzi kwa sababu moja kubwa, mbinu mbovu za ufundishaji wake lakini pia kukosekana kwa walimu waliobobea.
Tunajua kuwa serikali inaguswa na lawama ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake kwamba imeshindwa kutatua tatizo la kuporomoka kwa uelewa wa somo la Hisabati kwa wanafunzi wa taifa hili, na ni kwa sababu hiyo kwa mfano imekuwa na mikakati kama ya kutoa mikopo ya asilimia mia kwa wanafunzi wanaofanya vizuri masomo ya sayansi kujiunga na vyuo vya elimu ya juu; ni kweli mkakati huo unaweza kuwa kichocheo. Nasi tunaunga mkono juhudi hizo.
Kadhalika, serikali inajitazama na kutafakati hatua zaidi za kuongeza ufaulu kwa masomo hayo kuanzia ngazi ya elimu ya msingi kwa nia ya kwanza kuongeza idadi ya wanafunzi wa masomo hayo, lakini pia kuongeza kiwango cha ufaulu. Tunasema mikakati hiyo ni mizuri, lakini ni lazima iwe ya kisayansi inayozingatia uhalisia wa masomo husika na kupata maoni ya wadau wakuu wa somo lenyewe.
Itakuwa ni kujidanganya kwa watendaji serikali ama wenyewe au kwa kushinikizwa na wanasiasa kuibuka na mikakati kama hii ya kuwapima wanafunzi kwa majibu ya kuchagua tu kwenye somo la Hisabati bila kutoa mwanya wa kumpima mwanafunzi kama kweli anatambua anachokifanya katika somo hilo.
Tunaishauri serikali ijiepushe na mipango ya zima moto katika kukabiliana na changamoto zinazohitaji kujipanga vema kisayansi kutatua changamoto za elimu ya watoto wa taifa hili. Ni kwa jinsi hii tunaishauri kuwa isikilize maoni ya walimu wa Hisabati kwani wao ndio wadau wakuu wa somo hilo.
No comments:
Post a Comment