Wednesday, December 26, 2012

BODI YA MIKOPO YAWADAI WATANZANIA WANAOISHI NJE SHILINGI BILIONI 51

Bodi ya Elimu ya Juu inadai zaidi ya Sh. bilioni 51 toka kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi, ambao walikuwa wakisoma vyuo mbalimbali hapa nchini kwa udhamini wa bodi hiyo.

Hayo yalibainishwa jana na Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa bodi hiyo, Cosmas Mwaisobwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Maonyesho ya Nanenane, mjini hapa.

Alisema ili kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa tayari mikakati imeshaanza kufanywa ikiwemo kuwasiliana na balozi za Tanzania ili kuanza kukusanya fedha hizo toka kwa watu hao. Alisema hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu jumla ya Sh. bilioni 4.2 zilikuwa tayari zimerejeshwa kutoka kwa baadhi ya watu ambao walikopeshwa na bodi hiyo kwa ajili ya masomo.

Hata hivyo, alisema bado kiasi hicho cha urejeshaji wa mikopo ni kidogo ikilinganishwa na fedha ambazo zimekopeshwa kwa watu mbalimbali kwa ajili ya masomo.

Mwaisombwa, alieleza kuwa ili kuhakikisha kuwa mikopo hiyo inarejeshwa, bodi imekuwa ikishirikiana na mawakala wa ukusanyaji madeni katika kanda mbalimbali hapa nchini ambao wamekuwa wakikusanya madeni hayo kwa wadaiwa waliopo ndani ya nchi.

Aidha, alisema kuwa bodi imekuwa ikishirikiana na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na mifuko ya hifadhi ya jamii kuwabaini watu ambao walikopeshwa na bodi hiyo lakini bado hawajaanza kurejesha mikopo hiyo.

Alieleza changamoto kubwa ambayo wamekuwa wakikabiliana nayo katika urejeshaji wa mikopo ni kushuka kwa thamani ya fedha kwa wakati ambao mikopo hiyo inarejeshwa kwa kuwa mikopo hiyo imekuwa haina riba.

Pia aliitaja changamoto nyingine kuwa ni kutopata ushirikiano toka baadhi ya waajiri, ambapo wamekuwa hawatoi ushirikiano ili kuhakikisha kuwa watumishi wao wanalipa madeni.

Kutokana na baadhi ya wakopeshwaji kutokuwa na utamaduni wa kulipa madeni, tayari bodi ya mikopo imeshaanza kuwaandikia baadhi yao barua za onyo na kutoza asilimia 5 zaidi ya deni kutokana na kuwa wazembe katika ulipaji wa mikopo hiyo.

TUSIIME YAENDELEA KUONGOZA MATOKEO YA DARASA LA SABA DAR

Mkoa  wa Dar es Salaam umetoa matokeo yake ya waliohitimu darasa la saba mwaka huu ambapo shule ya Tusiime ya Tabata jijini Dar es Salaam imeongoza kwa Mkoa mzima wa Dar es Salam na katika Wilaya ya Ilala.

Shule hiyo ndiyo imekuwa ikiongoza matokeo ya mkoa na Wilaya ya Ilala tangu mwaka 2005.

Katika matokeo hayo wanafunzi kumi bora wa kike waliofanya vizuri wanatoka shule ya Tusiime na wavulana walioingia kumi bora saba wanatoka shule  hiyo.

Akitangaza matokeo hayo katika ofisi ya mkoa jana, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mbando akiwa na Ofisa Elimu wa Mkoa, Raymond Mapunda, aliwataja wanafunzi kumi bora wa kike kuwa ni Janeth Kijazi aliyepata alama 234 (Tusiime), Justina Kalalaa 234 (Tusiime), Kellen Mudogo 234 (Tusiime), Thecla Ngewe 231 (Tusiime), Stella Kagumila 230 (Tusiime), Asia Komba 229 (Tusiime), Grace Nyondo 226 (Tusiime), Praise Bagenda 226 (Tusiime), Lisa Magoti 225 (Tusiime) na Najima Majid 224 (Tusiime).

Kumi bora waliofanya vizuri kwa upande wa wavulana ni Jimmy Luhomvya 233 (Tusiime), Dule Mutagwaba 231 (Tusiime), Fray Seyumwe 231 (Tusiime), Maximillian Machage 229 Moga Kinondni,  Saad Mussa 229 (Tusiime), Gerald Kasamala 229 (Tusiime), Gift Kilupa 229 (Tusiime).

Wengine ni Joel Mutagwaba 228 (Tusiime), Shaban Kawaia 227 Mtoni Temeke na Alfred Shami wa shule ya msingi Mlimani.

Katibu tawala alisema waliofanya mitihani wa kumaliza la saba mwaka huu walikuwa 58,093  na waliofaulu mtihani huo ni 51,433 sawa na asilimia 88.5 na waliochaguliwa kujiunga na shule mbalimbali za sekondari ni 39,681.

Alisema wanafunzi waliofaulu mitihani ya kumaliza la saba mwaka 2011 walikuwa asilimia 79 wakati mwaka huu ni asilimia 88 hivyo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 10.

Akizungumzia matokeo hayo, Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mapunda aliipongeza shule ya Tusiime kwa kufaulisha wanafunzi wengi zaidi na kwa alama za juu.

“Walimu waliofanikisha wanafunzi hawa kufanya vizuri naomba wataambuliwe na uongozi ikiwezekana wapewe motisha na naomba manispaa ya Ilala nayo iwatambue kwa kufanya vizuri zaidi ili iwe motisha kwa wengine,” alisema Mapunda
.
 
CHANZO: NIPASHE

Saturday, December 15, 2012

MAAFISA ELIMU WASHITAKIWA KWA WIZI



JENGO LA HALMASHAURI YA MANISPAA YA ILALA

Kaimu Maofisa Elimu wanne wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Juhudi na Ukonga, jijini Dar es Salaam, wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kushindwa kufanya uhakiki wa mishahara ya walimu 23, kutumia madaraka vibaya na kuiba Sh. milioni 11.8 zikiwa ni mali ya serikali.

Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Agnes Mchome, Jana.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Allen Kasamala, aliwataja Makaimu Maofisa Elimu hao kuwa ni Elizabeth Thomas, Mercy Nyalusi na Joseph Kaika.

alimtaja Mwalimu Mkuu wa Shule hizo kuwa ni Simon Jerome na Clara Nyongeja aliyeajiriwa na Wizara ya Fedha kama mtaalamu wa kompyuta.

Inadaiwa kuwa mshitakiwa Elizabeth na Mercy hawakuweza kupanda kizimbani baada ya kuuguwa ghafla kazini kabla ya kufikishwa mahakamani.

Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mchome jana, Kasamala alidai kuwa Februari 2010, washitakiwa walitumia madaraka yao vibaya kwa kushindwa kufanya uhakiki wa masalia ya mishahara ya walimu 23 yenye thamani ya Sh. 11,825,000.

Kasamala alidai mashtaka sita yaliyobaki yote yanamkabili Mwalimu Jarome.

Alidai kwa kutumia madaraka yake vibaya, Machi Mosi, mwaka juzi alimlazimisha Mwalimu George Masinde wa Shule ya Msingi Ukonga ampe Sh. 3,900,000 katika masalia ya mishahara yake.

Kasamala alidai pia kuwa Machi 2, mwaka juzi, Jarome alimlazimisha Bahati Saidi, ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Ukonga ampe Sh. 3,895,000 kutoka katika masalia ya mishahara yake.

Alidai katika tarehe hiyo hiyo, Mwalimu Jerome alimlazimisha Mwalimu mwingine wa Shule hiyo, Ester Mdachi, ampe Sh. 4,030,000 kutoka katika masalia ya mishahara yake ili kujinufaisha.

Mwendesha mashtaka huyo alidai Machi 3, mwaka juzi, mshtakiwa huyo kwa kutumia madaraka yake vibaya alimlazimisha Mwalimu Mwaija Chowo wa Shule ya Msingi Ukonga atoe katika masalia ya mishahara yake Sh. milioni 3 ampe.

Alidai pia kuwa Jarome aliiiba Sh. 11,825,000 Machi 3, mwaka juzi, zikiwa ni mali ya serikali na kwa njia ya rushwa mshtakiwa huyo alijipatia Sh 3,000,000 kutoka kwa Mwaija Chowo ikiwa ni kishawishi cha kutomchukulia hatua kwa kukataa kumkabidhi masalia ya mishahara yake.

Washitakiwa wote walikana kutenda makosa hayo, upelelezi haujakamilika na Hakimu Mchome alikubali wadhaminiwe kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili, mmoja awe mfanyakazi katika ofisi inayotambulika na wasaini dhamana ya Sh. milioni 5.

Kasamala aliomba mahakama itoe hati ya kuwaita washitakiwa wasiofika mahakamani wafike ili wasomewe mashitaka yanayowakabili.

Hakimu alikubali kutoa hati hiyo, washitakiwa waliofikishwa mahakamani walidhaminiwa na kesi iliahirishwa hadi Oktoba 24 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

CHANZO: NIPASHE

LOWASA ASEMA ELIMU YA SEKONDARI SASA IWE BURE




Waziri  Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, amesema wakati umefika sasa elimu ya sekondari iwe bure ili kumwondolea mwananchi mzigo.

Lowassa aliyasema hayo jana mjini Babati kabla ya kuendesha harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Babati.

Alisema kwa sasa kila kata hapa nchini ina shule ya sekondari na huo ulikuwa mpango wake akiwa Waziri Mkuu na alisimamia na kufanikiwa kwa asilimia 100.

''Ni lazima tukubali na tujadili suala hilo kwa manufaa ya nchi kwa kila Mtanzania kukubali ushauri huo wa elimu ya sekondari kuwa ya bure," alisisitiza.

Aliongeza kuwa serikali inapaswa kugharimia elimu ya sekondari bila woga na mwananchi anapaswa kuchangia mahitaji mengine ikiwemo kupata elimu ya kilimo kwanza kwani kilimo ndiyo uti wa mgongo wa nchi.

Aidha, Lowassa alisema wito wa Rais Jakaya Kikwete, wa shule za sekondari kujenga maabara kwa wingi, unapaswa kuungwa mkono pia na kila Mtanzania.

WALIMU WATATU WAPATA AJALI




Baadhi ya madaktari wakiwajibika katika Hospitali ya KCMC Moshi.

Walimu  watatu na walezi wawili wa wanafunzi katika shule ya Scolastica iliyopo eneo la mji mdogo wa Himo, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamefariki katika ajali mbaya ya gari mjini humo.

Katika ajali hiyo iliyotokea, pia walimu wanane wamejeruhiwa, baadhi vibaya na wengine kupata majeraha madogo madogo na kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi na
kuruhusiwa.

Ajali hiyo ilitokea Disemba 10, mwaka huu, majira ya saa 2:30 usiku, wakati walimu na walezi hao wakitoka kwenye mazishi ya mwanafunzi wa kidato cha tatu wa shule hiyo, Jackson Kisiri, aliyefariki kwa kugongwa na pikipiki eneo la Kwa Mrefu wilayani Arumeru, mkoani Arusha.

Akizungumzia suala hilo mara baada ya kupatiwa matibabu na kuruhusiwa katika hospitali ya KCMC, Mkuu wa shule hiyo, Marko Shiloli, alisema kwenye gari hilo kulikuwa na walimu kumi, walezi wawili na dereva na kwamba walimu watatu walifariki katika eneo la tukio na walezi hao walikutwa na mauti wakiwa KCMC.

Alisema mwanafunzi huyo alifariki wakati akiwa likizo nyumbani kwao na kwamba walimu na walezi hao walikwenda kwenye mazishi yaliyofanyika Disemba 10, mwaka huu nyumbani kwao.

Kamanda wa Polisi Mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, hata hivyo alisema chanzo halisi hakijafahamika.

Alisema gari lililokuwa na walimu hao lilikuwa likitokea mkoani Arusha kwenda Himo.

Kamanda Boaz alisema ajali hiyo ilihusisha gari lenye namba za usajili T 771 AQD mali ya shule hiyo lililokuwa linaendeshwa na Alexanda Mosha (54), ambalo liligongana ubavu wa kulia na lori aina ya Fuso lenye namba za usajili T 212 AHH likiwa na tela lenye namba za usajili T 653 AAJ likiendeshwa na Omar Abdalah (37).

Alisema ajali hiyo ilitokea karibu na mto Kikavu Chini mahali yalipo makaburi ya raia wa Japan wilayani Hai na kwamba dereva wa gari la shule ya Scolastica anaendelea na matibabu hospitalini.

Mkuu wa shule hiyo aliwataja walimu waliofariki kuwa ni, Julius Kimario (28) wa masomo ya Kiingereza na general study, Joseph Leon Okolot raia wa Kenya wa somo la Historia aliyefariki wakati akifanyiwa upasuaji kutokana na kuvuja damu nyingi na Bernard Amukunyo (30) wa masomo ya Jiografia na Historia raia wa Kenya.

Wengine waliofariki ni Ernest Ambani (48) mlezi wa wanafunzi wa kiume na Nelly Sasaka Deruya raia wa Kenya ambaye alikuwa mlezi wa wanafunzi wa kike shuleni hapo.
CHANZO: NIPASHE

MPAMBANO NA SERIKALI BADO PALEPALE - CWT



Chama  cha Walimu Tanzania (CWT) kimeahidi kuendelea kupambana na serikali mpaka kihakikishe walimu wanalipwa zaidi Sh. bilioni 24 kama malimbikizo ya madai yao bila masharti yoyote kwa kuwa ni haki yao.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Rais wa CWT, Gratian Mukoba, alipozungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuanza kikao cha viongozi wa vyama vya walimu kutoka nchi mbalimbali.

Alisema serikali inadharau walimu na kuwaona kama watu, ambao hawana umuhimu na imeendelea kufanya hivyo licha ya watumishi hao kutaka kufanyika mazungumzo ya kumaliza tatizo hilo.

Aliitaka serikali kuacha mchezo wa kukimbia mazunguzo ya mezani na badala yake ikubali kukaa na walimu na kutatua kero zilizoanishwa kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma.

Kuhusu kuwapo tetesi kuwa kuna baadhi ya walimu wanaotaka kugoma mkoani Simiyu, alisema jambo hilo haliwezi kuepukika na kwamba, Mkuu wa Mkoa huo hana uwezo wa kuwazuia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vyama vya Walimu Duniani (EI), Fred Leeuwen, alisema, baadhi ya nchi zinawanyima haki walimu.

Rais wa Chama cha Walimu nchini Uganda (Unatu), Rwabushaija Margaret, alisema maslahi ya mwalimu ni muhimu na kwamba, hatua hiyo itasaidia kuboresha ubora wa mwalimu.



CHANZO: NIPASHE

LOWASA AIBUA TUME YA ELIMU



Baada  ya kuvuma kwa muda mrefu na hadhari juu ya ukosefu wa ajira kwa vijana kuwa ni bomu linalosubiri kulipuka, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, ameibuka na pendekezo jipya la kusaidia sekta ya elimu nchini kwa kupendekeza kuundwa kwa tume ya elimu.

Akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) jijini Dar es Salaam jana, Lowassa alisema kuwa tume hiyo itaundwa na wataalam ili kuchunguza na kutathmini kama mfumo wa elimu nchini unaendana na hali ya sasa na mahitaji yake.

Alisema kuwa ni kosa kusema kuwa mitalaa ya elimu nchini haifai na kuongeza kuwa suala la msingi ni kuundwa kwa tume hiyo.

“Mimi nasema kuwa sasa wakati umefika kama Taifa kuunda tume ya elimu ili kuangalia na kupitia mfumo wote wa elimu, kuangalia mitalaa yetu kuanzia elimu ya awali mpaka vyuo vikuu, kuangalia ubora wa elimu hiyo, vitabu gani vitumike, hali ya maisha ya walimu, yaani kwa ujumla tuangalie upya kuhusu mfumo wa elimu yetu,” alisema Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM).

Alitoa mifano ya nchi zilizoendelea duniani kama Marekani kuwa zimekuwa zikifanya hivyo, na sasa kuna mchakato wa kuangalia elimu inayotolewa kama inaendana na changamoto za karne ya 21.

Akihutubia taifa hilo kubwa lenye nguvu baada ya kushinda uchaguzi wa urais mwezi uliopita, Rais Barrack Obama, alisema kuwa Marekani inakabiliwa na changamoto kubwa ya kujenga mfumo wa kuhakikisha uwekezaji unafanywa Marekani na siyo China ili kutengeneza nafasi zaidi za ajira.

Kauli hiyo ya Obama ilikuwa inajibu maswali ya wapinzani wake kwamba nafasi nyingi za ajira zimekuwa zikihamishiwa China kwa sababu mbalimbali, kama vile mfumo wa elimu, kodi na vivutio vya uwekezaji.

Kwa Tanzania kumekuwa na malalamiko mengi miongoni mwa wadau wa sekta ya elimu kwamba mitalaa ya elimu nchini haimwandai mwanafunzi kukabiliana na changamoto za maisha ya karne hii ikiwa ni pamoja na kuweza kujiajiri.

Hata hivyo, Lowassa aliipigia debe serikali ya awamu ya nne kuwa imepata mafanikio makubwa sana katika sekta ya elimu.

Alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni ujenzi wa shule za sekondari katika kata zote nchini kazi ambayo alipokuwa Waziri Mkuu kati ya Desemba 2005- Februari 2008 aliisimamia kwa nguvu zote.

“Mimi nilipata bahati ya kuongoza juhudi hizo za serikali kwa mafanikio makubwa kujenga shule hizo, lakini mafanikio hayo yamekuja na changamoto zake.”

“Tume hii itaangalia changamoto hizo zote na kutoa mapendekezo ambayo yatajadiliwa na wadau wa sekta hii katika kuboresha mfumo wa elimu nchini.”

Kadhalika, Lowassa aliweka wazi kuwa shule zinakabiliwa na changamoto kubwa kuwa ni ubora wa elimu inayotolewa na shule hizo, uhaba wa walimu, nyumba za walimu, maabara na vitendea kazi vikiwamo vitabu.

Alisema Tanzania ina bahati ya kuwa na wasomi waliobobea ambao wana uwezo wa kuangalia kama mitalaa inayotumika inakidhi haja na matakwa ya karne ya sasa.

CHANZO: NIPASHE

Friday, February 10, 2012

THE BEST FORM FOUR STUDENT IN TANZANIA



THE BEST FORM FOUR STUDENT IN TANZANIA CONGRATULATIONS -
NUMBER: S0189/0039

NAME: MOSES ANDREW SWAI

RANK: FIRST POSSITION

POINT (7) DIVISION I

CIV-A
HIST  -A
GEO  -A
KISW  -A
ENGL  -B
PHY  -A
CHEM  -A
BIO  -A
COMP STUD-B
B/MATH   -A

FROM FEDHA BOYS...

''WALIMU WAPYA MANISPAA YA KINONDONI TUNATESEKA''

SISI walimu kutoka mikoa mbalimbali ya hapa nchini, tuliopangwa kufanya kazi katika manispaa ya Kinondoni mpaka sasa hatujalipwa fedha zetu za kujikimu.

 Tangu tumefika hapa Februari Mosi, hatujapewa fedha zozote, hatuna pa kulala, wala pa kula, ukizingatia kuwa wengine hatuna ndugu hapa jijini.

Kwa mfano hivi majuzi baada ya kufika hapa Manispaa ili watupe posho zetu wanatuambia hawafanyi kazi walijua ni siku kuu ya Maulid. Kweli wanakosa huruma kiasi hiki wakati sisi tungali katika maisha magumu.

 Hawajui tunaishi wapi, tunakula nini wala tunapata usafiri kwa njia gani.
Tunaomba serikali itusaidie, kama kweli wanamthamini mwalimu, basi watuokoe katika jahazi hili la tabu.

Tunataka tulipwe posho zetu zote, kama ambavyo walimu wengine walikuwa wakilipwa.

Walimu Wapya,
 Manispaa ya Kinondoni,
Dar es Salaam.

MWANANCHI

WALIMU WAPYA DODOMA WALIPWA POSHO ZAO

Hamisi Mwesi, Dodoma
HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma, imetumia Sh54 milioni kulipa posho za walimu 133 wa shule za sekondari waliopangiwa kufanya kazi katika halmashauri hiyo.

Juzi walimu hao wapaya waliandamana kwenda katika viwanja vya bungeni kushinikiza kulipwa posho hizo.

Jana mwandishi wa habari hizi, alishuhudia mkusanyiko wa idadi kubwa ya walimu hao katika ofisi za elimu ya sekondari za halmashauri ya manispaa hiyo, wakisubiri kulipwa fedha zao.

Kulipwa kwa posho hizo ni utekelezaji wa ahadi iliyokuwa imetolewa na uongozi wa manispaa hiyo ya kulipwa walimu fedha hizo jana.

 Kaimu Ofisa Elimu wa Shule za Sekondari katika Manispaa ya Dodoma, Suma Mwampulo, alisema fedha hizo ni kwa ajili ya posho ya kujikimu kwa siku saba na nauli walizotumia kutoka makwao kwenda katika manispaa hiyo.

 “Tumetumia zaidi ya Sh54 milioni kuwalipa walimu hawa 133 posho zao za kujikimu kwa siku saba na nauli walizotumia kutoka makwao kuja Dodoma,” alisema Mwampulo.

Alisema walimu hao wamepangwa katika shule mbalimbali za manispaa hiyo na kwamba wameajiri hivi karibuni, katika jitihada za Serikali za kupunguza tatizo la upungufu wa walimu katika shule za sekondari hasa za kata.

“Tunaishukuru serikali kwa kusikiliza kilio chetu lakini bado kuna upungufu katika baadhi ya shule tunazidi kuiomba Serikali iajiri walimu zaidi ili kumaliza kabisa tatizo la walimu nchini, ”alisema Mwampulo
Pia aliwataka walimu hao kuwa wavumilivu katika utendaji wao na kukubali kuwa na moyo wa kujitolea katika kuitumikia nchi yao.

Habari kwa hisani ya gazeti la mwananchi

MWANAFUNZI AZIMIA NDANI YA INTERNET CAFEE BAADA YA KUGUNDUA AMEFELI VIBAYA

Mmwanafunzi mmoja aliyejulikana kwa jina la sikudhani kibwana ameanguka na kuzirai mara baada ya kugundua kuwa amefeli vibaya. hayo yametokea katika internet cafee moja inayopatikana pembeni mwa uwanja wa jamhuri morogoro
Binti huyo ambae ni mwanafunzi wa shule ya sekondari morogoro alipatwa na kadhia hiyo mara tu alipojigundua kuwa katika kundi walilopo ni pekee ndie aliyefeli vibaya kwa habari za picha mcheki hapa chini

 hapa mwanafunzi mwenzake ambae walikuwa wote akimsubiri mwenzake aghalabu apate nafuu waondoke

                        Taratiibu akipata nafuu masikini pole SIKUDHANI rudia mtihani mungu atakusaidia

PICHA KWA HISANI YA GLOBAL PUBLISHERS

Saturday, January 21, 2012

SHULE YA SEKONDARI NANENANE MABATI ''PURUKUCHU'' SHULE YASIMAMA KWA MUDA WA SIKU KADHAA KUSUBIRI UJENZI UKAMILIKE TENA




paa ambalo liliruka kutoka kwenye madarasa mawili na kurushwa mpaka karibu na ofisi za mwalimu mkuu likioneakna kwa mbali ambapo lilikwenda kugonga nguzo ya bendera ya taifa na kuivunja bendera hiyo na ndio ikawa salama ya kuleta uharibirfu kwenye maeneo mengine

mwalimu mkuu wa shule ya nanenane sekondari Mwal Irine Dimoso akiahirisha masomo kwa wanafunzi wa shule hiyo kutokana na matatizo yaliyotokea shuleni hapo ya kuezuliwa kwa mabati ya shule hiyo na mvua zilizoambatana na upepo mkali sana ulioleta madhara hayo, bahati kadhia hiyo haikumdhuru mtu

MAANDAMANO YA UMOJA WA WANAFUNZI WA KIISLAMU MOROGORO, BAADHI YA WANAFUNZI WAUMIA KWA TAFRANI ZA MABOMU







Thursday, January 19, 2012

SERIKALI YAFANYA KWELI AJIRA ZA WALIMU WAPYA HIZOOOOOOO

Serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania jana iliweka majina ya walimu waliofanya vizuri na kuajiriwa katika shule mbalimbali, walimu hao wanatakiwa kuwa wawe tayari wamekwisharipoti katika vituo vyao vya kazi mpaka itakapofikia katikati ya mwezi wa pili na hii ni kwa maelezo ya kwamba ikiwa hukufika mpaka muda huo katika kituo chako cha kazi ni kwamba umejiondoa mwenyewe

Hivyo shima walimu wapya tuchangamkie ajira kabla serikali haijabadili maamuzi ya kukupa nafasi hiyo na pia tufanye kazi kwa bidii ikiwezekana kwenye kuongeza taaluma na tuongeze , kwenye kupongezana tupongezane na kwenye kudai haki zetu basi tuungane tudai.

kwa maelezo zaidi  tembelea www.moe.co.tz

AHSANTE, ni mimi MWANAMAPINDUZI

 

Saturday, January 7, 2012

KAMBI ZA WAATHIRIKA ZATIWA KUFULI

Joseph Zablon
SERIKALI imetangaza kuzifunga kambi rasmi 15 zilizokuwa zikitumika katika kuwahifadhi watu waliokumbwa na mafuriko, yaliyotokana na mvua zilizonyeshwa mwishoni mwa mwezi uliopita, jijini Dar es Salaam.  Hatua hiyo inalenga katika kutoa nafasi kwa wanafunzi wa shule zilizotumika kwa shughuli za kambi hizo, kuanza masomo baada ya shule hizo kufunguliwa rasmi Jumatatu ijayo.

Kufungwa kwa kambi hizo, kulitangazwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadick ,ambaye alisema kambi hizo zilifungwa jana jioni.  Sadick alisema hatua hiyo imekuja wakati maandalizi kuhusu makazi mapya kwa ajili ya watu hao, yakiwa yamekamilika.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kwa msingi huo, kuanzia leo wananchi waliokumbwa na mafuriko, hawapaswi tena kuonekana katika kambi hizo.

Alisema badala yake,  wanapaswa kuhamia katika  eneo la viwanja vyao vilivyopo Mbweni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.  Alisema hata hivyo, viwanja hivyo ni kwa ajili ya watu waliokuwa wanamiliki nyumba zilizoathiriwa na mafuriko katika maeneo ya mabondeni. Kuhusu wapangaji, alisema wanapaswa kutafuta nyumba zingine za kupanga katika maeneo mbalimbali salama, kama ilivyoagizwa na Serikali.

 "Mbweni na kwingineko ni kwa ajili ya watu waliokuwa wanamiliki nyumba mabondeni na wale ambao walikuwa wapangaji wanapaswa kutafuta nyumba katika maeneo mengine na hilo tuliishawatangazia" alisema Sadick.   Kuhusu watoto wanaosoma, Mkuu wa mkoa alisema  watapatiwa nafasi katika shule za jirani na eneo wanakohamia wazazi wao.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, tayari Serikali imeshawataka  wazazi kushughulikia uhamisho wa watoto hao kutoka katika  ofisi za elimu za wilaya ambazo nazo zimetakiwa kuondoa urasimu katika kushughukilia uhamisho huo.
"Tumewaagiza waondoe urasimu na kuwapa watoto uhamisho wa haraka ili  waweze kuendelea na msomo wakati mipango inafanywa ya kuongeza vyumba vya madarasa katika shule wanazokwenda,” alisema Mkuu wa mkoa

kwa niaba ya gazeti la MWANANCHI

MADENI YASIYOLIPWA SHULE HAZIFUNGULIWI ASEMA MKOBA

Gedius Rwiza
MVUTANO kati ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na Serikali ,kuhusu malipo ya madeni ya walimu, unaonekana kushika kasi baada ya Rais wa chama hicho, Gratian Mukoba, kupinga kauli ya Serikali kwamba wamekubaliana kusitisha mgomo wa walimu uliopangwa kufanyika Januari 9 mwaka huu.

Jana Naibu Waziri Tamisemi anayeshughuliki Elimu, Kasim Majaliwa aliliambia gazeti hili kuwa mgomo huo umesitishwa baada ya Serikali kukutana na viongozi wa CWT Desemba 25 mwaka jana na kukubaliana wafanye hivyo.

Hata hivyo kwa upande wake, Mukoba alipinga kauli hiyo ya waziri.“Ni kweli tulikutana na Serikali lakini sisi hatukukubali kusitisha mgomo kwa sababu madai yetu hayajatekelezwa," alisema Mukoba.

Alisema Serikali imekiuka makubaliano kwamba fedha za walimu zingelipwa kati ya Novemba na Desemba mwaka jana.Huko nyuma Serikali ilikuwa imekubaliana na CWT, kwamba fedha hizo kiasi cha Sh49.6 bilioni zingelipwa katika Novemba na Desemba lakini baada ya kufanya tena uhakiki ilibaini kuwa fedha hizo zimeongezeka hadi kufikia Sh52 bilioni.

Uhakiki huo ulikamilika Desemba 2 mwaka jana baadaye Serikali ilitangaza kuwa fedha hizo zitalipwa kwa awamu mbili,Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Ufundi, Selestin Gisimba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, sababu za kusogeza mbele malipo hayo ni kutaka kufuata utaratibu wa makato ya kodi ikiwemo mifuko ya hifadhi  ya jamii kwa kupitia katika akaunti zao.

“Tumeishagundua ujanja wa Serikali wamefanya makusudi kusogeza siku mbele ili walimu wafungue shule na mgomo uyeyuke lakini napenda kusema kwamba tayari ujanja huo tumeufahamu na kama ikishindwa kulipa fedha hizo mwezi huu shule hazifunguliwi,”alisema Mukoba.

Alisema kwa sasa makubaliano hayo hayawezi kubadilika kwa sababu suala la uhakiki limeishamalizika na kwamba kinachotakiwa ni kulipa fedha za walimu.

habar kwa niaba ya gazeti la MWANANCHI

Tuesday, January 3, 2012

WAMETHUBUTU, WAMEWEZA NA WANASONGA MBELE

TAARIFA YA GROUP MPYA YA ''WALIMU TANZANIA'' NDANI YA FACEBOOK

 Walimu Tanzania ni kundi huru lenye lengo la kuwaweka pamoja walimu nchini, kutoa elimu, taarifa zinazohusu au kuathiri sekta ya elimu, kukosoa, kupongeza, kujadili, na hatimaye kuwa jukwaa huru zaidi ya yaliyopo mpaka sasa. Imethibitika kuwa Serikali, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (MOEVT), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Maafisa Elimu Madaraja ya Uteuzi na Chama Walimu Tanzania (CWT), wanashirikiana kudidimiza sekta ya walimu hususani walimu kulingana na mapunngufu mengi yaliyopo ambayo yanatuweka nyuma ya maendeleo ya dunia katika elimu.

Tunaamini kuwa changamoto zinazotukabili katika kufanikisha kuundwa kwa taasisi, mabalaza, mikusanyiko na mikakati madhubuti na endelevu ya kutoa elimu kwa walimu na jamii katika kuwania mabadiliko ya kweli ni nyingi sana. Weledi wetu unatuwezesha kupata ufahamu zaidi, kufanya mipango zaidi, kuchanganua harakati zetu zaidi, kujirtekebisha mapena tutakapokosea na hatimaye kuwa na majukwaa huru kutoka katika jamvi hili adhimu.

Kwa kuwa sekta ya elimu inajengwa na watu wenye uwezo wa kuleta mabadiliko katika sekta nyingine zote nchini. Miongoni mwa ale wanaridhika na mwenendo wa viongozi walio juu yetu kimamlaka ni wanaopokea mishahara minono, posho kubwa na kutumia rasilimali zinazotokana na kodi za wananchi ikiwamo magari. Wengine wanaoingia katika kundi hili la wachache ni walimu wasiojua haki zao kisheria, waoga, wanafiki, na wasiohitaji mabadiliko ya kweli. Mabadiliko yanayozuiwa kupatikana kutokana na ushabiki wao, upenzi wao na kuwasujudia viongozi wao wanaowatisha mithiri ya watoto wadogo na waliopoteza mika mingi katika taasisi mbalimbali za elimu walizopitia kwa kukariri.

Kwa kutumia uzoefu wa masuala yaliyoangamiza, kusambaratisha au kutokomeza kabisa makundi, asasi, na makusanyiko mengine mbalimbali. Walimu Tanzania itasimama imara dhidi ya kiongozi, muwakilishi au mshikadau yeyote atakayethubutu kutumia itikadi za udini, ukabila, ukanda, uchama wa chama chochote cha siasa, undugu, unafiki, au kusudio lolote la siri au bayana kuvuruga kusanyiko hili. Wote tunatambua kuwa kila mtu yupo huru kwa kuishi anavyopenda kwa mujibu wa vitabu vitabu vitakatifu vya Mwenyezi Mungu, Misingi ya Kitamaduni, Sheria za kimataifa na za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au kadiri mja anavyokubali kuwa ni misingi sahihi kutawala maisha yake. Hivyo uanzishaji na kuchangia mada, ushauri, kukosoa kwa ushahidi, kuelimisha au kuboresha mikakati, mipango, mbinu za kufanikisha maazimio mbalimbali, utendaji kwa ujumla uakisi lengo kuu la kuwaunganisha walimu katika kupambana na changamoto zinazoikabili sekata ya elimu. Wataalamu wengine pia wana haki ya kushirikishwa lakini iwe katika kufanikisha harakati hizi ambazo kamwe hazitofutika kwa vitisho, husda, au uharamu wowote.

Nitoe rai kwa wadau wote sasa kuongeza nguvu maradufu kuongeza wadau wengine zaidi lakini pia wasisahau kutoa utambulisho mfupi kwa kila mdau wanayewania kumpa nafasi ya kujumuika nasi katika kundi.

Ahsanteni kwa ushirikiano,

Lukinga,A (kwa niaba ya)
Ficky, M. na
Mkoba, A."

TUBURUDIKE KIDOGO KWA WALE TUNAOKIKUMBUKA KITABU HIKI



unaikumbuka hii?

haya tuburudike kidogo basi.

SIZITAKI MBICHI HIZI
1. Hadithi inayokuja, ni ya Sungura sikia,
    Hadithi uliyongoja, leo ninakuletea,
    Alitoka siku moja, njaa aliposikia,
    Njaa aliposikia, Sungura nakuambia.
2. Siku ile akaenda, Porini kutembelea,
    Akayaona matunda, mtini yameenea,
    Sungura akayapenda, mtini akasogea,
    Mtini akasogea, Sungura nakuambia.
3. Sungura karukaruka, lakini hakufikia,
    Matunda hakuyashika, mikononi hakutia,
    Hakika alisumbuka, nguvuze zikapungua,
    Nguvuze zikapungua Sungura nakuambia.
4. Mtazame hapo juu Sungura amelegea,
    Mtazame na miguu, matunda anarukia,
    Atafanya sikukuu, matunda akifikia,
    Matunda akifikia, Sungura nakuambia.
5. Karuka tena karuka, matunda akarukia,
    Mwisho wake akachoka, kachoka hata mkia,
    Penye mti akatoka, pembeni akasogea,
    Pembeni akasogea, Sungura nakuambia.
6. “Sizitaki mbichi hizi” Sungura akagumia,
    “Naona nafanya kazi, bila faida kujua”,
    Yakamtoka machozi matunda akalilia,
    Matunda akalilia, Sungura nakuambia...